Sunday, April 14, 2013

Sugu awashambulia Mawaziri

MBUNGE wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema), maarufu kwa jina la Sugu, juzi alilishambulia Baraza la Mawaziri akisema kuwa limejaa wapumbavu. Tukio hilo lilitokea juzi jioni wakati mbunge huyo akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/14.

Sugu, alisema Baraza lote la Mawaziri linaundwa na wapumbavu, kwa kuwa linashiriki kubomoa nchi linayoiongoza.

“Kabla sijaanza kuchangia, nataka ninukuu maandiko katika biblia yanayosema kwamba: ‘Mwanamke mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe’ vilevile Serikali pumbavu inabomoa nchi yake yenyewe, yaani namaanisha Baraza la Mawaziri wapumbavu. 

“Mambo mengi nchi hii hayaendi kutokana na Serikali pumbavu, juzi hapa Mbatia (James Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa kupitia NCCR-Mageuzi) alileta hoja bungeni kuhusu mitaala ya elimu nchini, mkatumia wingi wenu kuinyanyapaa sasa matokeo ya form four (kidato cha nne), yamewaumbua.

“Hatuwezi tukawa na Waziri wa Elimu boya, mwenye elimu ya kuungaunga halafu tukafanya vizuri katika elimu.


Sugu alikwenda mbali akisema jambo hilo lilikuwa ni kazi ya Idara ya Usalama wa Taifa, kufanya uchunguzi wa mawaziri wanaotarajiwa kuteliuliwa na Rais ili kubaini uwezo wao.

Aliwashutumu Usalama wa Taifa kwa kuacha kufanya mambo hayo ya msingi na kubaki na kazi ya kuifuatilia Chadema na kung’oa watu kucha.

“Mimi binafsi sijisikii kuwa sehemu ya Bunge hili, kukaa na wabunge kama wakina Mwigulu (Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Iramba Magharibi kupitia CCM), huyu naye ni mpumbavu,” alisema Mbilinyi.

Kabla ya kuendelea na mjadala, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alimkatisha mbunge huyo na kumtaka kutotumia neno pumbafu wakati akiendelea kuchangia hoja yake.

Hata hivyo, Sugu aligoma kutotumia neno hilo kwa kusema kuwa: “Mheshimiwa Spika, naomba taifa lielewe upumbafu sio tusi ndio maana lipo hata kwenye biblia, upumabavu ni ‘stupidity’, lucky of knowledge of understanding’ ambayo mawaziri wote wanayo,” alisema Sugu.

Mbali na Sugu Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), naye akichangia mjadala huo, alisema Tanzania ni nchi tajiri ila wanaosababisha umasikini wa Watanzania ni viongozi.

“Kila kitu cha utajiri tunacho, nchi yetu ni nchi ya pili kwa vivutio vya utalii duniani, lakini mapato yetu ni chini ya asilimia 10, kwa nini tunashindwa kuwatajirisha Watanzania,” alihoji Kafulila.


Bonyeza Read More Kuendelea






Aliwataka pia wabunge kutokubali mkutano wa Bunge kumalizika bila majibu ya Serikali kuhusu taarifa za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

“Kwa sababu mnaona CAG anaikosoa Serikali mnaleta sheria za kuifinya ripoti yake, hii mnafanya kwa faida ya nani? Hii nchi ni yetu sote, hamuwezi mkasema nchi ni ya amani wakati mnakula wenyewe,” alisema.

Kafulila pia alizungumzia misafara ya viongozi isiyo na tija ambayo inasababisha fedha nyingi za Serikali kupotea.

Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala (CCM) akichangia hotuba hiyo ya bajeti yeye aliwashambulia Chadema akisema kuwa vitendo vyao ni vya kipuuzi.

Alisema Chadema wanachezea mchakato wa uundwaji wa Katiba mpya, kitendo alichodai kuwa ni cha kipuuzi.

Aliishangaa Serikali kuona inawaacha watu wachache kutaka kuharibu mchakato huo ambao ni muhimu kwa mustakabali wa taifa.

Mbunge wa Mkanyageni, Habibu Mnyaa (CUF) aliitaka Serikali kumaliza mgogoro wa Mtwara ndani ya miezi minne kwa kuwa mgogoro huo bado upo licha ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kusema umekwisha.

Aliyataja madai ya watu hao kuwa ni uzalishaji wa umeme wa Megawati 300 katika Mkoa wa Mtwara, kuunganisha mkoa huo katika gridi ya taifa na kufungua fursa za viwanda na bandari.

Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), alisema Serikali lazima ichukue tahadhari kulinda amani na umoja wa kitaifa nchini.

Alisema migogoro inayoendelea sasa kuhusiana na udini, ardhi na maliasili nyingine kama vile gesi idhibitiwe ili kuiepusha nchi katika machafuko.

No comments:

Post a Comment