Wednesday, June 19, 2013

Arfi, Lissu watiwa mbaroni Arusha

Wabunge wanne wa Chadema, Said Arfi (Mpanda Mjini), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mustapha Akunaay (Mbulu) na Joyce Mukya (Viti Maalumu) wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mkusanyiko usio halali kwenye Uwanja wa Soweto jana.
Mkuu wa Operesheni wa Polisi, Kamishna Paul Chagonja alisema jana kwamba pamoja na wabunge hao pia wamewakamata watu wapatao 60 kutokana na vurugu zilizozuka jana baada ya Polisi kuwatawanya kwenye uwanja huo waliokuwa wamekusanyika kuomboleza vifo vya watu watatu; Judith Moshi, Ramadhan Juma na Amir Ally waliofariki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea kwenye uwanja huohuo, Jumamosi iliyopita.
Mbali ya viongozi hao, alisema wanawasaka Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema.
“Tunawasaka wabunge ili tuwajumuishe na watu hawa kwa kosa la kuhusika na mkusanyiko usiokuwa halali. Hadi sasa tumefanikiwa kulinasa gari la Mbowe,” alisema Chagonja.
Pia kamatakamata hiyo imemkumba Mpigapicha wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Ashraf Bakari. Polisi walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya waombolezaji hao.
Awali, Kamishna Chagonja alisema jana asubuhi kuwa wamelazimika kuzuia viwanja hivyo kutumika baada ya wamiliki wake, AICC kuzuia shughuli za Chadema kwenye eneo lao.
Kamishna Chagonja aliwaonyesha waandishi wa habari barua aliyosema imeandikwa na uongozi wa AICC kuzua Chadema kuendelea kuutumia Uwanja wa Soweto.

Bonyeza Read More Kuendelea



Mabomu yarindima
Dalili za kuzuka kwa vurugu zilianza kuonekana asubuhi baada ya polisi kuzingira uwanja huo na kuzuia watu waliokuwa wameanza kufurika katika eneo hilo kuanzia saa moja kuingia kwa ajili ya maombolezo.
Wakati Polisi wakiwa uwanjani, wananchi walijaa nje ya uwanja na kuonekana kama wamewazingira.
Viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe waliwasili uwanja hapo yapata saa nane mchana na kukuta zuio hilo na kuanza kuzungumza na wananchi ingawa FFU walikuwa wakiwataka watu kutawanyika. Mabomu yalianza kurindima wakati Arfi aliposimama na kuwahimiza wananchi kuelekea Hospitali ya Mount Meru kwa ajili ya kuaga miili ya marehemu.
“Tuna muda mfupi sana wa kuzungumza hapa, tunaomba wote tuelekee Hospitali ya Mount Meru kuaga miili ya marehemu kwa sababu uwanja huu umezuiwa na polisi,” alisema Arfi kabla ya kukatishwa na milipuko ya mabomu.
Awali, Lissu ambaye pia ni Mwanasheria wa Chadema alitoa msimamo wa chama hicho kuwa Mwenyekiti wao, Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wa tukio la bomu wala kujisalimisha polisi kwa sababu hawana imani na jeshi hilo.
“Namtaka Chagonja atangulie mahakamani, tutakutana hukohuko. Mbowe na Lema hawatatoa ushahidi wala kujisalimisha polisi...” alisema Lissu na kuongeza:
“Kisheria haiwezekani polisi ambao ndiyo watuhumiwa ndiyo wadai kukabidhiwa ushahidi ili wauharibu.”
Mapema Kamishna Chagonja aliwataka Mbowe na Lema kutoa ushahidi wa polisi kuhusika na tukio la kurusha bomu kwenye mkutano wa Chadema la sivyo polisi watatumia sheria kuwalazimisha kufanya hivyo.
Hekaheka
Baada ya polisi kuanza kutupa mabomu saa 8.45 mchana, wabunge, viongozi waandamizi wa Chadema na watu waliokuwa wamekusanyika walilazimika kutimua mbio.
Watu walioshuhudia tukio lile wanasema viongozi hao akiwamo Mbowe na mwenzake Lissu walikimbilia kwenye magari yao. Lema alilazimika kukimbilia kwa wachoma nyama ya nguruwe, (kitimoto) kwenye maeneo ya Kaloleni.
Kabla ya polisi kurusha bomu mahali alipokuwapo Lema, mbunge huyo alisikika akisema:
“Jaribuni kuvumilia, tunajaribu kuwasiliana Serikali ya Mkoa, ili watupe kibali cha kuleta miili ya wapendwa wetu hapa, kuweni wastaarabu kwa sababu mbele yetu kuna wana usalama ambao wanalinda amani, ingawa kufa ni kufa tu, wenzetu wameshakufa na sisi ipo siku tutakufa, lakini kila anayetangulia lazima tumzike kwa heshima zote.”
Kauli hiyo iliwachefua polisi ambao walishatangaza amri ya watu kutawanyika katika viwanja hivyo na kwamba hakutakuwa na suala la kuaga miili ya watu hao katika eneo hilo. Ghasia hizo zilisababisha kusimama kwa shughuli za biashara na kijamii kwa muda jijini Arusha huku watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na maeneo yalikorushwa mabomu wakilazimika kutoka nje kupata hewa safi baada ya nyumba hizo kujaa hewa ya mabomu.
Polisi waliokuwa wakirusha mabomu waliwakimbiza wananchi hadi maeneo ya Sakina huku wakiendelea kufyatua mabomu kila walipoona mkusanyiko wa watu.
Katika eneo la Kaloleni, mkabala na Ofisi ya Mtendaji wa Kata hiyo baadhi ya wafuasi wa Chadema walichoma matairi barabarani na kusababisha ifungwe. Pia walichoma matairi katika eneo la Mianzini.
Katika eneo la Tanki la Maji, Barabara ya kwenda Moshi, baadhi ya wafuasi wa Chadema walipanga mawe barabarani na kusababisha msongamano wa magari.
Katikati ya jijini Arusha barabara zilikuwa hazipitiki kutokana na nyingine kufungwa na kusababisha usumbufu mkubwa.
Waandishi nao matatani
Katika vurugu hizo, baadhi ya waandishi wa habari walishambuliwa na polisi. Hao ni pamoja na Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti dada la The Citizen, Zephania Ubwani ambaye kabla ya kuchomoka katika mikono ya askari, alikuwa akiwaonyesha kitambulisho chake cha kazi.
Hata hivyo, askari hao walimtishia kumtandika na kisha kumwambia aondoke katika eneo hilo kwa kuwa haijalishi yeye ni nani.
Mwingine ni mwandishi wa gazeti la Nipashe, Cnythia Mwilolezi ambaye alilazimika kuacha viatu na vitendea kazi vyake katika Uwanja wa Soweto na kukimbilia kwenye moja ya nyumba zilizopo jirani na eneo la tukio.
Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha, Moses Kilyinga alipigwa na polisi baada ya kuonekana akichukua maelezo.
Kilyinga ambaye alishambuliwa na askari hao alisema mara baada ya askari hao kumkamata, alijitambulisha lakini hawakumwelewa na wakaendelea kumchapa kabla ya kufanikiwa kuchomoka.

Polisi wavamia hospitali
Wakati baadhi ya majeruhi wakidai kushuhudia polisi wakiwapiga risasi watu waliokuwa wakimkimbiza mtu aliyerusha bomu katika tukio la Jumamosi, askari hao juzi walifika katika Hospitali ya Seliani saa mbili usiku wakitaka kumchukua mmoja wa majeruhi kwa mahojiano kuhusiana na tukio hilo. Hata hivyo, hawakufanikiwa baada ya mgonjwa kutokomea kusikojulikana baada ya kupata taarifa za kutaka kuhusishwa na tukio hilo.
Ingawa si polisi wala Chadema waliokuwa tayari kumtaja mgonjwa huyo, inaelezwa kwamba majeruhi anayesakwa ni Abdallah Alila aliyekaririwa na vyombo vya habari jana na juzi akidai kumshuhudia aliyerusha boma akiondoka kwenye moja ya magari ya polisi.
Hata hivyo, Kamishna Chagonja jana alisema kwamba jeshi lake linapenda kushirikiana na raia kupata taarifa na si kutumia nguvu katika kukusanya ushahidi wake.

5 comments:

  1. Jamani polen Chadema na wahanga wote wa haya maswahibu ila mi nasema mwisho wa ubaya ni aibu na ipo siku ukweli utajulikana.Inatosha haya mateso,watanzania tuamke yaliyotokea juzi Arusha ya naweza kutokea na kwako pia.Eee Mungu iokoe Tanzania.



