Thursday, May 30, 2013

Katibu CHADEMA adakwa kwa ugaidi

KAIMU Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Mtwara, Felician Melikisedeki, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa muda wa siku 10 bila kufikishwa mahakamani.
Melikisedeki inadaiwa anaandaliwa mashitaka ya kutaka kufanya ugaidi huku akizuiwa kuonana na watu walio karibu naye akiwemo mwanasheria wake.
Kada huyo amepokonywa simu yake ya kiganjani na polisi wanaodai imetumika kupiga picha nyumba ya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi na serikali waliojenga mkoani Mtwara.
Taarifa kutoka mkoani Mtwara zinaeleza kuwa Melikisedeki, alikamatwa Mei 17 mwaka huu, siku iliyodhaniwa ingesomwa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Vyanzo vyetu ndani ya Jeshi la Polisi mkoani humo vimeiambia Tanzania Daima, kabla ya kukamatwa kwa Melikisedeki, lilikuwa likimfuatilia kwa hofu ya kuwashawishi wananchi mkoani humo kutenga muda wa kusikiliza bajeti ya wizara hiyo.
“Siku ile makachero wawili walikuwa wanamfuatilia na Melikisedeki akiwa katika moja ya grosari alipigiwa simu akasogea pembeni kwenda kusikiliza, kwa kuwa pale kulikuwa na kelele nyingi mmoja wa wale askari akamfuata lakini hakumuona,” kilisema chanzo chetu.

Bonyeza Read more Kuendelea



Inaelezwa kuwa baada ya mmoja wa makachero waliokuwa wakimfuatilia kutokumuona alianza kuhangaika kwa kumtafuta, hatua iliyomfanya askari huyo kuchungulia katika moja ya dirisha la nyumba na kukutana na watoto walioanza kupiga kelele kwa hofu.
Aliongeza kuwa kelele za watoto hao zilimshitua mama yao aliyetoka na kumuona askari huyo akikimbilia katika grosari iliyo jirani na nyumba yao.
Kutokana na hali hiyo, mama mwenye nyumba na wanawe walimfuata askari huyo kwa ajili ya kutaka kujua sababu za kuchungulia katika nyumba yao ndipo mzozo ulipozuka.
“Kumbe yule aliyekuwa akiongea na Melikisedeki pale grosari kabla hajapigiwa simu ndiyo mwenye nyumba ambayo askari alichungulia na kupigiwa kelele sasa aliporejea na familia ya yule bwana ilikuwa nyuma yake ndipo wakaanza kumhoji sababu ya kwenda kuchungulia,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo chetu kingine kimesema katika mabishano hayo ndipo Melikisedeki aliporejea kuungana na baba mwenye nyumba kuhoji sababu ya mtu huyo kuchungulia katika nyumba za watu, hali iliyowafanya makachero hao wajitambulishe kuwa wako kazini na kuwapigia wenzao simu kisha kuondoka na katibu huyo.
Kiliongeza kuwa baada ya kuchukuliwa kwa katibu huyo alikaa kwa muda wa siku mbili huku ndugu zake wakikataliwa kupeleka chakula au kuwasiliana naye kwa namna yoyote.
“Tunasikia kuwa wanataka kumfungulia kesi ya ugaidi kwa madai ya kuwa amepiga picha nyumba ya Waziri George Mkuchika na Hawa Ghasia tena wanasema alitumia simu ya mkononi ambayo Jeshi la Polisi ilichukua na kukaa nayo zaidi ya siku tano bila mtu yeyote kushirikishwa,” alisema mmoja wa ndugu wa katibu huyo kwa njia ya simu.
Kufuatia taarifa hizo, gazeti hili lilimtafuta Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa, kwa muda wa siku tatu mfululizo na alipopatikana alisema yupo kwenye kikao apigiwe baadaye.
Kamanda huyo alipopigiwa simu baadaye alitaka atumiwe ujumbe, alipotumiwa ujumbe hakuujibu na alipopigiwa simu alijibu yupo kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Jitihada za Tanzania Daima, kupata ufafanuzi wa polisi zilizidi kugonga mwamba kwani kamanda huyo kila mara alikuwa akidai yupo katika mikutano.

No comments:

Post a Comment