UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
kwa Mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, toleo la 2013;
napenda kuchukua fursa hii kuwasilisha maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na CHADEMA, kuhusu mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya 2012/2013
na makadirio ya mapato na matumizi katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa
mwaka wa fedha 2013/2014.
Mheshimiwa Spika, Kufuatia
shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki, Kigango cha Olasiti, Jimbo Kuu
Katoliki la Arusha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatoa salamu za Rambi
Rambi na pole nyingi kwa Kanisa Katoliki nchini na kwa familia za marehemu na majeruhi wa
shambulio hilo. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalaani kwa nguvu zote
kitendo hicho cha kigaidi dhidi ya raia wasio na hatia waliokuwa katika ibada
ya kumwabudu Mungu.
Mheshimiwa Spika,
hii ni changamoto kubwa kwa Serikali ya CCM ambayo mara zote imekuwa
ikishindwa kuzuia matukio ya
kihalifu dhidi ya raia na mali zao,
lakini imekuwa hodari kuzuia ukuaji wa demokrasia nchini kwa kuvikandamiza
vyama vya upinzani na hasa CHADEMA.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka kuikumbusha Serikali na wananchi wote kwamba tarehe
24 Oktoba, 2012 Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Arusha Shekhe Abdul Karimu Jonjo
alilipuliwa kwa bomu nyumbani kwake eneo la Esso mjini Arusha, na taarifa za
uchunguzi wa tukio hilo bado hazifahamiki. Aidha, mwezi Novemba, 2012 Katibu wa
Mufti wa Zanzibar, Sheik Fadhil Soraga, alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana na
bado hakuna za uchunguzi juu ya watu waliohusika na uhalifu huo.
Mheshimiwa Spika,
muda mfupi baadaye, makanisa yalichomwa moto huko Zanzibar na Dar es Salaamu na
watu wasiojulikana na mpaka leo hakuna taarifa ya kuwashughulikia waliohusika
na uhalifu huo.
Mheshimiwa Spika,
jaribio lililoshindwa la kumuua Padre Ambrose Mkenda wa Kanisa Katoliki Zanzibar lililofanyawa na watu wasiojulikana
pia, ukichanganya na matukio ya kuchoma moto makanisa na kushambuliwa kwa
viongozi wengine wa dini tayari lilishatoa picha kwamba viongozi wa dini na
taasisi zao wanalengwa na mashambulizi ya kigaidi.
Mheshimiwa Spika,
tukio la kuuwawa kwa kupigwa risasi kwa Padre Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki
Zanzibar tarehe 13 Februari, 2013 tayari Serikali ilikuwa inajua kwamba
viongozi wa dini wanawindwa na magaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni kwanini Serikali haikutoa ulinzi kwa viongozi
wa dini wakati tayari ilijua kuwa viongozi wa dini ni walengwa wa mashambulio
ya kigaidi?
Mheshimiwa Spika,
baada ya mashambulio hayo kwa viongozi wa dini na makanisa, Serikali ilijua
kwamba kuna makundi ya watu (magaidi) yanalenga makanisa ili kuyachoma moto.
Serikali haikutoa ulinzi kwa makanisa, matokeo yake jana tarehe 5 Mei, 2013
Kanisa limelipuliwa kwa bomu huko Arusha. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka
kujua ni kwa nini mpaka leo Serikali haijatoa ulinzi kwa makanisa ilhali
inafahamu kwamba makanisa yanalengwa na mashambulizi ya kigaidi? Aidha Kambi
Rasmi inaitaka Serikali itoe maelezo katika bunge hili, inahitaji watu wangapi
wauwawe ndipo ichukue hatua?
Mheshimiwa Spika, ni
hivi karibuni tu (22 Aprili, 2013) Jeshi la Polisi lilitoa angalizo kwamba
kunadalili za kuibuka kwa Al Quaeda na Al Shabab nchini. Hata mwezi mmoja
haujapita, Kanisa limelipuliwa kwa bomu, Kambi Rasmi ya Upinzani inaliuliza Jeshi
la Polisi, kama walikuwa na taarifa za ki-intelijensia kuhusu Ugaidi mbona
hawakuchukua tahadhari?
Mheshimiwa Spika, kutokana
na matukio haya ya kigaidi yanayoendelea
kushamiri katika nchi yetu na Serikali ikiwepo na kunyamaa bila kuchukua hatua
za makusudi za kuyakomesha, Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili na wananchi wote kwa
ujumla KAMA INA UHALALI WA KUENDELEA
KUTAWALA IKIWA IMESHINDWA KUZUIA MATUKIO YA KIGAIDI KAMA HAYA NA IKIWA PIA
IMESHINDWA KUWACHUKULIA HATUA WALE WALIOHUSIKA NA VITENDO VYA KIGAIDI.
Mheshimiwa Spika, baada
ya kutafakari kwa kina jinsi ambavyo Serikali haithamini tena uhai na utu wa
mtanzania kwa kuangalia matukio ya mauaji na unyanyasaji wa kiimani ambao una
malengo ya moja kwa moja ya kuvunja amani na utulivu wa nchi yetu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa
na CHADEMA, imeona kwamba kuna haja ya
kutafakari tena kama taifa uzito wa
jambo hili kwa kuwa ni muhimu kwa
mustakabali wa taifa letu. Aidha Kambi
Rasmi ya Upinzani inapenda kuchukua nafasi hii kuionya Serikali kuacha kufanya mzaha
na amani ya nchi yetu kwani kwa kutoshughulikia wahalifu wanaoivunja amani yetu
ni sawasawa na kuivuja amani yenyewe moja kwa moja. Kwa kutambua umuhimu wa amani
na utulivu katika maendeleo ya Taifa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kipindi
hiki, itajielekeza kwenye mambo machache ya msingi ambayo ambayo yanatakiwa
kufanyiwa kazi ili kujenga mustakabli bora wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA inapenda wananchi wote wajue
kwamba kamwe haitakaa kimya kwa udhalimu wowote dhidi ya raia wa Tanzania. Aidha,
Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa angalizo kwa Serikali na wananchi wote kwamba
kama hatutasimama kidete kama taifa kupinga kwa nguvu zote matukio yoyote yenye
kuhatarisha usalama na uhai wa raia wa taifa letu, kuna hatari kubwa ya matukio
haya kuzoeleka na kuonekana kuwa ni ya kawaida na hali hiyo itakapotokea, basi
nchi itaingia katika machafuko makubwa kwani sheria za nchi zitakuwa
zimeshindwa kuweka utaratibu katika nchi.
Bonyeza Read More Kuendelea
- HAKI YA KUFANYA
MIKUTANO YA SIASA
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya
Bunge na. 3 ya mwaka 1988 (The Parliamentary Immunities, Powers and
Privileges Act) mbunge ana haki na uhuru wa kufanya mikutano ya hadhara katika
Jimbo lake na mamlaka zote za Serikali zinazohusika zinawajibu wa kuwezesha
mikutano hiyo kufanyika. Lakini kwa
masikitiko makubwa vyombo vya dola hasa polisi imekuwa ikizuia kufanyika kwa
mikutano hiyo na Spika wa Bunge amabaye kimsingi anatakiwa kuhakikisha kuwa
Sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge inaheshimiwa amekaa kimya wakati haki na madaraka ya bunge
yanadhulumiwa.
Mheshimiwa Spika, wabunge waliozuiliwa
kufanya mikutano na wananchi wao ni
pamoja na Mheshimiwa John Mnyika, Mheshimiwa Tundu Lissu, Mheshimiwa Meshack Opulukwa,
Mheshimiwa Ezekia Wenje, Mheshimiwa Said Arfi, Mheshimimiwa Magdalena Sakaya,
na Mheshimiwa God Bless Lema.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua kama kuna sera inayokataza
wabunge wa upinzani kufanya mikutano na wananchi katika majimbo yao. Kama
hakuna sera, ni kwa nini Serikali inawazuia wabunge kufanya mikutano na
wananchi wao?
