Sunday, May 19, 2013

Dk. Slaa ambana JK


AMTAKA AELEZE TRILIONI 1.7/- ZILIVYOTUMIKA, LEMA AWASHA MOTO
WAKATI serikali ikishindwa kutoa maelezo ya namna fedha zilizotolewa na serikali na kuidhinishwa na Bunge kwa ajili ya kuhuisha uchumi (Stimulus Package) sh trilioni 1.7 zilivyotumika, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amefufua kadhia hiyo, sasa akimtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza Watanzania fedha hizo ziko wapi.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana katika Kiwanja cha Kwaraa, Babati mjini katika siku ya kwanza ya ziara yake kutembelea maeneo mbalimbali ya wilaya zote za Mkoa wa Manyara, Dk. Slaa alisema serikali haijawahi kutoa majibu sahihi juu ya namna fedha hizo za wananchi zilivyotumika.
Alisema taarifa kutoka ndani ya serikali zinadai kuwa fedha hizo ziliwanufaisha watu wa karibu na Rais Kikwete.
Slaa alisema katika ukaguzi wa fedha za serikali, taarifa muhimu zilizotakiwa zilifichwa, huku Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) akishindwa kupata hesabu za matumizi ya sh bilioni 48 zilivyotumika.
Aliongeza kuwa fedha hizo zingetumika kwa ajili ya manufaa ya Watanzania hasa kwa kuwekeza katika kilimo, nchi ingeweza kuepukana na aibu ya kuwa ombaomba hadi wa chakula kutoka nchi ndogo kama Thailand, Taiwan na Japan.
“Wananchi wa Babati nimezungumzia masuala ya kilimo hapa kwa sababu najua ninyi ni wakulima na hata matatizo yenu mengi huku ni juu ya ardhi yenu ambayo imekuwa ikiporwa au kuhodhiwa kinyemela, huku serikali ikiangalia tu. Wameendelea kutudanganya kama ilivyo kawaida yao kwa muda mrefu sasa, wanadanganya wananchi waliowapatia dhamana ya kuongoza.
“Tunamtaka Kikwete awaambie Watanzania fedha zetu trilioni 1.7 tulizopitisha pale bungeni serikali yake ikisema kuwa ni kwa ajili ya kuwainua wakulima waliopata hasara kutokana na anguko la uchumi, hivyo fedha hizo zilikusudiwa kufufua uchumi, atuambie ziko wapi, zilitumikaje, akina nani walinufaika? Tunasema hivyo kwa sababu taarifa za ndani tulizonazo ni kwamba walipewa maswahiba wa Kikwete.
“Mwaka juzi, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali au CAG kama anavyoitwa na wengi, alibaini kuwepo kwa ubadhirifu mkubwa katika fedha hizo, kiasi kwamba serikali ilikataa kumpatia taarifa kamili ya matumizi ya fedha hizo ili azifanyie ukaguzi. Sasa tunamtaka Rais Kikwete maana yeye ndiye alipeleka bajeti ile bungeni kupitia kwa Waziri wa Fedha, atuambie fedha zetu ziko wapi,” alisema Dk. Slaa.
Aliongeza kusema kuwa fedha hizo zingewekezwa kwenye kilimo kupitia mipango mbalimbali yenye nia ya kuwakomboa Watanzania asilimia 74 wanaotegemea sekta hiyo, huku nchi pia ikitegemea kilimo kwa ajili ya uchumi wake, zingeweza kuwa mkombozi na nchi ingepiga hatua kubwa.
Dk. Slaa ambaye leo anatarajiwa kufanya mikutano ya hadhara katika maeneo ya Balangida na Gendabi, alisema ni aibu kwa nchi yenye utajiri kama Tanzania kuwa ombaomba hadi wa chakula kutoka nchi za nje.
“Ndugu zangu uhuru wetu kama nchi uko shakani mno, tunavyozungumza hapa tumefika mahali tumekuwa ombaomba wa chakula kutoka nje ya nchi, tena kutoka katika nchi ndogo ambazo hazina rasilimali kama hapa, nchi kama Japan, Thailand...
“Naambiwa wakubwa serikalini na washirika wao ndio wanaomiliki maduka makubwa yanayouza chakula kama mchele, ndiyo maana hawataki kuwajali wakulima wetu hapa nchini, badala yake wanatuletea vyakula kutoka Thailand ili wakulima wetu wafe, wao wanufaike,” alisema.
Dk. Slaa alidai kuwa kutokana na wakubwa serikalini na watu aliowaita kuwa ni washirika wao, kumiliki biashara kubwa za uagizaji wa chakula kama mchele na sukari kutoka nje, yametengenezwa mazingira yanayowaathiri wakulima wa Tanzania na wananchi kulazimika kulishwa vyakula visivyokuwa na ubora kutoka nje ya nchi vinavyouzwa madukani.
“Hata sasa kuna chakula kibovu kimeingizwa huko Zanzibar, nasikia wanataka kukivusha bara ili eti kiteketezwe, si ajabu wanatafuta njia ya kukiingiza sokoni kama ilivyo kawaida yao, imefikia mahali watu hawa hawajali chochote kabisa kufanya ufisadi hata unaohatarisha afya za wananchi,” aliongeza.

