Saturday, April 27, 2013

Ninalaani vikali kukamatwa kwa Lema! CHADEMA msipochora mstari... - Mwanakijiji

Sijui nitumie lugha gani kuelezea hisia zangu juu ya kile kinachoendelea nchini na hasa matumizi ya Jeshi la Polisi dhidi ya raia. Lakini siyo tu matumizi lakini hasa jinsi jeshi hili limekuwa likitumia nguvu kubwa sana kwa ajili ya vitu vidogo na hata visivyo na msingi. Kukamatwa kwa Lema na hasa namna alivyokamatwa ni dalili ya matumizi mabaya ya madaraka ya polisi (abuse of power). Kwamba, kwa vile polisi wana uwezo wa kupekua na kukamata basi wanaweza kufanya hivyo popote, kwa yeyote na kwa lolote wakijua kabisa kuwa hakuna wa kuwakemea. 

Jeshi la Polisi kama lilikuwa linamtaka Lema vibaya namna hiyo lingeweza kabisa kutumia njia za kawaida za kisheria ikiwemo kumpa wito wa kufika makao makuu ya Polisi wakimueleza anahitajika kwa nini na kama angekataa basi kupata kibali cha mahakama kumuendea na kumkamata na kama kutoa warranti ya kipolisi basi jambo hilo lingefanyika bila kuonesha hisia kuwa Lema analengwa bila ya sababu (targetted for no apparent reason) isipokuwa tu kwa vile ni Lema na ameonesha msimamo wake wa kutokuwapigia magoti watawala. Ni Uhuru huu wa Lema unawatisha watawala zaidi kuliko kitu kingine chochote. 

Mwendelezo wa vitendo vya aina hii dhidi ya wabunge wa CDM ni jambo la kukataliwa, kulaaniwa na kupingwa na kila mpenda demokrasia na anayeamini katika haki za raia (civil rights). Kwa miaka sasa tangu baada ya uchaguzi mkuu wa 2010 tumeona vyombo vya dola vikitumika kiunyanyasaji dhidi ya viongozi na wanachama wa CDM; kuanzia Arusha hadi Mbeya, Mwanza hadi Ruvuma, Dar hadi Kigoma. Ni vitendo vyenye lengo la kuwatisha na kuwakatisha tamaa viongozi na wanachama wa CDM lakini zaidi ni vitendo vyenye lengo la kufifisha na kudunisha mageuzi yanayokuja. 

Uongozi wa CDM unapaswa kuchora mstari - ambao naamini watashangaa kuwa umeshavukwa - wa kuhakikisha vitendo hivi vinakoma. Kuendelea kulalamika na kudai serikali na dola inawaonea hakutoshi tena (rejea "Karipio Kali). Nimewahi kuandika huko nyuma kuwa kama CDM hawatatuma ujumbe kuwa the balance of political power in the country has shifted - in CHADEMA'S favor - basi wajue wataendelea kunyanyaswa, kudhalilishwa, kuonewa na kubambikiziwa kesi na tuhuma za kila aina. Wanahitaji kuamua kama wataendelea kufanyiwa hivi au watume ujumbe kuwa "enough is enough". 

Wasipofanya hivi - na nimewahi kulisema hili pia - watajiandaa kulia na kusikitika na wasipoangalia kujikuta wanazika viongozi na wanachama wao kwani watawala hawaogopi maneno makali ya majukwaani, au vitisho vya matamko. CDM wafikirie namna moja itakayotuma ujumbe dhahiri, wa makusudi na usio na shaka wala utata kuwa mabadiliko ya nchi yanakuja na hakuna lolote ambalo CCM au serikali yake wanaweza kufanya kuzuia. NI mafuriko ya mabadiliko ambayo mkondo wake unatiririka kwa nguvu zote na CCM ama wapishe vinginevyo watasombwa. Jaribio la kuchimba mifereji na kuweka udongo njiani litafeli kwani mafuriko haya hayatakoma. 

Ni kwa sababu hiyo ninalaani vikali, na kupinga kitendo cha jeshi la POlisi kutumia nguvu ya chombo hicho kumkamata Lema - Mbunge wa ARusha na raia wa Jamhuri ya Muungano ambaye amekataa kufanya kile ambacho watu wengine ni rahisi kukifanya - kupiga magoti mbele ya madhabahu ya CCM na kutoa sadaka za sifa za uongo. 

MMM (BGM)

3 comments:

  1. Naunga mkono hoja ya Mzee Mwanakijiji, kwamba chadema kwa sasa mna kila support mnayoihitaji kutoka kwa wananchi hakuna sababu ya kuendelea kuburuzwa na hawa vikwaragosi.

    ReplyDelete
  2. Kwa hili Mzee Mwanakijiji nami nakuunga mkono. Nangoja kusikia kauli ya viongozi wa chama hiki, CHADEMA.

    ReplyDelete
  3. Mzee mwenzangu, za leo?

    Ni kweli kabisa umefika wakati CDM ni lazima wachore mstari ardhini mtu akivuka tu anapewa haki yake kisawa sawa

    Kama anatumia jino anapata jino,
    Kama anatumia nyengo anapata nyengo,
    kama anatumia kamba anapata kamba
    kama anatumia ngumi anapata ngumi,

    Mkuu wa mkoa sio Mungu wa Mkoa wala hatokua.
    Najua Mkuu wa mkoa kapata maagizo kutoka kwa baba Rizi1, ambaye naye hana mamlaka ya kumkamata raia yeyote bila kuwa na kosa na sembuse Mbunge??!!

    Mzee mwenzangu,
    CCM wametumia njia zote kuzuia nguvu na upepo mwanana wa mabadiliko nchini Tanzania na zote zimeshindwa.
    KWa muda mrefu walitumia uongo na kutishia watu nyau.
    Walijikweza na kudai mawazo yao ni sahihi kama ya Mungu wapi bwana tukawamaindi
    Wakatumia vitisho vya polisi fedha na kutongoza watu kwa kanga na fulana.

    Sasa wamerudi kwa nguvu zote wanatumia Polisi na staili yao maarufu ya kubambika kesi na kupindisha taratibu zote za kisheria Kifashisti.

    Mwenendo huu wa CCM hauwezi kukubalika hata kidogo.

    Nadhani sasa ni wakati wa kuiga mfano mzuri wa watu wa Mtwara na Lindi.

    Anakuibia anjenga Nyumba ya Fahari, gusa nyumba yake mpaka ubakie msingi.

    ReplyDelete