MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo amewataka viongozi waliopo madarakani kuwa waadilifu na kulinda rasilimali zilizopo.
Ndesamburo alisema hayo jana alipozungumza na wananchi kutoka kata za Pasua na Boma Mbuzi katika mkutano wa hadhara na kuongeza kuwa viongozi waliopo madarakani wanapaswa kufahamu kuwa wapo kwa ajili ya kulinda kodi za wananchi.
Alisema wapo baadhi ya viongozi si waadilifu na wamekuwa wakitumia mali za wananchi bila kujali kuwa ni ubadhirifu na kuwataka kufahamu wakati wowote watadaiwa kutokana na kutotimiza wajibu wao.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Japhary Michael, aliwataka viongozi wa CCM wanaodai kuwa CHADEMA ni chama cha kidini waache mara moja, kwani suala la udini katika siasa ni chanzo cha uvurugwaji wa amani.
Alisema CHADEMA haina chembechembe za udini na kamwe hawataruhusu hali hiyo kutokana na dhamira yao ya kuiongoza nchi bila ubaguzi.
No comments:
Post a Comment