Wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana jioni walilitikisa Bunge walipochangia hotuba ya makadirio ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Kauli nzito zilimlazimisha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, kusimama kueleza masikitiko yake kuhusiana na maneno waliyoyatumia dhidi ya serikali wakati wakichangia.
Aliyeanza kuchafua hali ya hewa ni mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje, ambaye alisema hali ya elimu nchini iko katika hali mbaya, lakini serikali haichukui hatua kutafuta ufumbuzi pamoja na mambo mengine yanayokwenda kombo.
Wenje alisema serikali inajali twiga wawili waliochukuliwa nchini na kupelekwa Uarabuni ambao alisema wana thamani ya Sh. milioni 100, na kuwapuuza wanafunzi 360,000 waliofeli mtihani wa kidato cha nne mwaka jana.
Alisema kama ubora wa elimu ni madaraka ndiyo maana hali iko hivyo.
Alisema ndiyo maana hotuba ya Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ya kutaka Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru kawambwa ajiuzulu kutokana na matokeo hayo mabaya.
Wenje ambaye alionekana kukerwa wabunge wa CCM kushangilia pale wabunge wao wanapozungumza mambo ya siyo na tija, alitumia msemo kwamba “akili ndogo inatawala akili kubwa”.
Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), alitumia maneno ya Biblia kwa kusema kuwa mtu mpumbavu hastahili heshima.
Alisema kupuuza mambo yaliyokuwamo katika hotuba ya Kiongozi wa Upinzani ni upumbavu na kwamba mpumbavu ukimweka kwenye kinu ukamchanganya na ngano na kumtwanga kwa kinu atabakia kuwa mpumbavu.
Alisema aliwahi kumweleza Waziri Mkuu kuhusiana na migogoro ya dini, lakini hakupewa majibu ya kuridhisha na kwamba kuna bunduki imekutwa katika Kanisa la Anglikana ambalo hakulitajwa ikiwa na risasi.
Baada ya hapo ndipo Lukuvi aliposimama na kueleza kuwa alishindwa kuvumilia wakati wabunge hao wakichangia kwa kutumia maneno makali ambayo hayapawi kutumika bungeni.
Naye Naibu Spika, Job Ndugai, alisimama na kueleza kuwa na yeye alishindwa kuwavumilia wabunge hao na kuonya matumizi ya maneno ya matusi.
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, alisimama na kuomba mwongozo kutoka kwa Ndugai kuhusu hatua ya Msigwa kutumia Biblia kuwatukana viongozi wa serikali.
Khatibu Said Haji, Konde (CUF), alihoji kama uchungaji wa Msigwa ni wa watu au wa nguruwe.
Alisema Msigwa amekuwa akiwatukana Wazanzibari na kuwaona kama tambala la kufutia makamasi.
Alisema mara nyingi hotuba za upinzani ambazo ni za Chadema zimekuwa zikiwashambulia Wazanzibari na kuwaona kama hawana maana na akutaka waonekane kama tambara la kufutia makamasi.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment