Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Rebecca Mngodo, amesema ameshangaa kuona hotuba yote ya bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kutozungumzia kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa waandishi wa habari ingawa wako chini ya wizara hiyo.
Amesema ingawa baadhi ya wabunge wamezungumzia kutekwa na kuteswa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Absalom Kibanda, na kuuawa kwa mwandishi wa Channel 10, Daud Mwangosi, wapo waandishi wengi wanaoteswa na kutishiwa wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
Aidha, mbunge huyo alisema serikali kwenye bajeti hiyo haijasema ilitumia kifungu gani kulifungia gazeti la MwanaHalisi bila kikomo na kwamba, huo ni ukandamizaji wa vyombo vya habari na namna ya kuwalinda waandishi wa habari wanaofanya kazi katika mazingira magumu.
Alisema ingawa haki ya kupata habari imeainishwa kwenye Ibara ya 18 ya Katiba, viongozi wengi serikalini na kwenye taasisi mbalimbali, wamekuwa wakiwakwamisha waandishi wa habari kupata taarifa.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Mikidadi, aliwapa pole waandishi wa habari waliopatwa na mikasa ya kutekwa na kuteswa na wengine waliouawa wakitekeleza majukumu yao.
Alimpa pole Kibanda, ambaye alitekwa na akuteswa vibaya nje ya nyumba yake na watu, ambao hawajajulikana hadi sasa.
Mbunge wa Nzega (CCM), Dk. Hamis Kigwangalah, alisema hakuna haki wala uhuru usio na mipaka na kwamba, lazima viwekewe mipaka.
Alisema katika baadhi ya vyombo vya habari, uhuru hautumiki vizuri na watu wamekuwa wakiandika na kusema mambo yanayokashifu na kuudhi wengine.
“Mambo yanaandikwa kwa lengo la kutugawa kikabila, kidini na kikanda, huu si uhuru
unaozungumziwa katika mikataba mbalimbali ya haki za binadamu, mambo hayo hayaruhusiwi na Katiba yetu, naomba wizara itakapoleta Sheria ya uhuru wa habari muweke mipaka,” alisema Dk. Kigwangalah.
No comments:
Post a Comment