Sunday, May 19, 2013

UCHIMBAJI GESI ASILIA: Wabunge wacharuka


Wabunge waipasha serikali kuacha papara ya kuingia kwenye mikataba ya uchimbaji gesi asilia, kwani itaipeleka nchi pabaya na kuiingiza kwenye hasara kama ilivyotokea kwenye mikataba tata ya madini.
Walitoa tahadhari hiyo jana wakati wakichangia rasimu ya sera ya gesi asilia kwenye semina ya wabunge, iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati na Madini mjini hapa.
Walisema serikali imeingia mikataba mingi ambayo haipo wazi, na haikushirikisha wataalamu wakiwamo wanasheria.
Wakahoji kwa nini serikali inafanya haraka kuijiingiza kwenye mikataba ya uchimbaji wa gesi asilia, wakati ile ya madini imeisababishia Tanzania madeni yanayoendelea kulipwa hadi leo.
Mbunge wa Dole (CCM), Sylvester Mabumba, alisema kwa vile nchi haina wataalamu wa gesi, mikataba itakayofanywa haitakidhi matakwa ya kitaalamu kwa maslahi ya nchi.
“Waliopitisha mikataba ya Richmond nina imani wapo hapa (bungeni) na hasara waliyotusababishia mfano dhahabu, Watanzania hatukunufaika nayo. Huu uharaka tunaoambiwa twende, hatuna macho, uharaka wa nini,” alihoji.
Alitoa mfano wa Uganda, kuwa haijaingia kwenye mkataba wa uchimbaji mafuta, badala yake Rais Yoweri Museven, aliwapeleka watalaamu nje kusomea sekta hiyo, wakarejea wakiwa wataalamu waliobobea.
“Tuna haraka gani kuuza mali yetu ili tubaki maskini, mikataba itakayoingia serikali yetu iletwe hapa bungeni ili tujue tunapata nini. Tunahitaji kuweka mfumo wa udhibiti ili yote utakayofanya kwenye sekta hii yawe na uwazi,” alisema.
Naibu Waziri wa Fedha, Janeth Mbene, alitaka kujua sheria ya mwaka 1980 ya uzalishaji na utafutaji mafuta kama bado inakidhi mahitaji ya sasa, ili nchi isije ikaingia katika `mitego’ kama ilivyokuwa kwenye madini.
“Ni bora sheria hiyo iangaliwe upya kubaini vipengele vinavyoleta matatizo, ningependa kuona tathmini mahususi, tuangalie yaliyotuletea changamoto katika sera na sheria za madini ambazo zilituingiza mkenge, tuyaepuke,” alisema.
Alisema kuna mambo mengi yamejitokeza, yanayoleta wasiwasi kwa wananchi kutokana na uvunjaji wa sheria na kuhimiza kuwasikiliza wananchi katika kutatua kero .
Pia alipendekeza kuwapo ukomo kwa vivutio kwa wawekezaji, ili watakapoanza kuzalisha waendelee kulipa kodi.
Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, alisema Tanzania isikubali watu wa nje kutwaa nafasi ya serikali katika kushiriki mchakato wa gesi.
Aliitaka serikali kuhakikisha kuwa Watanzania ambao rasilimali zinatoka kwao, wanafaidika.
“Hatusemi rasilimali zinufaishe Mtwara na Lindi, lakini wao lazima waone faida kuwapo kwa nishati pale, siyo kujengewa viwanda vya kuchuja tu, wanahitaji zaidi ya hapo,” alisema na kuongeza:
“Yaliyotokea Geita, Bulyanhulu, Nyamongo, hatutaki yatokee maeneo mengine,” alisema.

