Tuesday, May 7, 2013

Wabunge Chadema kitanzini 2015


Nafasi zao kutangazwa magazetini
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza mfumo mpya wa kuwapata wagombea nafasi ya ubunge kuanzia uchaguzi wa 2015. Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa alisema kuwa kuanzia uchanguzi ujao wa 2015, nafasi za wagombea ubunge majimbo yote nchini zitatangazwa kwenye magazeti.
Dk. Slaa alisema baada ya waombaji kujitokeza watafanyiwa usaili kwa kufanya mtihani utakaokuwa umeandaliwa kwa kuzingatia nafasi hizo.

“Mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe amekwisha kusema kwamba kuanzia sasa hatupokei makapi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hili naliweka wazi kwamba uchaguzi ujao utakuwa na mfumo mpya na wenye mabadiliko makubwa, tunaamini utaleta uzalendo na kuondoa upuuzi unaojitokeza.

“Kwa wale walio na mipango ya kujitokeza dakika za mwisho kugombea nafasi za ubunge kupitia Chadema au nje ya chama, naomba wasahau hilo tunataka mtu anayetetea wananchi, mwenye uzalendo, hoja, ujasiri na mwenye kuitoa Tanzania hapa ilipo na kuisogeza mbele,”alisema.

Akizungumzia suala la mchakato wa katiba mpya alisema Chadema haitakubali kuona inakuwa sehemu ya watu walioshiriki kutengeneza katiba isiyo ya Watanzania wote.

“Sasa kwa kuwa Serikali imetoa majibu yake bungeni kupitia kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda tunasubiria mwenyekiti wetu Mbowe awasilishe ripoti kwenye kamati kuu ndipo tutakapoamua.

“Pia suala la mwakilishi wetu katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu litazungumzwa kwenye kamati kuu, chama kikijitoa hata kama akibaki hayo yatakuwa ni mawazo yake,”alisema.

Hata hivyo alisema kuwa amani ya imevurugwa na viongozi wa Serikili na vyama vya siasa kutokana na kutanguliza ushabiki wa siasa badala ya uzalendo na misingi ya taifa.

Wakati huo huo Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Iramba Magharibi, Ntundu Emmanuel amehamia Chadema akidai kuchoshwa na matusi ya Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba.


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa, akimkabidhi kadi ya Uanachama aliyekuwa msaidizi wa Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM) Edgar Ntunda, baada ya kujiunga na Chadema jana. Picha kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

No comments:

Post a Comment