Tuesday, May 7, 2013

CC Chadema kuamua hatma ya Prof Baregu Tume ya Katiba


Kamati Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CC-Chadema), ndiyo itakayoamua hatma ya mwakilishi wa chama hicho katika Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu.

Aidha, kamati hiyo ndiyo itakatoa utaratibu wa namna bora ya Chadema kujitoa ama kutojitoa kwenye mchakato huo, kama ilivyoelezwa awali kwamba kitaususia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema baada ya kupata majibu ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na yale yaliyotolewa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, chama sasa kitayawasilisha kwenye Kamati Kuu ili ifanye maamuzi.

Alisema Chadema ni mdau mkubwa wa kuhakikisha Katiba mpya inapatikana lakini inapinga mchakato ambao unalenga kutengeneza Katiba ya kikundi kidogo.

"Malalamiko ya kasoro zilizojitokeza kwenye uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza ya Katiba yapo nchi nzima, hatuwezi kukaa kimya wakati tunaona kinachofanyika ni kutengeneza Katiba Dola kwa manufaa ya kikundi kidogo," alisema.

Dk. Slaa alisema hata kama serikali itaziba masikio na kuendelea na mchakato huo, Chadema itawaeleza wananchi aina ya Katiba iliyotengenezwa na athari zake.

"Tunasema Katiba itokane na wananchi kwa sababu wao ndio watakaoamua anayetaka kuwaongoza awaongozeje, siyo anayeongoza kutaka kutengeneza mfumo wa kuwaambia namna anavyotaka kuwatawala," alisema.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratias Munishi, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinakwepa kukubali mikutano ya Vijiji kuchagua Mabaraza ya Katiba kwa kuwa kinajua wananchi wengi watachagua wawakilishi wazuri kuliko waliopitishwa na wajumbe wa Kamati ya Kata (Ward C).

Alizungumzia pia ujangili, akieleza Chadema kimewataja wahusika wa biashara hiyo haramu ambao baadhi ni makada wa CCM na wengine wa Serikali, hivyo kinachotakiwa kufanyika ni CCM kueleza ni kwa namna gani wanachama wao hawahusiki.

Chadema ilitangaza kujiondoa kwenye mchakato wa Katiba Aprili 30, mwaka huu kama Tume isingerekebisha mfumo wa kuchagua wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya kwa kutaka mikutano ya vijiji ndiyo iwachague badala ya Ward C iliyofanya uchaguzi.

Wakati huo huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM jimbo la Iramba Magharibi ambaye pia ni msaidizi wa Mbunge wa jimbo hilo, Mwigulu Nchemba, amehamia Chadema.

Awali, kiongozi huyo, Emmanuel Ntundu, alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Iramba, hadi mwaka 2010 alipohamia CCM.

Akizungumza baada ya kumkabidhi kadi ya Chadema, Dk. Slaa alimionya kwamba tatizo la CCM siyo watu wenye sifa za viongozi bali ni mfumo mzima wa uongozi hivyo kuhamia kwake CCM kusingeweza kuleta mabadiliko.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

  1. Ni ukweli usiopingika kuwa Prof. Baregu ni mtu msomi na kiongozi mahiri, namfahamu vyema msimamo wake kwani aliwahi kuwa mwalimu wangu UDSM, yuko kwenye mchakato wa katiba ya Taifa na siyo Chama hivyo naamini hatakubaliana na kabisa na mawazo ya kichama zaidi bali atazingatia maslahi ya kitaifa zaidi. Prof. nakupongeza kutokubaliana na kakikundi hako na kuwaacha watanzania wakitungiwa katiba feki.

    ReplyDelete
    Replies
    1. sawa; lakini yeye mwenyewe akiwa mmojawapo wa kutunga Katiba Feki afanye nini? tatizo macho yako hayaoni mchakato wa uchaguzi wa wajumbe wa mabaraza vijijini na wilayani ulikuwaje. asipoangalia Prof. Beregu naye atakuwa amechangia katiba mbovu na U-Prof. wake utatukanwa.

      Delete