Bonyeza Read More Kuendelea


Utendaji wa Bunge
Wakati mjadala wa namna Bunge la Tanzania linavyotekeleza utendaji kazi wake mbele ya macho ya Watanzania, hasa namna ambavyo linadaiwa kuwa mhuri wa kupitisha kiulaini hoja za serikali ukizidi kupamba moto katika mijadala mbalimbali nchini, Dk. Slaa amewapongeza wabunge wake, akisema sasa Bunge limefika patamu.
Akiwapongeza wabunge wake, kwamba wamekuwa wakisimama kidete ndani ya Bunge kuiwajibisha serikali kwa niaba ya wananchi tofauti na wanavyofanya wabunge wa CCM walio wengi bungeni, Dk. Slaa alisema kuwa ni unafiki kuzungumzia nidhamu bungeni, wakati serikali inashindwa kusimamia nchi kwa niaba ya Watanzania na kuzuia ufisadi.
Dk. Slaa aliwataka wabunge wake kuongeza kasi kwani waliyonayo sasa bado ni ndogo, kulinganisha na matarajio ya Watanzania wengi aliosema wanataabika kwa kukosa uongozi.
“Wakati nikiwa bungeni, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kenya wakati ule, nafikiri anaitwa Kapalo... Francis Ole Kapalo kama sijakosea, alikuja bungeni wakati wa semina moja hivi, akatuambia Tanzania bado haijawa na Bunge, alituambia kuwa ule ulikuwa ni mkusanyiko tu wa mashehe na wachungaji wanaopiga mihuri hoja za serikali.
“Akasema hadi siku atakaposikia ngumi zimerushwa bungeni, pale atakapoona wabunge wanachachamaa dhidi ya serikali kwa niaba ya wananchi waliowatuma, bila kujali chochote isipokuwa kuwa wawakilishi wa sauti za wasiokuwa na sauti, ndiyo ataamini tumeanza kuwa na Bunge, nami nilikubaliana naye,” alisema Dk. Slaa.
CHADEMA wazindua kampeni Arusha
Katika hatua nyingine, CHADEMA imezindua kampeni zake jijini Arusha kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani wa kata nne; Elerai, Kaloleni, Themi na Kimandolu ambazo madiwani wake walifukuzwa uanachama na chama hicho huku kikitamba kuwa hakina uchaguzi Arusha ila CCM ndio wenye uchaguzi.
“Arusha CHADEMA hatuna uchaguzi, sisi tuna ushindi ila CCM ndio wana uchaguzi,” alisema Godbless Lema, Mbunge wa Arusha Mjini aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kampeni hizo.
Lema alitumia muda mwingi kunadi sera za CHADEMA na kuongeza kuwa madiwani waliofukuzwa ndani ya chama hicho, walipokea rushwa na katika kampeni zao kwenye kila kata, watatoa ushahidi jinsi walivyopokea rushwa.
Huku akishangiliwa na wananchi wa Arusha, Lema alimuonya Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Mkuu wa Wilaya hiyo kujiepusha na kampeni na kutoa tahadhari kuwa wakibainika wanafanya kampeni itakuwa ni makosa makubwa kwao.
Katika kampeni hizo, Lema alirudia kauli yake kuwa mwasisi wa siasa za udini nchini ni Rais Jakaya Kikwete na akaonya siasa zozote za ubaguzi wa kidini wala ukabila huku akiwaasa watu wa Arusha kuonesha ukomavu na kuchana na ukabila.
Lema pia alisema anaendelea na msimamo wake wa kutomtambua Meya wa Jiji hilo, Gaudence Lyimo hivyo anawaomba wana Arusha kumuunga mkono.
Kwa mujibu wa Lema, hayuko tayari kupeleka ushahidi bungeni kuonesha rais ni mdini na ndiyo maana wanaogopa kumdai ushahidi huo.
“Ushahidi huo ninao tayari, upo mwingi ndiyo maana hawawezi kunilazimisha kuwasilisha, mimi nataka kuwasilisha kwa uwazi, sipeleki ushahidi uchochoroni,” alisema Lema huku akishangiliwa.
CHADEMA katika uchaguzi huo imewasimamisha Injinia Jeremiah Mpinga katika Kata ya Elerai, Emanuel Kessy (Kaloleni), Melansi Kinabo (Themi) na Rayson Ngowi katika Kata ya Kimandolu.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya kufukuzwa  kwa aliyekuwa Naibu Meya na Diwani wa Kimandolu, Estomih Mallah; Diwani wa Elerai, John Bayo ambaye kwa sasa amesimama kugombea kwa tiketi ya CUF; aliyekuwa Diwani wa Themi, Reuben Ngowi;  aliyekuwa Diwani wa Kaloleni, Charles Mpanda na Diwani wa Viti Maalumu, Rehema Mohamed.

No comments:

Post a Comment