    ReplyDelete
  2. Jamani polen Chadema na wahanga wote wa haya maswahibu ila mi nasema mwisho wa ubaya ni aibu na ipo siku ukweli utajulikana.Inatosha haya mateso,watanzania tuamke yaliyotokea juzi Arusha ya naweza kutokea na kwako pia.Eee Mungu iokoe Tanzania.
    Lhumbika Manase,Dar es salaam.



    ReplyDelete
  3. HIVI KARIBUNI KUMEKUWEPO NA MFULULIZO WA VIONGOZI WA CCM KWENDA CHINA MARA KWA MARA NA LILE BOMU LILILOTUMIKA ARUSHA KWA MAELEZO YA PINDA LIMETKA CHINA

    MOJA YA VIONGOZI HAO WA CCM UKIMWANGALIA TABIA NA MAVAZI YAKE VIMEBADILIKA TANGIA ALIPOTOKA CHINA MAVAZI YAKE,KOFIA INA ALAMA ZA AJABU SANA.HUYU SIO MWINGINE BALI NI MWIGULU NCHEMBA,HEBU MUANAGALIENI ANAPOKUWA KWENYE HALAIKI YA WATU HUWA ANAPENDA SANA KUNYOOSHA JUU MKONO WAKE WA KUSHOTO,HII INAMAANISHA NINI?

    JESHI LA POLISI LINAFANYA KAZI KWA HISIA SANA SIO WELEDI TENA.NINASEMA HIVI KWA SABABU HIVI KARIBUNI AMEKUWA AKITOA MATAMSHI YENYE UTATA LAKINI JESHI LA CCM HALIKUWAHI KUMHOJI HATA MARA MOJA.KWA MFANO AMEKUWA AKIPITA KARIBIA NCHI NZIMA AKISEMA ANAO USHAHIDI UNAOONESHA CHADEMA WAKIPANGA KUUA WATU,JUZI JUZI HUKO ARUSHA AKASEMA WATU WA ARUSHA WASIPOICHAGUA CCM WATAKUFA NA KWELI WATU WAMEKUFA KWA MLIPUKO WA BOMU.CHA KUSHANGAZA HAMNA KIONGOZI WA SERIKALI WALA JESHI LA POLISI ALIYE THUBUTU KUMHOJI

    MAAJABU YA DUNIA NI KWAMBA BAADA YA MBOWE NA LEMA KUSEMA WANA USHAHIDI WA JINSI POLISI WALIVYOLIPUA BOMU KWENYE MKUTANO TUMEONA JESHI LA POLISI LINAVYO DINDISHA MIDOMO BILA HAYA HATA CHEMBE KUWATAKA VIONGOZI WA CHADEMA WAPELEKE USHAHIDI KWAO LA SIVYO WATAWAKAMATA

    SHEM ON YOU POLISI CCM

    ReplyDelete
  4. Poleni sana CHADEMA poleni sana wanancni wa Arusha, Kwa kweli ni wazi kabisa polisi wanatumika kufanya uharamia wote huo na kuua na wametumwa na wakuu wao. Sasa hivi hawa polisi na hao wakubwa wa CCM watatakiwa kushitakiwa katika mahakama ya THE HAGUE. Lakini ndio mwisho wa CCM na hao polisi watalipwa kwa yote waliyoyafanya ni mengi sana mabaya ya kuua wapendwa wetu hao na wengine, wamewaua lakini damu zao hazijamwagika bure Mungu wetu anaona hili. Watalipwa kwa Ubaya huu walioufanya na kutaka kuficha ukweli. Mungu ibariki Chadema Mungu Ibariki Tanzania,wananchi wameamka tutapigania amani ya nchi hii.

    ReplyDelete
  5. Poleni sana CHADEMA na wananchi wa Arusha. Hawa CCM wameshiriki kwa kuwatuma Polisi kufanya mauaji sasa imetosha wamefanya mauaji mengi ya wananchi lakini wananchi wataelewa tu ukweli ingawa wanajaribu sana kuficha ukweli kuwa wao polisi ndio wauaji wakuu kwa kutumwa na viongozi waandamizi wa CCM.John michael, Dar Es Salaam.

    ReplyDelete