Bonyeza Read More Kuendelea



Aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi , alisema sera iliyokuwapo kwenye mchakato wa kupata gesi, inaonyesha kuna kasoro na kwamba mchakato huo unahitaji sera yake pekee.
Alisema, Katibu Mkuu wa wizara hiyo alithibitisha kuwepo watalaam wanasheria wawili tu.
Mbunge wa Nzega (CCM), Hamisi Kigwangala, alisema wawekezaji wamekuja nchini na kuvuna Shilingi trilion 3 za madini Watanzania wamepata bilioni 50 .
“Tumefanya vibaya kwenye sekta ya madini tusiharakishe kwenda kwenye gesi,” alisema.
Ibrahim Sanya (CUF) alitaka kujua kuna utaratibu gani kwa Watanzania kupata hisa kwenye gesi wawekezaji watakapoanza kazi.
Peter Serukamba, alipendekeza kuwa ulinzi kwenye maeneo yanayotafuta gesi, usimamiwe na Jeshi la Wananchi (JW).
Alitoa mfano kuwa, Norway ilipogundua gesi, walijifunza na kuunda sheria mahususi hivyo Tanzania inapaswa kujifunza hivyo.
Mbunge wa Kisarawe (CCM), Suleiman Jafo, alisema mara nyingi wawekezaji wanapokuja wanatakiwa wajenge madarasa, zahanati, lakini rasilimali zilizopo hazilingani na huduma wanazozitoa.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini, alihoji Waziri na Katibu Mkuu walikuwa wapi wiki nzima kuleta rasimu ya sera hiyo ili isomwe na wabunge waweze kuchangia mawazo.
“Wanaopinga wana wasiwasi walishaumwa na nyoka, viongozi na watendaji ni hawa hawa. Tunalipa mabilioni ya fedha kwa sababu ya viongozi hawahawa,” alisema.
Aliongeza, “suala hili lisije likatugombanisha kama Nigeria. Tumepata gesi, serikali ieleze ni ya Muungano au ya Tanzania.”
Alitaka sera ibainishe wazi kwa kuonyesha asilimia ngapi itakwenda kwenye halmashauri ili kuondoa migogoro kuliko mwekezaji kupata faida ya trilioni za fedha kutoka sehemu husika, akaishia kujenga darasa lenye thamani ya Shilingi milioni 40.
Mbunge wa Serengeti (CCM), Kebwe Kebwe, alisema haiwezekani kutengeneza sera pana bila kuwa na mpango mkakati wa kutekeleza sera hiyo.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally Mohamed Keisy, aliwashangaa baadhi ya wabunge na wanasiasa kushabikia rasilimali zinazopatikana kwenye maeneo yao, kulalamika na kufanya maandamano yasiende sehemu zingine.
“Mambo ya kusema watu wa Mtwara na Lindi ndiyo waneemeke zaidi ni upotoshaji, nchi hii ni moja, gesi kutumika upande mmoja hatuwezi kukubali,” alisema.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Martha Mlata, alisema sera ya gesi itaje kampuni itakayokuja kuwekeza.
“Vurugu zinazoendelea katika sakata hili ni Mchina kupigwa vita asije kuwekeza. Mchina hana masharti na anajenga, Mchina ni ndugu yetu ni sawa na marafiki wawili walioishi pamoja mmoja amepata, anataka kumnyanyua mwingine,” alisema.
Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, alisema serikali ina kila sababu ya kwenda kwenye gesi kwa sababu ni muhimu kwa uchumi wa nchi.
Waziri wa Ulinzi, Shamsa Vuai Nahodha, akielezea suala la ulinzi alisema mwaka jana alikuwa kwenye utaratibu wa kutekeleza azma ya kampuni za ulinzi zilinde kampuni ya kuchimbia mafuta.
Alisema kampuni hizo zina vifaa vyenye gharama kubwa na jeshi la Tanzania lina kazi nyingi.
“Tumekubaliana kampuni za kigeni ziendelee Kulinda, lakini meli zote ziwe ndani,”alisema.
“Tumeomba meli mbili, tumetoa dola milioni 18. Desemba meli hizo zitakuwa zimefika na jeshi la ulinzi litachukua nafasi ya kulinda,” alisema.
Awali, Waziri Nishati na Madini, Profesa Sostenes Muhongo, alisema Mei mwaka ujao, Tanzania itakuwa na sera na sheria mpya.
Alisema hadi sasa, Tanzania imegundua futi za ujazo wa trilioni 41.7 ikilinganishwa na trilioni 200 za Msumbiji.
Alisema ili gesi hiyo itumike itachukua kati ya miaka 10 hadi 20 na kwamba kinachofanyika sasa ni utafiti.
“Haimaanishi tunapogawa vitalu hapo hapo gesi inaanza kuchimbwa. Agip ilipewa eneo haikupata kitu, itakuwa ni kosa kubwa sana tutakapoulizwa gesi yenu imefikia wapi tukasema tunasubiri vizazi vijavyo vije kuiona,” alisema.
“Hakuna mkataba mbovu utapita mbele yangu. Njoo wizarani utaiona. Hakuna mkataba ambao umepelekwa bungeni, hiyo itakuwa historia katika nchi yetu,” alisema.
Katibu Mkuu wa Nishati na Madini Aliakim Maswi, alisema wizara yake haiko kwa ajili ya kulea watu, kama kuna watu waliongia mkataba mbaya ni wakati ule siyo sasa.
“Ni lazima tuamue sasa ili nchi iweze kuendelea, lakini ni muhimu ya kuwa na mdhibiti wa mafuta na gesi.”

No comments:

Post a Comment