MWANASHERIA Mkuu mstaafu, Jaji Mark Bomani, amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufuata misingi ya sheria katika utendaji wao wa kazi.
Bomani amevitaka pia kuzingatia sheria katika matumizi ya silaha kwenye matukio mbalimbali wanayokabiliana nayo.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa Kongamano la Maadili ya Waandishi wa Habari lililofanyika jijini Dar es Salaam jana likiwa na kaulimbiu ya ‘Wajibu wa Vyombo vya Habari Kupambana na Kauli za Chuki na Itikadi Kali.’
Alisema kumekuwa na tabia ya baadhi ya vyombo vya dola kuwapiga watu bila kufuata sheria ambazo zinakataza kufanya hivyo, lakini mambo hayo yanatokana na uelewa mdogo.
Aliongeza kuwa hata maandamano na mikutano yoyote inapozuiwa pia ni lazima vigezo na sheria zifuatwe ili kila mmoja au kinachofanyika kimezingatia sheria na si uonevu au upendeleo.
“Sheria inaweka wazi ni maeneo gani vyombo vya dola vinaweza kutumia silaha za moto, lakini siku hizi naona mambo yanakwenda ndivyo sivyo,” alisema.
Bomani aliitaja Sheria inayohusu kumiliki au kubeba silaha ambayo ni Sura Na. 223 ya sheria za nchi, kifungu cha 4 cha sheria hiyo kinasema: “Ni kinyume cha sheria kwa mtu yeyote kumiliki au kubeba silaha ya moto bila ya kuwa na kibali cha kufanya hivyo,” alifafanua.
Alionya vyombo vya dola kuwa havipo juu ya sheria katika utendaji wao wa kazi, hivyo ni vema wakazingatia sheria za nchi.
Jaji Bomani aliongeza kuwa tasnia ya habari ina jukumu kubwa la kuandika habari zitakazokuwa chachu katika kudumisha umoja na mshikamano wa nchi.
Alisema bila ya tasnia hiyo kupiga vita mambo yote ambayo madhumini au matokeo mi kuvuruga amani ya nchi au kuchochea chuki na mfarakano katika jamii kama ilivyojitokeza siku za karibuni taifa litaangamia.
Bomani alisema kila mmoja anapaswa kujua kuwa amani ikivurugwa au kuvunjika itakuwa ni vigumu kuirejesha kwasababu madhara yake ni makubwa kwa wananchi.
Alisema vyombo vya habari vijiepushe na itikadi za vyama pamoja na kuzingatia maadili katika utendaji kazi wao wa kila siku.
“Wanahabari shurti wawe wenye ari ya kujipatia elimu na wanaopenda kujiendeleza kielimu, na ikiwezekana, wajikite katika mambo fulani ili waweze kuelewa na kutafsiri matukio mbalimbali ndani na nje ya nchi,” alisema.
Bomani alisema vyombo vya habari viwasogeze Watanzania wawe wamoja, washiriki shughuli za maendeleo kwa pamoja bila kujali dini au itikadi zao za kisiasa.
“Mwanahabari anapozungumzia matumizi ya nguvu kupita kiasi yakifanywa na vyombo vya dola, kigezo chake kinakuwa ni nini? Hili ninalozungumza limekuwa likitokea mara nyingi sana hapa nchini katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni,” alisema.
Mwandishi mwandamizi Makwaiya wa Kuhenga alisema magazeti ya zamani yalikuwa na mchango mkubwa wa kudumisha amani ya nchi na umoja wa kitaifa.
“Sasa hali ikoje katika zama hizi za gulio? Nimegusia kidogo mambo ya leo ya viongozi wa kisiasa kujialika kwenye hafla za kidini. Wapo wengi hao! Kuna mwiko gani unaowakataza? Gulio lina mwiko?” alihoji Wakuhenga.
Wakuhenga alisema pamoja na gulio la wanahabari ni lazima wajue wana wajibu mkubwa kuhakikisha nchi haiendi kubaya.
Naye Ndimara Tegambwage, alisema serikali imeendelea kulitambua Baraza la Habari (MCT), na haki zake; ilitumie kwa ushauri wa kitaalamu na kitaaluma (mfano NACTE).
Ndimara alisema Sheria juu ya vyombo vya habari itamke waziwazi kuwa taarifa za serikali zitapatikana bila kikwazo, ilinde waandishi na vyombo vyao vya habari; na ifute vipengele vya kubamiza au kuondoa uhuru wa habari vilivyomo katika sheria nyingine.
No comments:
Post a Comment