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, chama cha siasa kilichopata usajili wa
kudumu, kina haki ya kufanya mikutano ya siasa na kupatiwa ulinzi kwa mikutano
hiyo na Jeshi la Polisi. Hata hivyo, Jeshi la Polisi limeonesha upendeleo
mkubwa kwa namna linavyoshughulikia mikutano ya vyama vya siasa vya Upinzani na
ile inayofanywa na CCM. Hivyo basi, wakati sheria ya vyama vya siasa inataka
vyama vya siasa vitoe taarifa kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya, na kwa kiasi
kikubwa Makamanda wa Polisi wa Wilaya wamekuwa wakiruhusu mikutano hiyo,
Kumekuwa na tabia ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa kuingilia masuala ya mikutano
ya vyama ambayo hayawahusu kisheria.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Dkt. Emmanuel Nchimbi, chini ya uongozi wa
Jaji Ihema, iliyotolewa tarehe 9 Oktoba, 2012 “kuwepo kwa zuio la mikutano ya siasa ya CHADEMA mkoani Iringa wakati
wa zoezi la Sensa ya watu na makazi linathibitishwa na amri ya utendaji
(Operation Order) ya Kamanda wa Polisi Mkoa
(SAC Michael Kamuhanda) ya tarehe 1 Septemba, 2012. Uhalali wa amri au
zuio hili ulithibitishwa pia na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini katika barua
yake yenye Kumb. Na. DA.112/123/01/34 ya tarehe 28/08/2010 na wakati wa
mahojiano na Kamati ya Uchunguzi tarehe 22 Septemba, 2012.”
Mheshimiwa Spika,
hata hivyo, uhalali wa kauli hii umehojiwa na Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora. Katika taarifa yake ya tarehe 10 Oktoba, 2012 Tume ya Haki za
Binadamu ilisemayafuatay: “ Ili pawepo na
utawala bora mamlaka zote za Serikali ni lazima zifuate utawala wa sheria.
Uchunguzi umebaini kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda,
tarehe 02/09/2012 katika utekelezaji wa majukumu yake alikiuka Sheria ya vyama
vya Siasa (Cap 258 RE. 2002) kifungu cha 11(a) na (b) na Sheria ya Polisi (Sura
ya 322) kwa kuingilia kazi za OCD wa Mufindi na kutoa amri ya kuzuia shughuli
za CHADEMA wakati yeye hakuwa “Officer In-charge” wa polisi eneo husika. Kwa
maana hiyo, amri aliyoitoa haikuwa halali kwa kuwa ilitolewa na mtu ambaye
hakuwa na mamlaka kisheria kutoa amri hiyo. Haya ni matumizi mabaya ya mamlaka,
hivyo ni ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Aidha hatua ya Msajili wa Vyama
vya Siasa, Mhe. John Tendwa kuwaandikia
barua viongozi wa vyama vya siasa kuwataka kusitisha shughuli zao kwa sababu ya
sensa ilikiuka misingi ya utawala bora kwani maelekezo yaliyotolewa ndani ya
barua hizo yanakinzana na sheria ya takwimu Na. 1 ya mwaka 2002 inayotoa fursa
kwa wananchi kuendelea na kazi zao wakati wa sensa pia ni kinyume na sheria ya
vyama vya siasa (Cap 258 RE. 2002)
kifungu cha 11 (a) na (b) inayotoa fursa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli
zake bila kuingiliwa.”
Mheshimiwa Spika,
Aidha, katika mapendekezo yake, Tume ya Haki za Binadamu ilisema yafuatayo
kuhusiana na polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa; “ Jeshi la Polisi na Msajili wa Vyama vya Siasa waepuke kufanya maamuzi
au matendo yanayoibua hisia za ubaguzi au upendeleo miongoni mwa jamii wakati
wanapotekeleza majukumu yao ya kisheria. Mfano Jeshi la Polisi lilizuia
mikutano ya CHADEMA kwa sababu ya sensa wakati huohuo Chama cha Mapinduzi (CCM)
walikuwa wakifanya uzinduzi wa Kampendi huko Zanzibar. Aidha rai ya Msajili wa
vyama vya Siasa haikuzingatiwa kwa upande wa CCM Zanzibar huku CHADEMA
wakishurutishwa na Polisi kutii rai hiyo.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali itoe kauli mbele ya bunge hili kama
inakubaliana na taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu. Aidha Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali ilieleze Bunge hili hatua ilizochukua kama zipo
dhidi ya Makamanda wa Polisi wa Mikoa ambao wamekuwa wakiingilia mikutano ya
vyama vya siasa ambayo imekabidhiwa kisheria kwa Makamanda wa Polisi wa Wilaya.
Mheshikiwa Spika,
Mashinikizo ya wakuu wa Mikoa, Wilaya na Mawaziri uliikera hata Kamati ya Jaji
Ihema iliyoteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani mwenyewe. Kwa mfano katika
mapendekezo yake, Kamati ilisema yafuatayo, kuhusiana na CCM kutumiwa na
kulitumia Jeshi la Polisi kwa manufaa yake. “Muundo uliopo wa Jeshi la Polisi uangaliwe upya kisheria ili kuziba
mianya inayotoa nafasi kwa wanasiasa kulitumia Jeshi hilo kwa manufaa ya
kisiasa. Nafasi za Mkuu wa Wilaya na
Mkuu wa Mkoa kiutendaji ziangaliwe upua ili zisitumike na mhusika kwa ajili ya
manufaa ya kisiasa”.
Mheshimiwa Spika,
Mapendekezo haya yanakwenda sambamba na kauli aliyoitoa Mwenyekiti wa CCM Taifa
Dkt. Jakaya Kikwete alipokuwa akihutubia mkutanao wa Halmashauri Kuu ya CCM –
Dodoma kwamba CCM isitegemee Jeshi la Polisi kujibu hoja za wapinzani. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaliasa Jeshi la Polisi liache kazi za siasa na badala yake
wazingatie sheria na taratibu zinazowaongoza ili kurejesha imani ya jamii kwa
jeshi hilo ambayo kwa sasa inakaribia kutoweka kabisa.
Mheshimiwa Spika,
kwa miaka mingi CCM na viongozi wake imekuwa ikivikejeli vyama vya Upinzani kwa
kuviita vyama vya msimu. Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, CHADEMA kimethibitisha
kuwa si chama cha msimu kwa kufanya mikutano na maandamano kwa wingi kuliko
chama kingine cha siasa. Matokeo yake sasa CCM na Serikali yake wanakula njama
ya kuzuia vyama vya upinzani kufanya mikutano ya siasa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani imeona mapendekezo yaliyoandaliwa na Msajili wa Vyama
vya siasa, ambayo lengo lake ni kupiga marufuku mikutano ya vyama vya siasa
wakati ambao sio wa kampeni za uchaguzi. Kwa mapendekezo haya, haki ya vyama
vya siasa kufanya shughuli za kisiasa itakuwa imeuwawa na Serikali hii ya CCM
kwa kumtumia msajili wa vyama.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo
haya ya Msajili wa vyama vya siasa ambayo lengo lake ni kufanya marekebisho
kwenye sheria ya vyama vya siasa ambayo yakikubaliwa yatapelekea kupiga marufuku mikutano ya siasa
yanatokana na shinikizo la CCM na yana lengo la kuidhibiti CHADEMA. Hii ni kwa sababu, Taarifa ya Kamati ya Jaji Ihema iliyoundwa na mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Nchimbi inasema
hivi: “Kasi ya CHADEMA kuendesha mikutano
katika sehemu mbalimbali hapa nchini kwa ajili ya kujiimarisha kichama,
imepokewa kwa hisia tofauti na vyama vingine vya siasa. Wakati kuna makundi ya
watu katika jamii wakidhani kuwa hiyo ni haki yao kama chama cha siasa
kinachotaka kukua na kukubalika kisiasa , wengine wanaona mikutano hiyo ya
hadhara ya CHADEMA kama ni kuwapunguzia muda wa kufanya shughuli zao za
maendeleo hasa baada ya kipindi cha uchaguzi kumalizika. Katibu Mkuu wa CCM
Wilson Mukama alishauri kufanyiwa marekebisho Sheria ya vyma vya siasa Namba 5
ya mwaka 1992 itakayoweka wazi shughuli za vyama vya siasa baada ya Uchaguzi
Mkuu. Alisisitiza kuwa shughuli za siasa baada ya Uchaguzi Mkuu zihamie Bungeni
kwa wanasiasa kuhoji mipango wa maendeleo ya Serikali na matumizi ya rasilimali
za nchi na wananchi waachwe wachape kazi zao za maendeleo”.
Mheshimiwa Spika,
Ushauri wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM ndio uliochukuliwa na kufanyiwa kazi na
Msajili wa Vyama vya Siasa. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
itoe kauli mbele ya bunge hili juu ya hatua zozote kama zipo, za kutekeleza
mapendekezo haya ya Kamati ya Jaji Ihema.
Mheshimiwa Spika,
haki ya kufanya mikutano ya siasa na mikutano mingine yoyote na kwa wakati
wowote, inatambuliwa na kulindwa na katiba yetu. Ibara ya 20(1) ya katiba yetu
inasema,”kila mtu anao uhuru wa kukutana nawatu wengine kwa hiari yake na kwa
amani,kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa
mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa
kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi
mengineyo”. Uhuru huu haujawekewa masharti ya muda au wakati wa
kukutana au kuchanganyika na watu kwa wakati au kipindi fulani. Kwa hiyo
mapendekezo ya msajili wa vyama vya siasa ya kupiga marufuku mikutano ya siasa
kwa nyakati zisizokuwa za kampeni za uchaguzi yanaenda kinyume na katiba na
hayakubaliki.
Mheshimiwa Spika, ni
ajabu iliyoje kwamba wakati nchi nyingine jirani yetu zinapanua demokrasia kwa
kupanua haki ya kufanya mikutano na maandamano, serikali hii ya CCM inapendekeza kuminya demokrasia kwa kuthibiti na kufifisha haki hizo. Na hii
inafanyika wakati taifa likiwa kwenye mchakato wa kuandika katiba mpya. Jirani
zetu wa Kenya katika katiba yao mpya ya mwaka 2010 wameamua ifiatavyo katika
ibara ya 37 ya katiba yao “kila mtu ana haki, kwa amani na bila kuwa
na silaha kukutana, kuandamana, kufunga njia au eneo au jengo( to picket) na
kupelekea malalamiko katika mamlaka za umma”. Marafiki zetu wa Zimbabwe
baada ya miaka mingi ya utawala wa kiimla wa ZANU –PF nao wamepata katiba mpya iliyopitishwa mwezi
februari mwaka huu. Na katiba yao inasema yafuatayo katika ibara ya 58(1) na 59
“
kila mtu ana haki ya uhuru wa kukutana na kuchanganyika na haki ya kutokutana
na kuchanganyika na wengine”. Aidha, kila mtu ana haki ya kuandamana na
kuwasilisha malalamiko lakini haki hizi zitatekelezwa kwa amani”. Kwa maana
hiyo masharti pekee ya haki ya kukutana, kuandamana na kuchanganyika na watu
wengine katika katika Jamhuri ya Kenya na Zimbabwe ni kwamba, maandamano au
mikutano hiyo ifanyike kwa amani. Badala ya kujifunza kwa wenzetu wanaopanua
haki serikali hii ya CCM inatuelekeza njia nyingine ya kuminya na kufifisha
haki.
- MASLAHI
NA STAHILI ZA ASKARI POLISI
Mheshimiwa Spika, mara
zote Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikitetea maslahi bora na mazingira
mazuri ya kazi kwa watumishi wa Serikali na hata wa Sekta binafsi ili kuwapa
motisha watumishi jambo ambalo huongeza tija katika uzalishaji na hatimaye
kukuza uchumi.
Mheshimiwa Spika,
katika maboresho ya maslahi na stahili mbalimbali kwa watumishi wa Serikali,
askari wa Jeshi la Polisi wamekuwa wakiachwa nyuma sana. Tumeshuhudia posho
zikipanda mara dufu kwa kada nyingine za watumishi Seikalini huku fedha za
kujikimu kwa askari wa Jeshi la Polisi na Magereza zikiwa palepale licha ya
gharama za maisha kupanda kila kukicha. Ikumbukwe kwamba, kitendo cha gharama
za maisha kupanda huku mishahara na stahili nyingine za askari kubaki katika
kiwango kilekile cha zamani ndicho kinachofanya askari wetu kuingia tamaa ya
kupokea rushwa na kutoa vitisho kwa raia ili kujipatia kipato cha ziada
kunusuru maisha yao na wategemezi wao.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa jeshi la polisi, linafanya kazi zinazoshabihiana na Jeshi la Wananchi,
na kwa kuwa askari wa Jeshi la Polisi wanahitaji chakula kama vile ambavyo
Jeshi la Wananchi wanahitaji ili waweze kufanya kazi kwa ufanisi, Hivyo basi, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kuongeza posho ya chakula (Ration allowance) kwa askari wa Jeshi la
Polisi ili walau posho hiyo ishabihiane
na posho ya Jeshi la Wananchi ambayo kwa sasa ni shilingi 7,500 kwa siku kwa
akari mmoja. Pamoja na kwamba posho hii ya shilingi 7,500 kwa Jeshi la Wananchi
haitoshi, kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kuiboresha ili majeshi yetu yaweze kukabiliana na ugumu wa
maisha.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaamini kabisa kwamba jambo hili linawezekana kama
tukipunguza posho mbalimbali ambazo si za lazima (discretionary allowances).
Itakumbukwa kwamba wakati wa bajeti ya Wizara ya maji, Mheshimiwa Spika alisema
kwamba fedha iliyoongezwa katika bajeti ya maji ya shilingi bilioni 181
haikutoka kwingine isipokuwa kwenye posho mbalimbali. Kwa hiyo Kambi Rasmi ya
Upinzani inaamini kabisa kwamba ikiwa Serikali hii ya CCM itajibana kidogo na
kujiondolea posho zisizo za lazima, sio tu kwamba Polisi watapata Ration
Allowance ya tunayopendekeza ya shilingi 7,500 bali pia fedha hizo zinaweza
kuelekezwa pia kwenye ujenzi wa nyumba za polisi na magereza na hivyo polisi
wakawa na nyumba nzuri na maisha yao yakawa ya staha zaidi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali kuboresha posho ya chakula kwa askari
wa jeshi la polisi na magereza kama tulivyopendekeza ili waweze kukabiliana na
ugumu wa maisha.
- UMRI
WA KUSTAAFU KWA MAAFISA WA POLISI NA MAGEREZA
Mheshimiwa Spika,
Kati ya marekebisho ya sheria mbalimbali yaliyofanyika katika bunge lilipita,
ilikuwa ni kuongeza umri wa kustaafu kwa akari polisi na magereza kutoka miaka
50 kwenda 55 na kutoka miaka 55 kwenda 60.
Mheshimiwa Spika,
kumekuwa na ukimya juu ya utekelezaji wa sheria hiyo, kwa upande wa Serikali na
hivyo kuwaacha maafisa wa polisi na magereza wanatakiwa kustaafu njia panda kwa
kutojua wafuate utaratibu wa zamani wa kustaafu au wasubiri utekelezaji wa
sheria hii mpya.
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kutoa mwongozo kwa maafisa wa polisi na magereza wanaotakiwa kustaafu
juu ya sheria ya kufuata.
- UTARATIBU
WA KUJIENDELEZA KIMASOMO NJE YA KITUO CHA KAZI KWA MAAFISA WA POLISI NA
MAGEREZA.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa General Service Order (GSO) na sheria nyingine za kazi, mtu
akiajiriwa kwa mara ya kwanza (first appointment) na akataka kujiendeleza
kimasomo nje ya kituo chake cha kazi
anatakiwa kukaa kazini kwa muda wa miaka miwili au mitatu ndipo aweze kuomba
ruhusa ya kwenda masomoni.
Mheshimiwa Spika,
Jeshi la Magereza wamechakachua sheria na kujiwekea utaratibu wao kwamba ili
askari aweze kupata kibali cha kwenda masomoni ni mpka akei miaka sita, yaani
aende lizo 2 ndipo aombe kibali cha kwenda masomoni.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaona huo ni urasimu usio na tija na ni kulidumaza
jeshi la magereza kwani kwa utaratibu huo wengi watakata tamaa ya kujiendeleza
kielimu na kwa maana hiyo ufanisi wao katika jeshi utakuwa unapungua. Aidha kwa
kuzingatia ugumu wa kupata nafasi (admission) katika vyuo, ambapo mtu anaweza
kuomba na kukosa nafasi hata kwa miaka miwili mfululizo, kama masharti
yataendelea kuwa askari akae kazini miaka sita ndipo aombe nafasi, kuna
uwezekano ikamchukua askari hata miaka kumi kabla hajapata nafasi ya kuosoma,
na akija kupata umri wake unaweza ukawa umeenda sana kiasi cha kuathiri masomo
yake.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuliagiza Jeshi la Magereza kufuta
haraka sana masharti hayo ya kukaa kazini miaka sita ndipo askari apate fursa
ya kujiendeleza kimasomo kwani hauna tija hata kidogo.
- HALI
DUNI YA MAISHA KWA ASKARI MAGEREZA
Mheshimiwa Spika,
askari magereza wanaishi katika mazingira magumu kiasi ambacho wanashindwa
kufanya kazi zao kwa ufanisi. Askari
hawa wanashinda mashambani na maeneo ya kazi kusimamia wafungwa, wanakesha
magerezani kuwalinda wafungwa wakati wafungwa wamelala na wanapopata muda wa
kupumzika, hakuna mahali pazuri pa kupumzika, nyumba zao zipo katika hali duni
sana.
