CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeibuka kidedea katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kwekitui kilichopo Jimbo la Bumbuli linaloongozwa na January Makamba (CCM).
CHADEMA kimeibuka mshindi dhidi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hivyo kufikia idadi ya vijiji vitano kwenye uchaguzi huo wa marudio.
Kimepata ushindi katika uchaguzi huo ambao awali msimamizi wa uchaguzi alifuta matokeo kutokana na kile kilichodaiwa na CCM kutoridhishwa na mwenendo wa uchaguzi.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika jana, Msimamizi wa uchaguzi, Erick Muhumbo, alisema mgombea Miraji Mussa (CHADEMA) ameibuka mshindi kwa kumshinda mgombea wa CCM, Ally Nyangasa.
Muhumbo alisema watu walioandikishwa ni 396 na waliopiga kura ni 395 na kura 10 ziliharibika.
Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi huo yamezusha hofu kutokana na kwamba vijiji vilivyokwenda upinzani ndiyo ngome ya CCM Jimbo la Bumbuli.
Wakizungumza na Tanzania Daima baada ya matokeo hayo, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho walikiri kuwa ni ngome ya CCM na kusema anguko hilo ni mwanzo wa chama hicho kuchokwa na watu.
Shaban Mtunguja, aliuelezea uchaguzi huo kuwa ni dira ya CCM ya kuonyesha inakoelekea katika chaguzi zijazo na kwamba wananchi sasa wameamua kuiadhibu kutokana na ubabe na ukiritimba inaoendelea nao.
Aidha, Katibu wa CCM Wilaya ya Lushoto, Loth ole Lemeirut aliyaita matokeo hayo kuwa ni bahati mbaya licha ya kukiri kwamba hivyo ni vijiji ngome ya CCM na kusema kuwa ushindi huo ni wa hila na wanaangalia uwezekano wa kuyapinga matokeo mahakamani.
Aliyekuwa mratibu wa kampeni kuwakilisha uongozi wa CHADEMA Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje alisema hizo ni rasharasha na mvua itawaangukia CCM mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment