VIJANA na kinamama wamehamasishwa kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bila kujali vitisho vinavyotelewa na wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa mwishoni mwa wiki na Diwani wa Dodoma Makulu, Chiefi Ally Bilingi, alipozungumza na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata hiyo kwa lengo la uzinduzi wa tawi jipya la Mhande.
Chiefi Bilingi alisema wananchi wanatakiwa kutambua kuwa mapambano ya ukombozi yanataka watu kujitoa mhanga bila kuogopa jambo lolote, ili mradi hawavunji sheria ya nchi.
“Ndugu zangu wananchi ambao mliniamini na kunikabidhi kata hii ya Dodoma Makulu, sasa nataka kuwaeleza kinamama na vijana naomba mjitokeze kushika nafasi mbalimbali kupitia CHADEMA, ili kuweza kuikamata nchi.
“Msiogope vitisho najua CCM ina vitisho na ina mbinu nyingi za kuwafanya watu kushindwa kutetea haki zao.
“Nasema hivyo kwani mimi nilikuwa huko lakini sasa ninajivunia kuwa CHADEMA kwa maana naweza kusema ukweli na kuikosoa serikali. Ukiwa CCM huwezi kuikosoa serikali hata kama unaona wazi kinachofanyika si sahihi,” alisema.
Aidha aliwataka wananchi kuhakikisha wanafanya mageuzi katika kuwachagua viongozi kuanzia ngazi ya ubalozi hadi ngazi ya taifa, ili kufutilia mbali utawala wa CCM ambao haujali maslahi ya Watanzania.
Katika uzinduzi wa tawi hilo, Chiefi pia alisimamia uchaguzi wa viongozi wa tawi hilo kuanzia ngazi ya uwenyekiti, BAVICHA, Bawacha, wazee pamoja na mabalozi.
No comments:
Post a Comment