Sunday, May 26, 2013

Mnyika alitwisha Bunge lawama

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA) amesema nchi imefikia hali hii kutokana na udhaifu wa Bunge kushindwa kuisimamia serikali.
Alisema kuwa kitendo cha Bunge la tisa chini ya Spika Samuel Sitta na kisha la kumi chini ya Anne Makinda kushindwa kuisimamia serikali itekeleze maazimio ya Bunge kuhusu sakata la kampuni hewa ya kufua umeme ya Richmond na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo kumeisaidia serikali kuendelea kufanya mambo kwa staili ya zimamoto.
Katika taarifa ya kambi ya upinzani aliyoiwasilisha bungeni wiki hii, Mnyika alisema kuwa vurugu za Mtwara zimeisaidia serikali kupata kisingizio cha kutotimiza wajibu wake.
“Hii wizara kila mwaka wakati wa bajeti inakuwa na matukio ambayo yanafunika mjadala kwa wabunge kushindwa kuisimamia serikali na badala yake wanajikita kwenye tukio.
“Wakati wa bajeti mwaka jana, iliibuliwa kashfa ya aliyekuwa Mkurugenzi wa TANESCO, William Mhando, wabunge wote wakahama kwenye mjadala wa kuibana serikali ieleze utekelezaji wa maazimio ya Bunge badala yake tukajadili Mhando na TANESCO,” alisema.
Mnyika aliongeza kuwa hata hili la vurugu za Mtwara litafifishwa kwa kuwapiga wananchi mabomu ili bajeti ipitishwe kwa haraka kusudi wabunge wasijikite kufichua udhaifu na ufisadi unaotaka kufanywa kwenye mikataba ya gesi asilia.
“Katika sekta za nishati na madini, kama ilivyo katika sekta nyingi nchini; tumefika hapa tulipo kwa sababu ya udhaifu wa serikali inayoongozwa na Rais Kikwete, uzembe wa Bunge na ulegelege wa CCM,” alisema.
Aliongeza kuwa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata la Jairo, baadhi ya mapendekezo yake yalipitishwa kuwa maazimio, ikiwa ni pamoja na kuitaka serikali ichukue hatua za kinidhamu kwa katibu huyo kwa matumizi mabaya ya madaraka, kukusanya na kutumia fedha za serikali kinyume cha sheria.

Bonyeza Read More Kuendelea



Mnyika ameitaka serikali kulieleza Bunge hatua za utekelezaji wa maazimio hayo ya Bunge, kwani baadhi ya wahusika bado wapo maofisini wakiendelea na kazi na wengine wakiendelea kuteuliwa kushika nafasi zingine katika uongozi na utumishi wa umma kama vile hakuna lililowahi kutokea.
“Itakumbukwa kwamba taarifa mbili za serikali kuhusu utekelezwaji wa maazimio ya kamati teule kuhusu Richmond ziliwasilishwa bungeni na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Agosti 28, 2008 na Februari 11, 2009.
“Taarifa moja ilikabidhiwa na kujadiliwa na kamati, ambazo zililitaarifu Bunge kuwa utekelezaji wa maazimio 10 kati ya 23 yaliyotolewa na Bunge, yalifanyiwa kazi hadi Februari 2009 na maazimio 13 bado yalikuwa hayajakamilika,” alisema.
Alifafanua kuwa Bunge liliazimia kwamba taarifa za utekelezaji wa maazimio yaliyobaki ziwasilishwe kwa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama ambayo hata hivyo hadi inagawanywa, haikuwasilisha taarifa yoyote bungeni ya kueleza kukamilika kwa utekelezaji wa maazimio husika.
“Katika hali inayozua maswali kuhusu umakini wa Bunge katika kusimamia maazimio yake mwaka 2011, Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu na kujiuzulu kufuatia kashfa ya Richmond, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama.
“Kamati hiyo ndiyo iliyopewa dhamana na Bunge kufuatilia utekelezaji wa maazimio kuhusu mkataba kati ya TANESCO na Richmond. Katika hali hiyo, haishangazi kwamba kwa miaka miwili toka wakati huo, mpaka mabadiliko ya kamati za Bunge yalipofanyika kamati hiyo katika taarifa zake zote bungeni haijawahi kuisimamia serikali kuhakikisha maazimio husika ya Bunge yanatekelezwa,” alisema.
Alisema serikali ieleze kwanini hadi sasa haijatekeleza maazimio hayo na Bunge liweke muda wa ukomo wa kutekeleza maazimio yote ya Bunge yaliyokuwa yamesalia katika sakata hilo la Richmond ili mara moja na daima sakata hilo limalizwe.

No comments:

Post a Comment