Monday, May 6, 2013

TAARIFA MAALUM KUTOKA BAVICHA KUMTAKA WAZIRI KAWAMBWA AJIUZULU


WAZIRI KAWAMBWA NA WATENDAJI WA BARAZA LA MITIANI WANAPASWA KUJIUZULU NA KUCHUKUKULIWA HATUA ZA KISHERIA
Tume ya waziri mkuu imetoa ripoti yake ya awali  kuhusu sakata la kufeli vibaya kwa wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2012.
Taarifa hiyo inabaanisha kuwa moja ya sababu za maafa ya kufeli kupindukia kwa wanafunzi wa mwaka jana ni kutumika kwa alama mpya tofauti na miaka ya nyuma  bila hata taarifa kwa wanafunzi waalimu na hata wazazi huku mabadiliko hayo yakiwa ni siri ya baraza la mitiani na wizara ya elimu ambayo kimsingi ndio inasimamia masuala ya kisera ya elimu nchini.
BAVICHA inaona, japo ni taarifa ya awali, kilichosomwa bungeni ni muendelezo wa siasa na mzaa kwa watanzania kunakofanywa na serikali ya CCM kwenye mambo nyeti ya maisha ya watu.
Kwamba  viwango vipya vya madaraja viliwekwa na Baraza la mitiani bila kushirikisha wadau ni kiashiria cha uzembe uliokithiri wa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi ambaye ndiye msimamizi wa Baraza la Mitihani nchini (NECTA) na ambae alipaswa kuhakikisha taarifa hizo ambazo ni za kisera zinafika kwa walengwa.K
Kama Baraza lilifanya maamuzi hayo bila waziri kujua nako kunaashiria uzembe uliobobea wa waziri huyu wa kushindwa kujua kinachofanyika na taasisi zilizo chini yake na kwa maana hiyo ni mzigo kwa taifa na BAVICHA inasisitiza waziri Kawambwa na wasaidizi wake wajiuzulu nyadhifa zao ili kupisha watu wenye uwezo wa kusimamia sekta hii na taasisi zilizo chini yake.
Pia kwa kuwa ripoti hiyo inaonyesha kuwa viwango vipya vya madaraja vilitumika pasi walengwa kuhusishwa na kwamba tayari malaki ya vijana wameathirika kwa uzembe huu ambapo wengine wamepoteza maisha kwa kujinyonga, ni wazi kua watendaji wa Baraza la Mitiani la Taifa wanapaswa kuchukuliwa hatua za haraka kwa kuondoshwa kwenye nafasi hizo sambamba na waziri anayewasimamia kujiuzulu.
Licha ya kufukuzwa mara moja kwenye nafazi zao, BAVICHA inataka sasa, kutokana na ripoti hii, Waziri na Watendaji wa NECTA wachukuliwe hatua za kisheria kwa kusababisha mauaji ya vijana 3 waliojinyonga kutokana na matokeo mabovu kwa uzembe uliokithiri.
BAVICHA inakumbusha kuwa kurudiwa kupangwa kwa matokeo ya kidato cha nne sio tiba ya kufeli kwa wanafunzi bali ni lazima sanaa za kisiasa zinazochezwa na serikali ya CCM kwa kuwa imeacha kushukua hatua ngumu za wahusika waliosababisha aibu hii na pia  kushughulikia matatizo ya msingi ya sekta ya elimu ili kuboresha ubora wake.
BAVICHA tunasisitiza kuwa ubovu wa matokeo ya mwaka jana ni kilele cha kudharauliwa kwa walimu wa nchi hii na serikali ya CCM, mazingira mabovu ya kutolea elimu ambapo zipo shule zisizofanana na shule, idara ya ukaguzi wa shule kushindwa kufanya kazi yake kutokana na kutokuwa na meno  na mfumo mbovu usiokidhi mahitaji ya sasa ya taifa na dunia.
Imetolewa leo tarehe 4.5.2013 jijini Dar es salaam na;
Deogratias Munishi
Katibu Mkuu –BAVICHA
+255715 887712

No comments:

Post a Comment