INGAWA si kawaida, lakini naomba nianze makala yangu na hitimisho, badala ya utangulizi. Kwamba pendekezo la mfumo wa Muungano wenye Serikali tatu (Shirikisho), la Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, ndiyo mfumo sahihi unaotakiwa chini ya Mkataba wa Muungano, uliotiwa sahihi na waasisi wake, Mwalimu Julius Nyerere wa Tanganyika na Sheikh Abeid Amani Karume wa Zanzibar, Aprili 22, 1964.
Kwa mantiki hiyo, ilichofanya Tume ya Jaji Warioba, si kupendekeza mfumo mpya, bali ni kurejesha mfumo sahihi uliovurugwa kibabe tofauti na kile kilichokusudiwa chini ya Muungano huo, kama tutakavyoona katika makala haya.
Kwa hili, hakuna kipya kilichoanzishwa na Tume, mbali na kutukumbusha tu kile kilichokusudiwa chini ya Muungano huo wa nchi mbili hizo.
Mkataba wa kimataifa uliofikiwa kwa HIYARI kati ya nchi mbili zilizokuwa huru; Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, juu ya ushirikiano kwa mambo kadhaa chini ya masharti MAALUM, unajulikana kama ‘Mkataba wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Mkataba huo ndio uliozaa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa nchi mbili hizo kujivua mambo hayo tu kila upande (maarufu kama Mambo ya Muungano), na kuyaingiza kwenye kapu moja lililoundiwa Serikali ya kuyasimamia, maarufu kama ‘Serikali ya Muungano,’ na kuziacha nchi hizo kubakia na mamlaka mengine, kwa yote yasiyo ya Muungano.
Mambo kumi na moja (11) kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Mkataba huo ni pamoja na; (a) Katiba na Serikali ya Jamhuri ya Muungano; (b) Mambo ya Nje; (c) Ulinzi (si Ulinzi na Usalama kama ilivyo sasa); (d) Polisi; (e) Mamlaka juu ya Hali ya Hatari; (f) Uraia; (g) Uhamiaji; (h) Biashara ya Nje na Mikopo; (i) Utumishi wa Umma katika Jamhuri ya Muungano; (j) Kodi ya Mapato kwa watu binafsi na mashirika, ushuru wa forodha na ushuru wa bidhaa; (k) Bandari, usafiri wa anga wa kiraia, posta na simu za maandishi (Telegraphs).
Kuthibitisha kwamba Tanganyika na Zanzibar hazikufa kufuatia kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano, angalia matakwa machache yafuatayo ya Mkataba wa Muungano. Sote tunafahamu namna Muungano huo ulivyofikiwa kwa njia ya dharura kwa shinikizo la mataifa makubwa katika kuokoa hali ya kisiasa Zanzibar. Kwa dharura hiyo, Muungano ulianzishwa bila maandalizi ya Katiba.
Kwa hiyo, iliwekwa wazi ndani ya Mkataba huo (Ibara ya 6) kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano, kwa makubaliano na Makamu wa Rais, ambaye pia ndiye Mkuu wa Serikali ya Zanzibar; (a) Atateua Tume ya Kupendekeza Katiba ya Jamhuri ya Muungano; (b) Ataitisha Bunge la Katiba likihusisha wawakilishi kutoka Tanganyika (na si Tanzania wala Tanzania Bara, majina ambayo si ya Kikatiba) na kutoka Zanzibar kwa idadi watakayoona inafaa ndani ya mwaka mmoja kutoka siku ya Muungano, kwa ajili ya kujadili na kupitisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Niharakishe kutamka mapema hapa kwamba huu ndio utaratibu unaotakiwa kufuatwa katika kupata Katiba ya Jamhuri ya Muungano, na kwamba utaratibu uliotumika katika kutunga Katiba ya 1977 inayotumika sasa, kwa kuigeuza Tume ya Watu 20 ya vyama vya TANU na ASP iliyopendekeza kuunganishwa kwa vyama hivyo na kuzaa Chama cha Mapinduzi (CCM), na kuwa Tume ya kupendekeza Katiba iliyopo sasa, ni batili kwa mujibu wa matakwa ya Mkataba wa Muungano.
