Thursday, April 11, 2013

Mbowe kuzindua kanda ya Pwani


KANDA maalumu ya kichama ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) inayohusisha mikoa ya Pwani, Ilala, Temeke na Kinondoni, itazinduliwa rasmi Aprili 14, mwaka huu.
Uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya Mailimoja wilayani Kibaha mkoani hapa na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa pamoja na wabunge wengine wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha jana, Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Pwani, Said Ukwezi alisema kuwa mkutano huo utatanguliwa na mapokezi ya viongozi wakuu wa chama saa nane mchana kisha kuelekea uwanjani.
Ukwezi alisema kuwa mkutano huo pia utatumika kuwatambulisha rasmi kwa wananchi viongozi wa chama hicho katika kanda hiyo na kuwaunganisha kwa ajili ya vuguvugu la mabadiliko (M4C) katika vijiji, mitaa, kata na majimbo yote ya mikoa ya kichama ya Pwani, Ilala, Temeke na Kinondoni.
Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo alilalamikia tabia ya Jeshi la Polisi ya kutaka kuwapangia wapinzani maneno ya kusema kwenye mikutano yao ya hadhara.
Alisema kuwa katika maeneo ya Bagamoyo, Rufiji na Kisarawe kila CHADEMA wanapoomba kibali cha kufanya mikutano, polisi wamekuwa wakiwaandikia barua kuwaelekeza mambo ya kuzungumza.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alikanusha madai hayo. “Hakuna kitu kama hicho, tunachokifanya sisi ni kuwasihi wazungumze maneno yasiyoikashifu serikali iliyoko madarakani,” alisema.

No comments:

Post a Comment