Wednesday, April 17, 2013

Ndesamburo ataka umeme wa uhakika K’njaro


JIBU LA SWALI LA MBUNGE MOSHI MJINI
NAIBU Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, amekiri kuwapo kwa tatizo la umeme katika Kanda ya Kaskazini hususan Mkoa wa Kilimanjaro, kwamba hali hiyo imetokana na mtandao wa umeme katika mkoa huo kuwa mkubwa.
Simbachawene alitoa kauli hiyo jana bungeni alipokuwa kijibu swali la Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo(CHADEMA), ambaye alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kutatua tatizo hilo la umeme.
Katika swali lake Ndesamburo alisema kuwa Kilimanjaro kuna mtandao mkubwa wa umeme wa gridi ya taifa, lakini umeme unaopatikana ni hafifu sana ambao haufai kutumika hata kuwasha  mshumaa.
Kutokana na hali hiyo, Ndesamburo alitaka serikali ieleze ina mkakati gani wa kurekebisha umeme huo ili uwe umeme wa ukweli tofauti na ilivyo sasa.
Akijibu swali hilo, Simbachawene alisema kuwa ni kweli kuna matatizo mbalimbali ya umeme katika Kanda ya Kaskazini hasa mkoani Kilimanjaro kutokana na ukweli kwamba mtandao wa umeme katika mkoa huo ni mkubwa na ni wa muda mrefu.
Alisema kuwa hali hiyo inasababisha kuzidiwa kwa gridi ya taifa kwa upande mmoja, na kuzidiwa kwa vituo vyote vya kupoozea umeme, hivyo kusababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara na kuwa na umeme hafifu kwenye mfumo.
Kutokana na hali hiyo serikali kupitia TANESCO inatekeleza mradi mkubwa wa TEDAP katika mikoa ya Kilimamjaro na Arusha ili kutatua matatizo ya umeme hafifu.
Simbachawene alieleza kuwa miradi hiyo ya kuimarisha umeme katika mikoa hiyo inahusisha ujenzi wa nijia kubwa ya kupoozea umeme ya msongo wa Kv 66 kutoka Kiyungi hadi Mkuyuni.

No comments:

Post a Comment