Hivi kwamba uhalali wa Katiba hiyo, iliyozaliwa kwa utaratibu batili, unahojika. Tume ya sasa ya Jaji Warioba, imezingatia matakwa ya Mkataba huo wa Muungano, kama yalivyobainishwa kwenye Ibara ya 7 (a) na (b) ya Mkataba.
Na kwa kuwa ilikuwa dhahiri kwamba kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu siku ya Muungano, Muungano huo usingekuwa na Katiba, ilikubaliwa kwa mujibu wa Ibara ya 2, 3, 4 na 6 ya Mkataba wa Muungano, kwamba Katiba ya Tanganyika itumike kwa muda kama Katiba ya Muungano, kwa kuingiza katika Katiba hiyo, mambo yote kumi na moja (11) ya Muungano; na hivyo kumfanya (kwa muda) Rais wa Tanganyika ambaye alikuwa Rais wa Kwanza wa Muungano, kuwa Rais wa Tanganyika na pia Rais wa Muungano, chini ya Katiba ya Tanganyika iliyorekebishwa, hadi Muungano utakapopata Katiba yake.
Ilivyotokea ni kwamba si Tume ya kupendekeza Katiba iliyoteuliwa, wala Bunge la Katiba lililoitishwa na hivyo, kwa kipindi cha miaka 13 mfululizo tangu 1964, Muungano uliendeshwa kwa Katiba ya muda hadi mwaka 1977 ilipotungwa Katiba ya sasa ambayo uhalali wake unahojika, kama nilivyoeleza hapo juu.
Bonyeza Read More Kuendelea
Zipo kumbukumbu na ushahidi wa kutosha kuonyesha kuwa Tume ya Katiba haikuundwa kutokana na mfarakano baina ya Waasisi wa Muungano, kutokana na Mzee Karume kuamini kuwa aliingia Mkataba wa Muungano wenye Serikali tatu.
Ndiyo maana, kadri Mwalimu alivyokuwa akizidi kusisitiza Muungano wenye Serikali mbili, Mzee Karume aliona kama amesalitiwa; na si mara haba alisikika akisema kuwa Muungano umembana kama koti, na hivyo uvunjwe!
Kwa upande wake, Mwalimu, kwa kuchoshwa na vitisho vya Karume, alinukuliwa akisema; kama Wazanzibari kwa nia njema, na bila ya kurubuniwa kutoka nje, wataona Muungano unawabana na hivyo hawauhitaji tena, asingewapiga mabomu kuwalazimisha kuendelea na Muungano huo.
Na katika kipindi hicho hadi sasa, marekebisho lukuki yenye kuleta kero na mkanganyiko kwa Muungano yalifanyika ki-imla kwa chukizo na mitafaruku ndani ya Muungano. Kwa mfano, kitendo cha kuongeza mambo ya Muungano kutoka kumi na moja ya kimkataba hadi 23, ni ukiukaji dhahiri wa Mkataba huo wa kimataifa pamoja na sheria mbili za Muungano (Acts of Union) za mwaka 1964, zilizohalalisha utekelezaji wa Muungano huo kwa misingi ya Mkataba wa Muungano.
Ukiukaji huo wa Makubaliano ya Muungano, bila hofu ya kuhojiwa, na ambao kwa sehemu kubwa ulifanyika kwa ubabe wakati wa utawala wa Chama kimoja kushika hatamu za uongozi wa nchi, umejenga imani potofu kwamba Serikali ya Muungano inaweza kunyakua na kujiongezea mamlaka yoyote inayofikiri inafaa kufanya hivyo, ambayo vinginevyo ni mamlaka ya nchi za Tanganyika na Zanzibar.
Haya yamewezekana kutokana na sababu kuu mbili. Mosi, ni kwa wananchi kufichwa Mkataba wa Muungano, na hivyo tafsiri ya Muungano kuwa haki ya wahafidhina wachache wa kisiasa, tena kwa kupotosha kwa maslahi yao binafsi. Pili, ni ubabe chini ya utawala wa Chama kimoja, ambapo kuhoji Muungano lilikuwa kosa kubwa linalokaribia uhaini.
Rais wa awamu ya pili wa Zanzibar, Sheikh Aboud Jumbe, mwaka 1984, alitaka ufafanuzi juu ya ni upi mfumo sahihi wa Muungano, lakini, licha ya kwamba alitumia haki yake hiyo ya Kikatiba kuhoji, alivuliwa nyadhifa zote za uongozi wa Chama, Muungano na Visiwani.
Dalili za ubabe huo uliozoeleka kutaka kujirudia, zimeanza kujionyeha tunapoambiwa kwamba Kamati Kuu ya CCM, hivi karibuni imeketi na kuazimia kukataa pendekezo la Muundo wa Serikali tatu, na kutaka Muundo wa Serikali mbili uendelee, pengine ama kwa makusudi au kwa kutoelewa kuwa wanakiuka matakwa ya Muungano; au kwa kuelewa lakini bado wakiamini kwa kujidanganya kwamba Watanzania bado wamelala juu ya jambo hili.
Ubabe huo wa kichama, ukiruhusiwa kujirudia, unaweza kukaribisha machafuko ya kisiasa yanayoepukika, na hata kuvunja Muungano wenyewe. Wanasiasa wetu wanapaswa kusoma vyema alama za nyakati na hisia za wananchi, na si hisia za viongozi, na kuoanisha kwa makini ‘kero’ za Muungano ambazo zimeyumbisha Muungano wetu tangu uanzishwe miaka 49 iliyopita ili kuiepushia nchi mitafaruku ya kisiasa.
Aidha, Watanzania wamechoka na kero za Muungano na mitafaruku yake. Ni bora wanasiasa wakaziacha sauti za wananchi zisikike katika mchakato huu wa Katiba Mpya. Kutokufa kwa Tanganyika na Zanzibar kama nchi huru, zenye mamlaka ya nchi kwa mambo yasiyo ya Muungano, kunathibitishwa na Ibara ya 5 ya Mkataba wa Muungano inayobainisha kwamba pamoja na Serikali ya Muungano kubeba mambo kumi na moja ya Muungano, “Sheria za Tanganyika na za Zanzibar zilizopo na zitakazotungwa, zitaendelea kuwa na nguvu katika nchi husika.”
Sheria hizo ni nyingi, lakini itoshe tu kutoa mifano ya sheria mbili za mwaka 1971, miaka saba baada ya Muungano, zilizoendelea kutambua kuwapo na kutamka nchi ya ‘Tanganyika’ kwa kuheshimu Mkataba wa Muungano. Moja ya sheria hizo ni Sheria ya Ndoa ya 1971, ambayo imetamka kote kuwa ni kwa ajili ya Tanganyika na kwa wakazi wa Tanganyika.
Nyingine ni Sheria ya (muda) ukomo wa Madai (The Law of Limitation Act) ya mwaka 1971, ambayo inatamka wazi ni kwa ajili ya na katika Tanganyika pekee; na sheria nyingine nyingi.
Kwa mantiki hiyo, kwanini isiwe kweli kwamba Muungano unaotakiwa na uliokusudiwa tangu mwanzo, ni wenye mfumo wa Serikali tatu, kwa maana ya Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Zanzibar (ambazo hazikufa) na Serikali ya Shirikisho, kwa mambo kumi na moja tu ya Muungano?
Lakini pia, Ibara ya 6 (a) ya Mkataba wa Muungano wa mwaka 1964, inatanabahi kuwa; “Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano, atakuwa Mwalimu Julius Nyerere, na atatekeleza shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa mujibu na kwa kuzingatia matakwa ya Mkataba huo, kwa kusaidiwa na Makamu wa Rais wawili, Mawaziri na Ma-Ofisa wengine atakaowateua kutoka Tanganyika na Zanzibar.”
Kwa maelezo hayo, ni kipofu gani atabisha kwamba Tanganyika na Zanzibar hazikufa baada ya ujio wa Muungano? Wanaodai mfumo wa Serikali mbili, wanatoa wapi ujasiri potofu na wa kihafidhina kupotosha umma juu ya mfumo halali wa Muungano uliokusudiwa? Watuambie; kama Zanzibar ilisalimika, Tanganyika ilitowekaje?
Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1965, kwa kutambua uwepo wa Tanganyika hai, na kwa kuzingatia Mkataba wa Muungano, ilibainisha ifuatavyo katika ibara yake ya 13:
“Kutakuwa na Makamu wawili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano, ambapo mmoja atakuwa Msaidizi Mkuu wake kwa shughuli za kitendaji upande wa Zanzibar, na ambaye atajulikana pia kama Rais na Mkuu wa Serikali ya Zanzibar; na mwingine atakuwa Msaidizi Mkuu wa Rais kwa shughuli za kitendaji kuhusiana na Tanganyika.”