Mheshimiwa Spika,
kusema kweli wanaishi maisha magumu na wanajiona kuwa wao ndio wafungwa kuliko
wafungwa wenyewe. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kujibana kama
ilivyojibana kwenye bajeti ya Wizara ya Maji ili kujenga nyumba za Askari
Magereza na kuboresha makazi yao.
- HALI
YA MAGEREZA NA MSONGAMANO WA WAFUNGWA
Mheshimiwa Spika, Mfumo wetu wa Magereza unakabiliwa na msongamano mkubwa
wafungwa na mahabusu. Kwa mujibu
wa Kamishana
wa Jeshi la Magereza nchini, idadi ya wafungwa na mahabusu ni hapa nchini ni 36,365
amabapo wafungwa ni 18,452 na mahabusi ni 17,913
na Uwezo wa hifadhi magerezani ni nafasi 29,552.
Aidha kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya
Mambo ya ndani Magereza yana uwezo wa
kuhifadhi wafungwa na mahabusu 22,669 lakini kwa sasa inatunza zaidi ya
wafungwa na 45,000 kiwango ambacho kimezidi kwa zaidi ya asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, Pamoja na takwimu hizi kuwa tofauti ukweli
ni kwamba magereza yamefurika. Lakini pia tofauti ya idadi iliyotolewa na
Kamishna wa Jeshi la Magereza na ile ya tovuti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi ni uthibitisho kwamba hata serikali haijui kuna wafungwa wangapi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge
hili ni kitu gani kinachosababisha msongamano mkubwa hivi katika magereza yetu.
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Mahakama kutoa adhabu ya vifungo vya
nje na faini na kazi mbalimbali katika jamii kama njia mojawapo ya kupunguza
msongamano wa na wafungwa magerezani.
- HALI DUNI YA LISHE NA AFYA KWA WAFUNGWA NA MAHABUSU
Mheshimiwa Spika, fedha inayotolewa na Serikali kwa mlo wa mfungwa mmoja ni
shilingi 577 tu ambayo ni sawa na bei ya chupa ndogo moja tu ya maji. Huu ni
ukiukwaji mkubwa wa haki msingi za binadamu kwa maana kutompa mtu chakula cha
kutosha maana yake unamtakia kifo. Hii ina maana kwamba haki ya kuishi ambayo
ni ya kikatiba inakiukwa na Serikali kwa kutoa kiwango ambacho hakimtoshi mtu
kuishi.
Mheshimiwa Spika, wafungwa na mahabusu nchini wanakosa huduma muhimu za
kibinadamu ikiwemo mlo kamili, matibabu na maji. Viwango vya chakula
cha wafungwa magerezani vimewekwa kwa mujibu wa Kanuni za Magereza za mwaka
1968 kifungu cha 23(1) zilizotungwa kwa mujibu wa Sheria ya Magereza (Prisons
Act ya Mwaka 1967). Kwa mujibu wa kanuni hizo, wafungwa wanatakiwa kula milo
miwili: (asubuhi kifungua kinywa gramu 450 ambazo ni sawa na gramu 150 za unga
wa uji na gramu 300 za vitafunwa. Mchana wanapata gramu 500 ambazo ni milo
miwili ambayo ni gramu 250 za mchana na usiku gramu 250 ambazo hutolewa kwa
pamoja). Licha ya mlo huu kuwa hautoshi lakini pia umekuwa hauna makundi yote
ya lishe.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kuongeza kiasi cha fedha ya
mlo kwa mfungwa ili kiendane na gharama halisi za maisha kwa sasa. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua
ni kwanini wafungwa wapewe chakula mara mbili tu wakati kiafya mtu anatakiwa kupata mlo mara
tatu kwa siku? Kambi Rasmi ya Upinzani
inahoji ni kwanini wafungwa wanalazimishwa kulala saa kumi jioni badala ya saa
mbili usiku baada ya mlo wa jioni?
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwapa wafungwa milo mitatu (yaani kifungua
kinywa, chakula cha mchana na chakula cha jioni) kwa awamu tatu na sio
kuwapa kuwapa chakula cha mchana na cha
jioni kwa pamoja kwani kwa kufanya hivyo ni kuwatesa wafungwa kwa makusudi.
Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kubadili muda wa kulala
wafungwa kutoka saa kumi jioni hadi saa mbili usiku ili waishi kama binadamu
wengine. Kitendo cha wafungwa kutokuwa huru tayari ni adhabu ya kutosha,
kuongeza adhabu nyingine zisizo rasmi kama vile kupata milo miwili tu na
kulazimishwa kulala saa kumi jioni ni ukiukwaji wa haki za binadamu.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani pia inataka kujua kama
kuna huduma maalumu za lishe, matibabu na malazi kwa waathirika wa UKIMWI,
wajawazito na akina mama wanyonyeshao magerezani.
Mheshimiwa Spika, Ibara
ya 13 (6 )(d) na (e) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inakataza kumdhalilisha mtu au kumpa adhabu za
kumtweza utu wake. Mfumo wa upekuaji unaofanywa na askari magereza dhidi ya
wafungwa na mahabusu bila shaka yoyote ni wa kiudhalilishaji.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani haipingi wafungwa au mahabusu kupekuliwa au kukaguliwa
mara waingiapo gerezani lakini walau upekuaji huo uwe wa faragha kuliko ilivyo
sasa hivi ambapo wafungwa na mahabusu huvuliwa nguo mbele ya kadamnasi na
kulazimishwa kuinama wakiwa utupu ili kuhakiki kama hawajaficha chochote kwenye
sehemu zao za siri bila kujali hata tofauti ya umri wa wafungwa na mahabusu
wenyewee. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwatendea wafungwa na
mahabusu kama binadamu na sio kama wanyama.
- JESHI LA ZIMA MOTO NA UOKOAJI
Mheshimiwa Spika, kumekuwepo
na ukusanyaji wa fedha wa lazima kutoka kwa wafanyabiashara kwa ajili ya zima
moto bila kujua kama fedha hizo ni kwa ajili ya malipo ya ada, vifaa vya
kuzimia moto au huduma nyingine. Fedha hizo zimekuwa zikitozwa kwa kutumia
nguvu bila kuwapa raia elimu ya kutosha juu ya matumizi ya fedha hizo.
Mheshimiwa Spika, Kambi
Rasmi ya Upinzani inataka kujua kiasi cha shilingi 30,000 hadi 300,000
kinachotozwa na jeshi la zima moto bila kutoa kifaa cha kuzima moto (fire
extinguisher) ni kwa madhumuni yapi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inakemea tabia ya Serikali kuweka nguvu kubwa zaidi
kununua vifaa vya kuumiza na kuangamiza watu badala ya kununua vifaa vya
uokoaji wa maisha ya watu . Nasema hivi kwa kuwa pingu za kuwafunga na mabomu ya kuwapiga wana CHADEMA na raia wanaodai
haki zao hayakosekani lakini kunapotokea ajili ya moto au maghorofa kuporokoka,
au meli kuzama watu hufa na Serikali kubaki na kisingizio cha kuchefua cha
ukosefu wa fedha za kununulia vifaa vya uokoaji.
Kambi Rasmi ya Upinzani
inaitaka Serikali kuliimarisha Jeshi la Zima moto na uokoaji kwa kununua vifaa
vya kutosha na kuwapatia mafunzo ya uokoaji maafisa wa jeshi hilo ili liweze
kukabiliana na maafa mbalimbali yanayotokea hapa nchini
- UONEVU
UNAOFANYWA NA ASKARI WA VYEO VYA JUU DHIDI YA WADOGO
Mheshimiwa Spika,
kumekuwa na tabia ya Askari wenye vyeo vya juu kuwanyanyasa askari wa vyeo vya
chini jambo ambalo linawakatisha tamaa askari hao kufanya kazi kwa moyo.
Unyanyasaji huo unafanywa kwa makusudi ili kuwaziba midomo Askari wa vyeo vya
chini wasihoji kuhusu haki na stahili zao wawapo kazini.
Mheshimiwa Spika, unyanyasaji
huo umechukua sura mpya baada ya askari wa kada ya chini kusingiziwa kuwa ni
vichaa ili tu kubatilisha ukweli wanaousema kuhusu utendaji
mbovu na ubadhirifu unaofanywa na mabosi
wao. Kwa mfano PC MESIAKI SAMSON Na.
E.6767 wa Central Police, Arusha alisingiziwa na kuwa ni kichaa na SP
Mushumbusi wa Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam aliyekuwa Arusha kusikiliza
matatizo ya Polisi wa vyeo vya chini na
kutoa amri PC MESIAKI SAMASON kwenda
kupimwa maradhi ya Akili Katika Hospitali ya Mount Meru Arusha kutoka na
kuhoji watu wasi na sifa kupelekwa kusomea nyota wakati wenye sifa wanaachwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani inalaani tukio hilo kwani ni la kiudhalilishaji kwa
kuwa PC SAMSON MESIAKI hakukutwa na maradhi yoyote ya akili na hajawahi kwa na
historia ya maradhi ya akili.
Mheshimiwa Spika,
tangu hapo askari huyu ameendelea kunyanywasa na mabosi wake mpaka anashindwa
kufanya kazi kwa kuwa hapewi ushirikiano wowote. Kambi Rasmi ya Upinzani
inamtaka Waziri wa Mambo ya ndani kuingilia kati suala hilo na kutafuta
ukweli kwani inaonekana kuwa kupigwa
vita kwa askari huyu ni kutokana na kuwa na taarifa za utendaji mbaya wa
wakubwa zake na ndio maaana wanatafuta njia za kumfanya aonekane ni kichaa ili
taarifa alizo nazo zisitiliwe maanani.
- KUPOROMOKA
KWA MAADILI YA KAZI YA JESHI LA POLISI NA JINSI JESHI HILO LINAVYOTUMIWA
KUTIMIZA MASLAHI YA KISIASA YA VIONGOZI
Mheshimiwa Spika, ni
wazi kwamba maadili ya kazi katika Jeshi la Polisi yameporomoka kwa kiwango
kikubwa sana hasa baada ya kuanzishwa kwa siasa ya vyama vingi hapa nchini.
Katika matukio mengi, Jeshi la Polisi limeonekana wazi kabisa kutoshughulikia
uhalifu nchini (na kwa maana hiyo
kutowalinda raia na mali zao) na badala yake kutumia nguvu kubwa kupita kiasi
katika kuzuia mikutano na maandamano halali ya CHADEMA yanayolenga kutoa elimu
ya uraia na kuwafungua watu kifikra na kimtazamo kuhusu ushiriki wao katika
siasa na maendeleo ya nchi yao.
Mheshimiwa Spika, Jeshi
la polisi kwa sasa linaonekana kuacha maadili ya kazi na kujielekeza kukinusuru
Chama cha Mapinduzi kinachoelekea kushindwa badala ya kunusuru heshima yake
ambayo imekuwa ikipotea siku hadi siku mbele ya jamii.
Mheshimiwa Spika,
sasa hivi jeshi la polisi limekuwa likifanya kazi kwa mashinikizo na maelekezo
ya wanasiasa badala ya kuzingatia sheria na taratibu zinazoliongoza.
Mashinikizo hayo yamesababisha watu wasio na hatia kubambikiziwa kesi ili
kutimiza maslahi ya kisiasa ili kukomoa wapinzani wanaopiga kelele kudai haki za
wananchi
Mheshimiwa Spika,
wakati Jeshi la Polisi linawashtaki wabunge wa upinzani kwa makosa ya kutunga, limeshindwa
kuwachukulia hatua wabunge wa CCM waliofanya makosa ya jinai hadharani. Kwa
mfano sheria ya makosa ya jina inakataza mtu kutembea na silaha hadharani kwa
namna itakayotishia watu, lakini Mheshimiwa Ismael Aden Rage alifanya hivyo na
kupigwa picha na vyombo vya habari lakini hakuchukuliwa hatua hadi sasa. Aidha
Mheshimiwa Rage alimshambulia na kumpiga
mwanachama wa CHADEMA hapa Dodoma baada ya kuzuiwa na kijana huyo
kung’oa bendera ya CHADEMA akapigwa picha katika hekaheka za kumpiga kijana
huyo lakini bado yupo ilhali polisi waliona tukio alilolifanya.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani ina taarifa kwamba Jeshi la Polisi limeshakamilisha
uchunguzi wa matukio ya Mheshimiwa Rage lakini wanashindwa kumkamata na
kumpeleka mahakamani kutokana na mashinikizo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma
Dkt. Rehema Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi. Kambi
Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutenda haki sawa kwa wote ili kudumisha
misingi ya utawala wa sheria. Aidha Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali
itoe kauli juu ya hatua inazokusudia kuchukua dhidi ya kiongozi huyu anayefanya
makosa ya jinai hadharani.
- KUWINDWA KWA WAANDISHI
WA HABARI
Mheshimiwa Spika,
waandishi wa babari sasa nao kundi maalum linalolengwa na mashambulizi kutokana
na kazi yao ya kufichua maovu katika jamii na hasa ya viongozi. Kwa mfano,
katika tukio la kuuawa kwa mwandishi
mmoja huko Iringa, taarifa ya MCT ya Oktoba 2012 inasema kwamba: “ wanahabari waliokuwepo kwenye mkutano huo
wanakiri kwamba marehemu alikuwa ndiye mwandishi pekee aliyemuuliza RPC maswali
magumu kiasi cha kumkera kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi”.
Mheshimiwa Spika,
kati ya maswali aliyouliza marehemu ni
“kwa nini chama tawala CCM kiko huru kufanya mikutano ya kisiasa wakati chama
cha CHADEMA kinawekewa vikwazo na polisi kila wakati?” “Aidha
baada ya mkutano huo wa waandishi wakati wanahabari wakitoka kwenye ofisi za
mkoa za polisi, baadhi ya polisi ambao utambuzi wao haukufahamika mara moja
waliwaonya wasiende Nyololo kwa ajili ya kukusanya habari za shughuli za
kisiasa za CHADEMA kutokana na uwezekano wa kutokea kwa hali hatarishi”. Vilevile
kwa mujibu wa taarifa hiyo, “Baada ya
mkutano wa waandishi wa habari wa asubuhi katika ofisi za RPC, waandishi
waliokuwepo wanakumbuka kuwa askari mmoja mpelelezi alimfuata marehemu na
kumwambia: “ Ina maana gani kwenda Nyololo kuandika habari za shughuli za
CHADEMA ambazo zinaweza kuishia na kifo
chako?”
Mheshimiwa Spiaka, Uthibitisho
kwamba, Serikali ya CCM na Jeshi la Polisi wamekuwa wanawalenga waandishi wa
habari kwa makusudi kunathibitishwa na kauli ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa
Makosa ya Jinai aliyoitoa tarehe 05/09/2012. Kwa mujibu wa taarifa ya Pamoja ya
MCT na TEF, DCI Manumba alisema yafuatayo: “….matukio ya aina hii yapo na yataendelea
kuwepo”
Mheshimiwa Spika,
Kauli ya DCI Manumba imerudiwa tena na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magessa Mulongo
tarehe 01/05/2012. “unapoingia katika mkakati wa kumdhalilisha kiongozi wa
Serikali unaiweka roho yako rehani…. Kuweni makini”
Mheshimiwa Spika,
matamshi ya DCI Manumba na Magessa Mulongo ni matendo ya kigaidi kwa mujibu wa
sheria ya ugaidi 2002. Kifungu cha 4(3) a, b na I vinafafanua matendo ya
kigaidi kuwa ni pamoja na vitisho vinavyohusu mtu kusababishiwa maumivu au
majeraha makubwa kimwili, kuhatarisha maisha ya mtu na vinavyohusu usalama wa
umma ambavyo vimelengwa au ambavyo kwa hulka au muktadha wake vinaonekana
vimelengwa kutishia umma au sehemu ya umma.
Mheshimiwa Spika,
Kwa maana hiyo, Kauli ya DCI Manumba kwamba mauaji ya waandishi yamekuwepo na
yataendelea kuwepo na kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kwamba
waandishi wanaofuatilia nyendo za viongozi wa Serikali wanaweka roho zao rehani
ni matendo ya kigaidi. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini DCI
Manumba na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo hawajakamatwa na kufunguliwa
mashtaka ya ugaidi?
- MAMLAKA YA
VITAMBULISHO VYA TAIFA (NIDA)
Mheshimiwa Spika,
Wazo la kuwa na vitambulisho vya utaifa liliibuliwa kwa mara ya kwanza mwaka
1986 katika kikao cha kamati ya intelejesia ya pamoja (Inter – State
Intelligence Committee) ambapo viongozi wakuu wa nchi za Kenya, Uganda, Zambia
na Tanzania waliudhuria. Katika kutekeleza hazimio hilo, Kikao cha Baraza la
Mawaziri Na.3/85 cha mwaka 1985 kiliamua kwamba kuwe na usajili wa raia na
wasio raia.
Mheshimiwa
Spika, azimio hili lilitekelezwa kwa kutungwa kwa sheria ya Kusajili na
Kutambua watu Na.11 ya mwaka 1986. (The Registration and Identification of
Persons Act, No.11/86 1986). Hata hivyo
Serikali haikuwa na uwezo wa kuendelea na shughuli za vitambulisho,kwa sababu
ya gharama za maandalizi na utekelezaji wa program hiyo. Na pia kwa
wakati huo hakukuwa na mpango wa mweleko (road map) na gharama za shughuli hiyo
hazikuwa zinajulikana. Wakati huo wote huo, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM) haikujishughulisha hata kidogo na la Vitambulisho vya Taifa mpaka mwaka
2006 ilipo ingia mkataba wakufanya upembuzi yakinifu.
Mheshimiwa Spika,
Bunge lako tangu wakati huo limekuwa likitenga pesa kwaajili ya utekelezaji wa
shughuli hiyo muhimu, lakini NIDA imekuwa ikitekeleza shughuli hiyo kwa kasi ya
kinyonga na hivyo pesa zinazotengwa haziakisi ufanisi wala mafanikio ya
utekelezaji wa shughuli hiyo. Mathalani tangu wakati huo hakuna raia wa kawaida
aliyepewa kitambulisho ukiondoa watumishi wachache wa umma na watu wengine
wachache. Zoezi la majaribio (pilot study) lililofanyika Dar es Salaam
limeishia hewani na wananchi hawajui hatua gani inafuata.
Mheshiiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inahoji mambo yafuatayo:
- Ni kiasi gani cha
fedha kimeshatumiwa na NIDA tangu mwaka 2006 hadi leo na matumizi hayo
yamekuwa na tija kiasi gani (value for money) kwa kuwa hatuoni maendeleo
mazuri ya utoaji wa vitambulisho vya taifa?
- Ni lini wananchi wote
wa Tanzania watakuwa wamepata vitambulisho vya Taifa?
Mheshimiwa Spika,
Vitambulisho vya Taifa ambavyo waheshimiwa wabunge na watumishi wengine wa umma
wamepewa vina taarifa chache, na havina taarifa nyingi muhumu, mathalani,
hakuna taarifa ya kundi la damu, aina
ya kazi,
anuani ya makazi, tofauti na
vitambulisho vya Mataifa mengine, tofauti na hata ndugu zetu wa Zanzibar ambao
wanavitambulisho vyao vina taarifa zaidi kuhumhusu mwenye kitambulisho.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuweka taarifa zaidi zinazomhusu raia
katika vitambulisho vya taifa.
- KUZAGAA
KWA SILAHA NA MATUKIO YA KIJAMBAZI
Mheshimiwa spika mara
kadhaa kumetokea matukio ya kihalifu katika maeneo mbalimbali hapa nchini na
silaha zinazotumika katika matukio hayo ni silaha nzito za kivita. Hata hivyo
Kambi Rasmi ya Upinzani ilishatoa angalizo mara kadahaa juu ya uwezekano wa
kuzagaa kwa silaha kutokana na wahamiaji haramu na makampuni binafsi ya kigeni
kuajiri walinzi wao wenyewe na kutumia silaha zao wenyewe. Aidha, katika
mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani ilikuwa ni kwamba Serikali ichukue hatua
ya kuimarisha ulinzi zaidi mipakani ili kudhibiti wimbi la wahamiaji haramu
kutoka nchi jirani, kudhibiti wafugaji kutoka nchi jirani wanaoingia nchini
kwetu bila utaratibu kutafuta malisho ya mifugo yao na kuyazuia makampuni ya kigeni kutumia walinzi
na silaha zao wenyewe na baladala yake makampuni hayo yapewe ulinzi na vyombo ya dola vya hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza bunge kwamba imefikia hatua
gani katika kutekeleza mapendekezo ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ili
kuliepusha taifa kukumbwa na matukio ya kijambazi kutokana na kuzagaa kwa
silaha kiholela?
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni pia inaitaka Serikali kuwa makini sana inapotoa
Uraia kwa wakimbizi hapa nchini kwa kuwa kumekuwa na malalamiko kutoka kwa
wananchi kutoka maeneo yenye makambi ya wakimbizi kwamba wakimbizi wamekuwa
wakijihusisha na vitendo vya kihalifu vya uporaji na unyanganyi wa kutumia
silaha. Hivyo uraia utolewe kwa kuzingatia uadilifu, na pia ujuzi au utaalamu
alio nao mtu anayeomba uraia wa Tanzania na sio kutoa uraia kiholela.
Mheshimiwa Spika, kama
nilivyoeleza hapo awali, nchi yetu imekumbwa na tatizo kubwa la kuzagaa kwa
silaha haramu jambo ambalo linatishia amani na utulivu wa nchi yetu kama hatua
za haraka na madhubuti hazitaweza kuchukuliwa mapema na hasa ikizingatiwa kuwa
baadhi ya nchi ambazo tumepakana nazo hali yao ya usalama sio nzuri na
hairidhishi na hasa ikizingatiwa kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa 2012
silaha 889 zilikamatwa na risasi 10,210 zikiingizwa nchini kinyume cha
sheria.
Kambi Rasmi ya Upinzani,
inataka kujua kuna mkakati gani madhubuti wa kukabiliana na wimbi hili la
uingizwaji wa silaha haramu hapa nchini na hasa ikizingatiwa kuwa silaha hizi
zinatumiwa na wahalifu kwa ajili ya kuendesha vitendo vya kihalifu hapa nchini.
- BIASHARA YA DAWA ZA
KULEVYA NCHINI
Mheshimiwa Spika,
Takwimu za jeshi la polisi zinaonyesha kuwa matukio ya kukamatwa kwa dawa za
kulevya hapa nchini ni makubwa sana na kiwango kinachokamatwa kinaongezeka
mwaka hadi mwaka, kwa mfano kwa mwaka 2012 kilo 55,499 za madawa aina ya heroin, cocaine, mandrax na morphine
zilikamatwa ikilinganishwa na kilo 17,776
zilizokamatwa mwaka 2011.Takwimu hizi sio nzuri hata kidogo kwani kiwango hiki
ni kikubwa sana na hasa ikizingatiwa kuwa hizi ni tani 55 na nusu
zilizokamatwa. Bado kuna kiwango kingine ambacho hakikukamatwa, hivyo nchi yetu
ipo kwenye hatari kubwa ya taifa kuangamia kutokana na matumizi ya madawa ya
kulevya.
Kambi Rasmi ya Upinzani,
inaitaka Serikali kutoa maelezo ni kwa nini madawa ya kulevya yanaongezeka
wakati kuna sheria kali za kudhibiti biashara ya madawa ya kulvya?
- WIMBI LA MAUAJI NA
UNYANYASAJI WA RAIA BILA HATUA KUCHUKULIWA
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa ripoti ya Haki za Binadamu Tazania
2012, idadi ya watu waliouwawa Tanzania kinyume na sheria (extra judicial
killings) toka mwaka 2003 hadi 2012 ni 246. Mchanganuo wa mauaji hayo kwa kila
mwaka ni kama ifuatavyo:
2003
|
2004
|
2005
|
2006
|
2007
|
2008
|
2009
|
2010
|
2011
|
2012
|
22
|
7
|
36
|
37
|
26
|
6
|
10
|
52
|
25
|
31
|
Mheshimiwa Spika tukirejea mauaji yenye sura ya kiasiasa
yaliyofanywa na polisi katika mikutano halali ya siasa ya CHADEMA huko Arusaha,
Morogoro na Nyololo – Iringa ambayo Serikali hii ya CCM imeamua kwa dhati
kabisa kuyafumbia macho licha ya tume mbalimbali za uchunguzi kuthibitisha
kuhusika kwa vyombo vya Dola katika mauaji hayo, Kambi Rasmi ya Upinzani
inashawishika kuamini kwamba sasa Serikali hii ya CCM imeamua kusimamia mauaji
ya raia wasio na hatia hapa nchini.
Tuna kila sababu ya kuamini hivyo kwa kuwa hatuoni hatua za makusudi
zikichukuliwa dhidi ya maafisa wa polisi waliofanya mauaji hayo na hasa kwa
aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Michael Kamuhanda ambaye ripoti za
uchunguzi zilithibitisha bila shaka yoyote kwamba alihuika na mauaji ya Nyololo
– Iringa.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa
tamko mbele ya bunge hili kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya aliyekuwa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na maafisa wengine wa
polisi waliohusika na mauaji ya raia wasio na hatia hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kuna kila dalili kwamba Wizara ya Mambo ya
Ndani ya Nchi, chini ya uongozi wa Dkt.Emmanuel Nchimbi, imeshindwa kabisa
kusimamia utendaji kazi wa Jeshi la Polisi na kwa maana hiyo imeshindwa
kusimamia usalama wa raia na mali zao ikiwa ni jukumu lake la msingi. Kambi
Rasmi ya Upinzani imefikia hitimisho hili kwa sababu
hivi
karibuni pia kumetokea mauaji ya kutisha katika mkoa wa Mara hasa katika Wilaya
za Butiama na Musoma Mjini ambapo watu
wengi wanauwawa kinyama kwa kukatwa vichwa na wauwaji kuondoka na vichwa na
viungo vingine vya marehemu huku wakiacha familia zao na wategemezi wao sio tu
na majonzi, bali pia na hofu kuu juu ya mauaji hayo kwani hawajui ni nani atayeuwawa
siku inayofuata. Hii ni kwa sababu mauaji yamekuwa yakiongezeka siku hadi siku,
na bila Serikali na Jeshi lake la Polisi kuonesha umahiri wake wa kuzuia mauaji haya
kama inavyoonesha umahiri huo kwenye
kuzuia mikutano halali ya CHADEMA.
Mheshimiwa Spika, sambamba
na matukio haya ya mauaji ya kutisha, miaka ya hivi karibuni pia kulizuka wimbi
la mauaji ya walemavu wa ngozi hapa nchini na wengine kukatwa viungo vya miili
yao wakiwa hai jambo ambalo lilizua hofu kubwa sana miongoni mwa familia nyingi
zilizokuwa na watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mheshimiwa Spika, jambo
la kutisha zaidi ni kwamba hata askari wetu wenye jukumu la kuwalinda raia na
mali zao, nao pia wanauwawa katika mazingira ya kutatanisha. Itakumbukwa kwamba
huko Zanzibar na Ngara – Kagera kuna polisi waliuwawa na pia hivi karibuni
aliyekuwa Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza naye aliuwawa katika
mazingira ya kutatanisha.
Mheshimiwa Spika,
katika mazingira kama haya ni nani anayeweza kushawishika kwamba Serikali, kwa
maana ya Wizara ya Mambo ya ndani, imefaulu katika kutekeleza majukumu yake?
Mheshimiwa Spika, uhalifu
mwingine unaofanywa dhidi ya binadamu hapa nchini ni ule wa kuchoma nyumba za
wananchi unaofanywa na vyombo vya dola kwa sababu zisizo na uzito kabisa.
Kitendo cha kuchoma nyumba za wakazi wa kijiji cha Mpago katika Kata ya Kaniha
wilayani Biharamulo na Kata ya Rutoro Wilayani Muleba Mkoani Kagera kwa madai kwamba wanakijiji hao wamevamia eneo
la hifadhi ya Taifa na Vitalu vya
vilivyogawiwa kwa mwekezaji na
NARCO kwa mtiririko huo, ni cha kinyama
na ni kinyume kabisa na haki za binadamu. Jambo la kushangaza ni kwamba eneo
hilo linalodaiwa kuwa ni la hifadhi lina miundombinu ya barabara, mashule na
hospitali zilizojengwa na Serikali ikiwa ni ushahidi kwamba ni eneo la makazi.
Baadhi ya familia zilizochomewa nyumba zao zimepotea kusikojulikana na mpaka
sasa haifahamiki kama wamekufa au wapo hai. Katika unyanyasaji unaofanywa
katika Kata ya Rutoro Wilayani Muleba ni kwamba wananchi wanauwawa kwa kupigwa
risasa na watendaji wa vitalu vya mwekezaji ambao ni wanyarwanda na badala ya
wahalifu hawa kushughulikiwa na polisi kinyume chake ni kwamba RCO wa Mkoa wa
Kagera amekula njama na mwekezaji na kuwasaliti wananchi na badala yake
kuwabambikia kesi ya mauaji Diwani wa Kata ya Rutoro, Mtendaji wa kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji Bwana Kahatano.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele ya bugne hili
kama imeruhusu wawekezaji kuwauwa wananchi kwa kuwapiga risasi. Pili Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni kwa viongozi wanaowatetea wananchi
wanabambikiwa kesi za mauaji kwa ili kumlinda mwekezaji?
- AJALI
ZA BARABARANI NA RUSHWA KWA ASKARI WA USALAMA BARABARANI
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu 2012, ajali za barabarani zinashika
nafasi ya pili nchini kwa kusabisha vifo baada ya Malaria. Sababu zilizotajwa
na ripoti hiyo kusababisha ajali ni rushwa iliyotawala kwa askari polisi wa
barabarani ambao mda mwingi wanajishughulisha zaidi kuomba rushwa kwa madereva
huku ajali zikiendelea kutokea. Aidha uendeshaji wa hovyo wa madereva na
mwendokasi vimetajwa na ripoti hiyo kama visababishi vya ajali.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa majibu mbele ya bunge
hili askari wa Usalama barabarani wanasaidiaje kupunguza ajli za barabarani?
- UTEKELEZAJI WA BAJETI
YA MWAKA 2012/2013
18.1.
Jeshi
la Polisi.
Mheshimiwa Spika ,
mnamo mwaka 2012/2013 jeshi la polisi
lilitengewa jumla ya shilingi bilioni
335.605 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na fedha za Maendeleo , mpaka
mwezi February 2013 jumla ya shilingi bilioni
232.750 tu ndio zilikuwa zimetolewa
ikiwa ni sawa na asilimia 69.3 ya
fedha zilizokuwa zimetengwa. Aidha hakukuwa na kiasi chochote cha fedha
kilichokuwa kimetolewa na hazina kwa ajili ya miradi ya Maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
pamoja na fedha kutokutolewa kwa wakati , lipo tatizo kubwa la baadhi ya
vikosi, mikoa na Wilaya kutokupata fedha kwa wakati ama chini ya kiwango
kilichoidhinishwa na Bunge kama ifuatavyo, fungu 28 ,kifungu 2002 polisi Marine
waliidhinishiwa shilingi milioni 767.2
ila mpaka Februari walikuwa wamepokea kiasi cha shilingi milioni 147.438 tu, kifungu 2006 polisi Anga “Airwing”
waliidhinishiwa shilingi bilioni 1.777
ila mpaka Februari, 2013 walikuwa wamepokea kiasi cha shilingi milioni 95.364 tu, kifungu 2008 FFU
waliidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni
818.030 ila mpaka Februari 2013 walikuwa wamepokea kiasi cha shilingi milioni 147.365 tu, kifungu 2009 polisi
wa usalama barabarani waliidhinishiwa kiasi cha shilingi milioni 161.455 na mpaka februari 2013 walikuwa wamepokea kiasi cha
shilingi milioni 78.354 tu.
Mheshimiwa Spika, kifungu 2012
kanda maalum ya DSM iliidhinishiwa shilingi bilioni 1.012 mpaka mwezi Februari
ilikuwa imepokea kiasi cha shilingi milioni
153.425 tu, pamoja na mwenendo huu wa jeshi la polisi kutokupewa fedha kwa
wakati hali ni ya tofauti sana ukienda kwenye kitengo cha Upelelezi (CID)kifungu
7001, ambacho walikuwa wameidhinishiwa shilingi bilioni 6.191 ila mpaka mwezi Februari 2013 walikuwa wametumia
kiasi cha shilingi bilioni 12.359
yaani nyongeza ya zaidi ya asilimia 100 ya kiwango kilichokuwa kimeidhinishwa
na Bunge .
Mheshimiwa Spika, pamoja
na kitengo hicho kutumia fedha nyingi kiasi hicho lakini randama ya wizara
inaonyesha kuwa upelelezi wa makosa makubwa ya jinai 72,765 ulifanyika na ni kesi 32,775
tu ndio zilifikishwa mahakamani na washitakiwa waliokutwa na hatia ni asilimia 11.6 tu ya kesi zote
zilizofikishwa mahakamani, Pia ni askari
511 tu ndio waliweza kupata mafunzo
ya Intelijensia na Upelelezi kwa mwaka huo wa fedha.
Kambi
Rasmi ya Upinzani , inataka kupata majibu kuhusiana na masuala yafuatayo;
i.
Ni kwanini fedha kwa ajili ya matumizi
kwenye vikosi vya polisi mwenendo wake umekuwa ni wa kusuasua sana kwenye mwaka
wa fedha uliopita, hasa kwenye mikoa na Wilaya nchini,
ii.
Je? Kiasi cha bakaa iliyokuwa bado
haijatolewa kitaweza kutolewa ifikapo mwishoni mwa mwaka huu wa fedha ?
iii.
Je? Ni kwanini mpaka mwezi Februari hapakuwa
na fedha yoyote iliyokuwa imetolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo
ilipaswa kufanywa na jeshi la polisi?
iv.
