Friday, June 28, 2013

Kauli ya Pinda bado yazidi kuwachefua wanaharakati

Kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kulitaka Jeshi la Polisi kuwapiga watu watakaokaidi amri ya jeshi hilo aliyoitoa bungeni wiki iliyopita, imezidi kumweka pabaya baada ya wanaharakati mkoani Morogoro, kumtaka aifanyie marekebisho au ajiuzulu.

Pinda alitoa kauli hiyo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kilwa Kaskazini (CCM), Murtaza Mangungu, wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwake.

Wanaharakati hao ambao ni Wasaidizi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria, walitoa tamko hilo kwa nyakati tofauti katika mafunzo ya siku tatu kuhusu haki za binadamu.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Mtandao Masharika Huduma za Haki za Kibinadamu na Kisheria (Tanlap).

Mwenyekiti wa Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria kwa Wanawake na Watoto mkoani Morogoro (MPLC), Frola Masoy alisema kauli ya Waziri Mkuu Pinda, kama Kiongozi Mkuu wa Serikali, hakupaswa kutoa kauli hiyo na ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Alisema kauli hiyo aliyotoa inaendelea kuchochea vitendo vinavyofanywa na vyombo vya dola hapa nchini vikiwamo vya kuwapiga na kuwatesa raia wasio hatia hasa pale wanapokuwa na mtazamo tofauti na serikali.

Naye Levina Mzaga, ambaye ni mmoja wasaidizi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria kutoka wilayani Mvomero, alisema kuwa Waziri Mkuu amepotoka kwa kauli yake hiyo.

Mzaga alisema alichotakiwa kutamka Waziri Mkuu ni kuwaagiza polisi kuwafikisha katika vyombo vya sheria wanaovunja sheria.

Alisema kauli ya Waziri Mkuu imelenga kuendelea kuchochea uvunjifu wa amani nchini, hivyo Bunge linapaswa kumchukulia hatua vinginevyo afute kauli hiyo.

Mwanaharakati na Msaidizi wa kisheria wilayani Morogoro, Syliverster Massawe, alisema kauli ya Waziri Mkuu inaonyesha hata matukio ya kuuawa kwa baadhi ya wananchi kunakofanywa na baadhi ya polisi na wengine kuteswa na kupigwa, ni maagizo ya serikali.

“Kwa kauli hiyo ya kuruhusu polisi kuwapiga tu watu wanaokaidi maagizo ya vyombo hivyo, tunaamini ni maagizo ambayo yalishatolewa na serikali ikiwamo kuuawa kwa Daud Mwangosi na kuteswa kwa Kibanda...Tunamtaka ajiuzulu," alisema.

Awali, akizungumzi kuhusu mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Tanlap, Chiristina Kamili, alisema mafunzo hayo kwa wasaidizi wa kisheria, yana lengo la kuwajengea uwezo ili kwenda kutoa huduma za kisheria na kuichambua Rasimu ya Katiba.

 

No comments:

Post a Comment