Tena Katiba hiyo hiyo, Ibara ya 20 na 24 (b) inasema: “Rais atateua mkuu wa mkoa kwa kila mkoa ndani ya Tanganyika, na Bunge litakuwa na uwezo wa kurekebisha idadi ya mikoa kwa Tanganyika na kwa Zanzibar…”
Na kuhusu majimbo ya uchaguzi, Katiba hiyo ya Muda ya mwaka 1965, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Muungano, na iliyozingatia na kuheshimu matakwa ya Mkataba na Sheria za Muungano kabla ya kuchakachuliwa na wahafidhina wa siasa za kibabe kwa njia ya marekebisho, katika Ibara ya 25 (1) na 25(3) inasema:
“Tanganyika itagawanywa katika majimbo kwa kuzingatia wakazi wa majimbo na kila jimbo litawakilishwa na mbunge mmoja…Tume ya Uchaguzi itapitia upya mgawo wa majimbo ya uchaguzi ya Tanganyika kila kipindi kisichopungua miaka minane, na kisichozidi miaka kumi…”
Mara nyingi, ubabe uliotumika kufanyia marekebisho Katiba yetu kinyume na matakwa ya Muungano asilia, umefanywa kwa maelekezo ya Chama Tawala, hata Chama hicho kufikia kuwa sehemu ya Katiba ya Muungano wakati ikifahamika wazi kuwa vyama vya siasa si jambo la Muungano.
Muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu uliokusudiwa chini ya Mkataba wa Muungano wa 1964, na ambao umependekezwa pia na Tume ya Katiba ya Jaji Warioba, ni mfumo unaotambulika kimataifa chini ya Sheria za Kimataifa.
Ni mfumo ambapo nchi zaidi ya moja huungana kwa mambo nyeti kadhaa, kama vile uraia, mambo ya nje, ulinzi na usalama, Polisi na kadhalika, na kuyaundia Serikali Kuu moja kuyasimamia, na kuziacha nchi husika kusimamia na kudhibiti mambo yake yote mengine yasiyo ya Muungano.
Bila shaka, wakati Mwalimu Nyerere alipomwagiza Mwanasheria Mkuu wake wa Serikali, Roland Brown, Aprili 19, 1964; aandae rasimu ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa muundo na mfumo wa uhusiano wa Serikali ya Uingereza na Serikali ya Ireland Kaskazini, alikuwa na maana ya Muungano aina ya Shirikisho kama nilivyoeleza hapo juu.
Chini ya mfumo huo, na kama ilivyopenekezwa na Tume ya Jaji Warioba, Tanganyika na Zanzibar zitasimamia mambo yake ya ndani yasiyo ya Muungano, kama ambavyo tu Zanzibar inavyosimamia mambo yake hivi sasa.
Kwa kuwa, kwa mfano, uraia ni jambo la Muungano, hapatakuwa na Watanganyika wala Wazanzibari, bali raia wa nchi hizi watajulikana kama Watanzania. Vivyo hivyo, kwa kuwa Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Kimataifa ni jambo la Muungano, Tanzania, na si Tanganyika wala Zanzibar, zitakazofahamika kama nchi au Taifa kimataifa.
Na ndivyo itakavyokuwa kuhusu Ulinzi na Usalama, kwamba kushambuliwa kwa Tanganyika au Zanzibar ni kushambuliwa kwa Tanzania. Tanzania, na si Tanganyika wala Zanzibar, ndiyo itakayokuwa dola na Rais wa Tanzania ataendelea kuwa Mkuu wa Vikosi vyote vya Ulinzi na Amiri Jeshi Mkuu.
Maadam, Tume ya Marekebisho ya Katiba ya Jaji Warioba, kwa mujibu wa Ibara ya 1 (3) ya rasimu yake, imebainisha kwamba msingi mkuu wa mapendekezo ya marekebisho hayo, ni Mkataba wa Muungano ya mwaka 1964, ambayo, kama tulivyoona, unatambua muundo wa Shirikisho lenye Serikali tatu, basi msingi huo uzingatiwe na kila mtu wakati wa kujadili rasimu hii ili tuweze kubakiza na kulinda Muungano uliokusudiwa.
Na Joseph Mihangwa, RAIA MWEMA
No comments:
Post a Comment