Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amelalamikia kitendo cha wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliokuwa wamepangwa kuchangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka 2013/14, kutofanya hivyo na hivyo, kusababisha muda pamoja na mamilioni ya shilingi za kuendesha shughuli za Bunge kupotea.
Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai (Chadema), alisema hayo alipoomba Mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya Bunge ya 68 (7).
Alisema Bunge ni chombo cha wananchi, hivyo ni wa wajibu wa wabunge wa pande zote kutumia muda kufanya mambo ya msingi.
“Katika orodha ya kazi za leo, ilipanga wabunge 18 wachangie hotuba ya waziri, lakini wabunge kutoka CCM wengi hawakuchangia, bali wanne na muda wa Bunge umepotezwa bila sababu za msingi,” alisema Mbowe na kuongeza:
“Tunapoteza fedha nyingi na tunapoteza saa nzima. Kwanini nafasi hizi zinapotezwa na wenzetu, hawapewi wabunge wengine wa upinzani kuchangia?”
Kabla ya Mwenyekiti wa Bunge, Jenister Mhagama, kutoa mwongozo huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisimama na kuomba kutoa taarifa.
Lukuvi alisema wakati wanapopitisha taratibu za kanuni za Bunge, majina yanaorodheshwa kutokana na wachangiaji wenyewe, hivyo, akasema mbunge mwenyewe ana uwezo wa kuchagua hotuba ya wizara ya kuchangia.
Kutokana na hilo, alisema wabunge wa CCM, ambao hawakufika jana bungeni kuchangia, waliorodhesha chaguo lao kwa hotuba ya pili na ya tatu au nyingine, ambazo alisema watazitoa kwenye wizara nyingine.
“Wote, ambao hawakuchangia leo (jana) hawakutaka kuwa chaguo lao. Na mimi ndiye ningelalalamika. Hawakujitokeza si kwa bahati mbaya, bali walichagua hotuba za umuhimu wa kwanza,” alisema Lukuvi.
Naye Mhagama akitoa mwongozo wake, alisema kwa mujibu wa kanuni, utaratibu wa uchangiaji unakwenda kwa uwiano wa vyama, mgawanyo wa dakika za uchangiaji ndani ya Bunge kwa kuzingatia uwiano wa vyama.
Alisema taarifa za wabunge watano wa CCM waliziacha dakika zao zitumiwe na mawaziri wa serikali kujibu hoja za wabunge.
“Huo ni mgawanyo, ambao tulikubaliana kwenye kikao,” alisema Mhagama na kuongeza kuwa dakika zilizotumiwa jana na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, kujibu hoja za wabunge zilipunguzwa.
Alisema walikubaliana hivyo kwenye kikao kwamba, mawaziri wakitaka kusema watumie dakika za mbunge fulani wa CCM, hivyo, akasema hajaona kama wamepoteza muda.
No comments:
Post a Comment