Wednesday, May 29, 2013

CHADEMA walalamikia rafu Makuyuni

KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, amelionya Jeshi la Polisi wilayani Monduli kutoendelea kutumika kukihujumu chama hicho katika uchaguzi wa udiwani Kata ya Makuyuni kama linavyofanya sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Golugwa alisema Jeshi la Polisi Monduli sasa linatumika kukamata vijana wote wanaodhaniwa wanakiunga mkono chama hicho kwa shinikizo la wanasiasa wakongwe nchini.
“Kuna vijana wamekamatwa Makuyuni tangu tulipozindua kampeni za uchaguzi za chama chetu baada ya kuonekana wakipeperusha bendera za chama… tuna ushahidi kuwa ni maagizo kutoka kwa mmoja wa vigogo wa CCM Monduli,’’ alisema Golugwa.
Aliliomba Jeshi la Polisi kutojitumbukiza katika kampeni chafu, kwani CHADEMA ina uwezo wa kujilinda na kupambana na hali zote.
Alifafanua kuwa wao kama chama tayari wanaanza kujipanga kupitia vijana wa chama hicho mkoani ‘Red Brigade’ kwa ajili ya kwenda kuwalinda viongozi Monduli na kupambana na wote watakaojaribu kuharibu kampeni za chama hicho.
Baada ya mkutano huo, katibu huyo aligawa pikipiki saba zenye nembo ya chama hicho kwa wilaya za Monduli na Arusha Mjini kwa ajili ya kusaidia shughuli mbalimbali za chama.
Naye mgombea udiwani wa Makuyuni, Japhet Sironga, alisema baada ya kuonekana anaungwa mkono na wananchi sasa kumeanza kampeni chafu za ukabila Monduli na yeye japo ni Mmasai wa asili akibatizwa kabila ambalo si lake.
“Hali ya Monduli inabadilika kila kukicha sasa wananchi wanatishwa na kampeni za ukabila zinaendeshwa na kuhatarisha umoja wa wakazi wa Makuyuni, kuna watu wametishwa wasipotoa kura kwa CCM watalaaniwa,” alisema Sironga.

No comments:

Post a Comment