Saturday, April 13, 2013

Lissu amlipua Pinda kwa kushuka ufaulu


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), amemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kujiuzulu kwa kushindwa kumwajibisha Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, kutokana na ufaulu kushuka nchini.

Lissu aliyasema hayo jana wakati akichangia hotuba ya bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka 2013/14 iliyowasilishwa bungeni Jumatano wiki hii. Lissu alisema mwaka jana ripoti ya takwimu za ubora wa elimu nchini ( Best Education statitics), kuanzia mwaka 2007 hadi mwaka juzi inaonyesha kushuka kwa ufaulu nchini.

Alisema takwimu hizo ziliandaliwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na kwamba miongoni mwa mambo yaliyoainishwa katika kitabu hicho ni kuporomoka kwa elimu ya sekondari kwa kiasi kikubwa.

Alisema kitabu hicho kinaonyesha katika kipindi cha miaka mitano ya mwisho ya utawala wa serikali ya awamu ya tatu iliyoongozwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, ufaulu wa wanafunzi ulipanda.

Alisema ufaulu wa wanafunzi ulishuka kuanzia mwaka 2006 (awamu ya nne) ukilinganisha na miaka mitano ya mwisho ya uongozi wa Rais Mstaafu Mkapa. Alisema waliopata daraja la kwanza katika kipindi cha miaka mitano ya mwisho ya awamu ya tatu walikuwa ni asilimia tano, waliopata daraja la pili walikuwa ni asilimia saba, la tatu asilimia 21 wakati wa daraja la nne walikuwa asilimia 52.
Alisema hiyo inamaanisha kuwa wastani wa ufaulu katika miaka mitano hiyo ulikuwa ni asilimia 84.5 na waliofeli walikuwa asilimia 14.8.

Alisema baada ya Rais Kikwete walishuka kutoka asilimia tano hadi 3.3, waliopata daraja la pili walishuka kutoka asilimia 7 hadi 5.8, daraja la tatu walishuka kutoka asilimia 21 hadi 16.3 wakati daraja nne walishuka kutoka asilimia 52 hadi 51.7 wakati waliopata daraja O walipanda kutoka asilimia 14.8 hadi 22.8.

“Wastani wa kufaulu katika miaka mitano ya kwanza ya serikali ya awamu ya nne ulikuwa ni 77.2 na hivyo umeshuka kutoka asilimia 85.4. Ukiangalia takwimu za kila mwaka 2006 wanafunzi ufaulu wa daraja la kwanza ulikuwa ni 4.9 lakini mwaka juzi ufaulu ulishuka hadi asilimia 2.8 ,”alisema.
Alisema ufaulu umeporomoka katika kipindi cha miaka mitano ya awamu ya nne.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment