Friday, May 3, 2013

Lema: Nimeaga familia yangu



MBUNGE wa Arusha Mjini Godbless Lema, amesema tangu alipoamua kupigania haki za wananchi alikwisha itaarifu familia yake kuwa iwe tayari kupokea mwili wake akiwa amekufa.
Lema alisema maneno hayo jana jioni katika viwanja vya shule ya Msingi Ngarenaro, wakati akihutubia maelfu ya wakazi wa Arusha katika kile alichoita kutoa ufafanuzi wa tukio la yeye kuhusishwa na vurugu zilizotokea katika Chuo cha Uhasibu wiki iliyopita."

Familia yangu, inafahamu na nilishaiarifu, kwa sababu napigania haki za wananchi, wawe tayari kupokea maiti yangu na si mgonjwa mwenye majereha," alisema.

Mbunge huyo, alitumia muda mwingi kumshambulia kwa maneno makali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo kama ndiye tatizo kubwa la demokrasia mkoani hapa.

"Mulongo akishirikiana na polisi, walijaribu kutengeneza kesi ya mauaji ya yule kijana ti mimi nilihusika,lakini kwa sababu nilishaandaa mikanda ya video nakuisambaza wakashindwa,

"Nilishajua nia yao,ndio maana nikatengeneza ile video na kuisambaza kama sivyo wangenipa kesi ya mauaji,nasema huu ni mpango wa Serikali kutaka kumpiga mchungaji wa kondoo ili kondoo watawanyike"

Aliishutumu vikali ofisi ya Bunge kwa kushindwa kukemea utaratibu uliotumiwa na polisi kumkamata.

"Nimedhalilishwa na kudhalilishwa kwangu ni ninyi mmedhalilishwa,kutukanwa mimi ni ninyi mmetukanwa,hawakuja na kibali cha Spika, wamekuja kama wanavamia nyumba ya mhalifu"

Lema alitumia mkutano huo, kuitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza uchaguzi katika kata ya Sombetini, ili kuwapa fursa wananchi kupata kiongozi wao.

"CCM kupitia tume iache uhuni huu kwa hofu kuwa tukishinda tutaunda halmashauri ya jiji kwa kumtoa meya aliyepo,nawaambia hatutakubali,ama tutafia barabarani au tutazuia mahakamani,hii haikubaliki"

"Sheria inasema diwani asipohudhuria vikao vitatu sio diwani tena (Alphonce Mawazo), aliyekuwa diwani Sombetini kupitia CCM, alijiunga nasi tangu mwaka jana ,hawa watu hawako makini hata kidogo"

Katika hatua nyingine, aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuia ya Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha ambaye sasa ni kada maarufu wa Chadema, James Millya amemfungulia mlango wa kutokea mbunge wa Simanjiro, Christofa Sendeka (CCM).

Millya alidai mwaka 2015, Simanjiro itakuwa jimbo la Chadema na Mungu akimweka hai na akipitishwa na chama chake njia ni nyeupe kwake.

"Simanjiro ni yetu,namtaarifu kuwa 2015 tutashinda kwa kishindo na si hapo tu lengo letu la msingi ni kuchukua dola" alisema Millya.

No comments:

Post a Comment