Ni kwanini kitengo cha upelelezi (CID)
kilitumia zaidi ya kiasi cha fedha ambacho kilikuwa kimeidhinishwa na Bunge,
wakati kiwango cha makosa yaliyoweza kupelelezwa na uwiano wa washitakiwa
kutiwa nguvuni mahakamani haviendani au ndio kusema hapakuwa na ushahidi
kutokana na watu kubambikiwa kesi?
18.2.
Jeshi
la Magereza
Mheshimiwa Spika,
mwaka wa fedha 2012/2013 fungu 29 jeshi hili lilitengewa jumla ya shilingi bilioni
114.358 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na kiasi cha shilingi bilioni 1.555 kwa ajili ya
Miradi ya Maendeleo .Hadi mwezi Februari 2013 fedha iliyokuwa imetolewa kwa
ajili ya matumizi ya kawaida ilikuwa ni kiasi cha shilingi bilioni 76.517 na fedha kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo ilikuwa
kiasi cha shilingi milioni 327.000
tu
Mheshimiwa Spika,kutokana
na mwenendo huu wa fedha ni dhahiri kuwa Jeshi la magereza limeshindwa kupata
fedha kwa ajili ya kuboresha magereza yetu,
na hata kukarabati nyumba ,ofisi na makazi ya askari magereza kote nchi
na hivyo kuendelea kufanya maisha ya mahabusu,wafungwa na askari magereza
kuendelea kuwa mabaya na wakiendelea kupata mateso kutokana na kukosekana na
Miundombinu dhabiti kwenye Magereza yetu.
Mheshimiwa Spika, kambi
ya upinzani inasikitishwa sana na hali hii ya Magereza kutokutengewa fedha na
hata zikitengwa huwa hawapewi kwa wakati na sasa jeshi hili limegeuka na kuwa
mdaiwa sugu ,kwani mpaka Februari 2013 jumla ya madeni yote walikuwa wanadaiwa
kiasi cha shilingi Bilioni 35.330 ,
na kiasi hicho kilikuwa kimegawanyika kama ifuatavyo , Bilioni 12.547 ni madeni ya askari Magereza,Bilioni 18.838 ni madeni ya wazabuni waliotoa huduma mbalimbali kwa
ajili ya wafungwa magerezani na shilingi Bilioni
3.994 ni madeni kwa ajili ya umeme na maji.
Mheshimiwa Spika, kutokana
na mwenendo huu wa fedha kidogo kutengwa kwa ajili ya magereza imepelekea kuwa
na msongamano mkubwa sana kwenye Magereza yetu hapa nchini na kwa sasa uwezo wa
magereza yetu ni kuwa na wafungwa 29,552
ila mpaka tarehe 01.02.2013 walikuwepo wafungwa 34,355 ,hali hii Kambi rasmi ya upinzani haikubaliani nayo kwani ni
kinyume na haki za Binadamu na kamwe hatutakuwa tayari kubariki vitendo vya
uvunjaji wa haki za Binadamu wa aina yeyote.
18.3.
Jeshi
la Zimamoto na Uokoaji
Mheshimiwa Spika,
jeshi la zimamoto na uokoaji lipo katika fungu 14 na katika mwaka wa fedha
2012/2013 zilitengwa jumla ya shilingi bilioni
16.967 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na hazikutengwa fedha zozote kwa
ajili ya Miradi ya Maendeleo zilizokuwa zimetengwa kwa mwaka huo wa fedha
.Aidha hadi mwezi februari 2013, ni asilimia 40 tu ya fedha ambazo zilikuwa
zimetengwa ndio zilikuwa zimetolewa na Hazina .
Mheshimiwa Spika,
kutokana na serikali kutotoa fedha zilizoidhinishwa na Bunge kwa wakati kwa
ajili ya Jeshi la zimamoto na uokoaji
kumesababisha madhara mbalimbali kama vile kushindwa kununua vitendea
kazi mbalimbali kama vile madawa ya kuzima moto, magari ya zimamoto,kutoa
mafunzo kwa ajili ya askari wa Zimamoto na kushindwa kujenga vituo vipya vya
Zimamoto.
Aidha,
kutokana na hali hiyo Jeshi hili limeshindwa kukabiliana na majanga ya moto
yanayotokea hapa nchini kama vile kushindwa kuzima moto kwenye maeneo
mbalimbali,kushindwa kukabiliana na maafa kama kuporomoka kwa ghorofa DSM
,kutokana na kukosekana kwa vifaa vya kisasa kwa ajili ya kufanyia kazi hiyo.
Kambi Rasmi ya Upinzani,
inaitaka serikali kuhakikisha kuwa jeshi hili sasa linapewa kipaumbele ili
liweze kukabiliana na maafa mbalimbali ya moto yanayotokea hapa nchini na
kuweza kuokoa mali za wananchi ambazo zimekuwa zikiteketea.
- UCHAMBUZI WA BAJETI YA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI 2013/2014
19.1.
Miradi
ya Maendeleo Mwaka 2013/2014
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa randama iliyowasilishwa na wizara ,fungu 28 limetengewa jumla ya shilingi 8,980,451,000
kwa ajili ya miradi ya Maendeleo , na katika mgawo huo ni kuwa kiasi cha
shilingi bilioni 5 ndio fedha za
ndani na zilizosalia ni utegemezi kutoka kwa wahisani/wafadhili.
Mheshimiwa Spika,
jambo la kusikitisha ni kuwa pamoja na matatizo lukuki yanayolikumba jeshi la
polisi bado serikali haijaona haja ya kuongeza fedha za kutosha kwa ajili ya
miradi ya maendeleo ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazolikumba jeshi la
polisi.
Kwa
mfano, hakuna fedha zilizotengwa kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kuimarisha
doria baharini (kifungu 6108), hakuna
fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya polisi (rehabilitation of police
building, kifungu 6303), na fedha
iliyotengwa kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi ya askari wetu ni shilingi
bilioni 2 tu (kifungu 6302),
vilevile hakuna fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya mawasiliano kama magari
kwa ajili ya kuhakikisha kuwa doria inaimarishwa.
Kambi Rasmi ya Upinzani,
haikubaliani na mgawanyo huu wa fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo na
tunaitaka serikali kutenga fedha kwa ajili ya makazi ya polisi, ukarabati wa
vituo na sero za polisi pamoja na fedha kwa ajili ya fulana za kuzuia risasi
ili kuwalinda askari wetu pindi wanapokuwa wakipambana na wahalifu .Serikali
imewaahidi sana polisi kuhusu makazi bora sasa sio muda wa ahadi tena ila uwe
muda wa kutekeleza ahadi hizo kwa vitendo.
- HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, ni
haki ya kikatiba ya kila raia wa Tanzania
kulindwa yeye na mali yake na kuishi kwa uhuru na amani katika nchi
yetu. Kwa kuwa watu ndio msingi wa taifa lolote lile duniani, wajibu wa kwanza
kabisa wa Serikali yoyote ni kuwalinda watu na mali zao. Wananchi huuza uhuru wao kwa kuipa Serikali
mamlaka na madaraka yote kumiliki vyombo vyote vya Dola ili iwalipe wananchi
ulinzi na usalama. Kwa hiyo kama Serikali imepewa mamlaka yote na wananchi na
inashindwa kutimiza jukumu lake la msingi la kuwalinda wananchi na mali zao,
kwa vyovyote vile Serikali ya namna hiyo haina uhalali wa kuendelea kutawala.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ijitazame upya na kuona kama ina
uhalali wa kuendelea kutawala ilhali kuna matukio makubwa ya kigaidi na
kijambazi yanayofanywa dhidi ya raia wasio na hati bila hatua madhubuti za
kukomesha uhalifu huo kuchukuliwa.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inasikitishwa kuona Serikali ikiwadhulumu wananchi kwa
kuendelea kukaa kimya juu ya mambo mengi yasiofaa yanayoendelea kutokea katika
nchi hii. Hivyo Kambi Rasmi ya Upinzani inatoa wito kwa wananchi wote kupima
utendaji wa Serikali hii ya CCM na kama hawaridhishwi na utendaji wa Serikali
basi wachukue hatua kwa kuchagua Serikali mbadala itakayoongozwa na CHADEMA
ifikapo 2015.
Mheshimiwa Spika, pamoja
na mazoea ya Serikali kubeza hoja za Kambi Rasmi ya Upinzani lakini ukweli
unabaki palepale na pia wito kwa wananchi wote waendelee kutuunga mkono kwa
kuwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inayoongozwa na CHADEMA imedhamiria na
imejipanga vizuri kutwaa madaraka ya Dola ifikapo 2015.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, naomba
kuwasilisha.
____________________________________________
Vincent
Josephat Nyerere (Mb) – Musoma Mjini
MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI
BUNGENI
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
6 Mei, 2013
No comments:
Post a Comment