Thursday, May 30, 2013

Slaa: Simchukii JK

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema hamchukii Rais Jakaya Kikwete kwa sababu ya dini yake bali kwa udhaifu wa serikali anayoiongoza.
Alisema udhaifu wa serikali anayoiongoza ndio umechangia maisha ya Watanzania yaendelee kuwa magumu licha ya Tanzania kubarikiwa rasilimali nyingi.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo jana Mbagala jijini Dar es Salaam, katika mkutano wa hadhara wa kumnadi Cusbert Gwata, anayewania udiwani wa Kata ya Mianzini.
“Sina chuki na Rais Kikwete kama baadhi ya waeneza propaganda chafu wanavyofanya…watu wengine wanajaribu kupindisha kuwa namchukia kwa sababu ya dini yake, suala hapa si dini, suala ni kwamba yeye kama rais hana uwezo wa kuongoza.
“Anashindwa kusimamia na kutawala, kama mtu hana uwezo hakuna neno jingine wala mbadala wa kusema hayo…ni dhaifu tu,” alisema Dk. Slaa.
Alisema serikali ya CCM imekuwa ikijitahidi kutengeneza propaganda mbalimbali ikiwamo tofauti za kidini baina ya viongozi na makada wa upinzani dhidi ya watawala.
Alibainisha kuwa lengo la propaganda hizo ni kuficha udhaifu wao na kuwasahaulisha Watanzania wanaoteseka na mgawanyo wa rasilimali unaofanywa na serikali iliyopo madarakani.
Alisema hatamung’unya maneno wala kusita kuukosoa udhaifu wa serikali iliyopo madarakani kwakuwa akinyamaza ataifanya iendelee kuwatesa na kuwanyonya wananchi.
Alisema Watanzania wanapaswa kukumbuka mifano hai ya watu waliofanya kazi zao bila kuhusishwa na tofauti za dini walizonazo kuwa ni Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi.
Dk. Slaa alisema kama angekuwa anawakosoa watu kwa sababu ya dini zao, basi asingemtaja Rais mstaafu Benjamin Mkapa pamoja na Waziri Mkuu wake, Frederick Sumaye, katika orodha ya mafisadi.

Bonyeza Read More Kuendelea



Aliongeza kuwa licha ya kumtaja Rais Mkapa katika orodha ya mafisadi 11 katika viwanja vya Mwembeyanga, pia alimbana kwa kuigeuza Ikulu kuwa pango la kufanyia biashara.
“Sumaye ni Mkristo na ni wa kabila langu, lakini nilimtaja kwenye orodha hiyo, hakusalimika katika kukemewa kwa vile ni dini au kabila langu,” aliongeza.
Katika mkutano huo Dk. Slaa alisema alipokuwa Katibu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) alifanya kazi kwa ukaribu na aliyekuwa Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Hemed Jumaa bin Hemed chini ya utawala wa Mwinyi.
Alisema ushirikiano huo ulikuwa imara sana kwani kila aliyepokea matatizo kuhusiana na dini walikaa chini kuyazungumzia na hatimaye kuyatafutia ufumbuzi.
Akizungumzia vurugu za Mtwara, Dk. Slaa alisema mwanzo walipoitahadharisha serikali iwasikilize wananchi hawakubahatisha bali walishajua madhara ya wananchi kutoshirikishwa kwenye rasilimali zilizopo katika radhi yao.
Alisema kama serikali ingekaa na wananchi mapema na kuwasikiliza na kisha kuwaelewesha wangeepusha madhara yaliyojitokeza, ikiwamo kupotea kwa maisha ya watu.
“Serikali inapaswa itambue kuwa masuala ya rasilimali hayamalizwi kwa kupeleka Jeshi la Wananachi au polisi kwa wananchi na kuwapiga mabomu, bali kwa kuwashirikisha wananchi kwa ukamilifu,” aliongeza Dk. Slaa.
Aliongeza kuwa sababu ya kumnadi mgombea udiwani wa Kata ya Mianzini ni pamoja na CHADEMA kubeba dhamana ya diwani huyo na kwamba kama watampa nafasi ya kuwahudumia na asitende haki chama kitamuwajibisha.
Aliwataka wakazi wa Mianzini kuhakikisha hawafanyi makosa ya kukichagua Chama Cha Mapinduzi katika uchaguzi huo wa marudio, huku akielezea kuwa mikoani wanasikitishwa na namna Jiji la Dar es Salaam linavyochelewesha mageuzi kwa kukikumbatia chama kilichopo madarakani.

No comments:

Post a Comment