Mheshimiwa Spika,
Ofisi ya Waziri wa Maliasili na
Utalii ilianzishwa kwa mujibu wa kipengele cha 21 cha Nyongeza ya Waraka wa
Rais uliochapishwa kama Tangazo la
Serikali Na. 494 la tarehe 17 Desemba 2010. Majukumu ya Ofisi hii
yameainishwa katika Tangazo la
Ukasimishaji wa Majukumu ya Kiuwaziri la mwaka 2010 (The Ministers [Assignment
of Ministerial Functions] Notice, 2010) lililochapishwa katika Gazeti la Serikali kama Tangazo la Serikali Na. 494A la tarehe 17
Desemba 2010. Kwa mujibu wa TS Na. 494A, majukumu hayo ni pamoja na ufugaji
nyuki, wanyamapori, malikale, makumbusho na sera za utalii na utekelezaji wake.
Katika utekelezaji wa majukumu haya, Ofisi hii ina idara mbali mbali kama vile
wanyama pori, utalii, mambo ya kale, usimamizi wa rasilmali watu, sera na
mipango. Aidha, Ofisi ina taasisi zinazojitegemea kama vile Mamlaka ya Hifadhi
za Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Uhifadhi wa Eneo la Ngonrongoro (NCAA). Vile
vile, Ofisi ina wakala na mifuko ya uhifadhi kama vile Wakala wa Misitu
Tanzania (Tanzania Forestry Agency) na Mfuko wa Uhifadhi Wanyamapori Tanzania
(Tanzania Wildlife Conservation Trust Fund) na Mfuko wa Hifadhi ya Misitu ya
Milima ya Tao la Mashariki (The Eastern Arc Mountains Forests Conservation
Trust Fund). Na mwisho, Ofisi ina vyuo mbali mbali kama vile Chuo cha Misitu
Olmotonyi, Vyuo vya Wanyamapori Mweka na Pasiansi.
Bonyeza Read More Kuendelea
Bonyeza Read More Kuendelea
Ni hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni kwamba Ofisi ya Waziri wa Maliasili na Utalii imeshindwa kutekeleza
majukumu yake kama yalivyoainishwa katika Tangazo la Serikali tajwa. Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba sababu kubwa ya kushindwa huko
kutekeleza majukumu ya kisheria ya Ofisi hii ni ufisadi na matumizi mabaya ya
madaraka ambao umetapakaa katika kila sehemu ya Ofisi hiyo ukiwahusisha
watendaji wake wakuu pamoja na watendaji wa ngazi za juu za Chama cha Mapinduzi
(CCM) na wafanya biashara makada wa chama hicho. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaamini kwamba kushindwa kwa Ofisi hii kutekeleza majukumu yake hayo
kumehatarisha utajiri mkubwa wa maliasili za nchi yetu kama vile wanyamapori,
misitu na malikale, na kulitia aibu kubwa taifa letu kwamba ndio chanzo kikubwa
cha ujangili wa kimataifa na biashara haramu ya wanyamapori. Maliasili kama
wamanyapori hai na nyara nyingine za serikali zimeporwa na kusafirishwa nje ya
nchi yetu kwa kupitia viwanja vyetu vya ndege vya kimataifa pamoja na bandari
zetu bila hatua stahiki kuchukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi
yetu.
Mheshimiwa Spika,
Bunge lako tukufu limepitisha
maazimio mengi kuhusu kashfa mbali mbali zilizogubika utendaji wa Ofisi ya
Waziri wa Maliasili na Utalii na utekelezaji wa majukumu yake kisheria. Aidha,
Bunge lako limeunda Kamati za Uchunguzi ili kuchunguza tuhuma za ukiukaji
sheria na matumizi mabaya ya mamlaka katika utekelezaji wa majukumu ya Ofisi.
Hata hivyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitika kuliambia Bunge lako
tukufu, maazimio ya Bunge yamepuuzwa na taarifa za Kamati zake za Uchunguzi
kuzimwa. Na katika hili, Mheshimiwa Spika, lawama za kwanza lazima zitupiwe
katika Ofisi yako mwenyewe kwa kuwa ndio imekuwa kaburi kubwa la kuzikia
taarifa za Kamati za Bunge ambazo pengine Ofisi yako inaona zitaonyesha udhaifu
katika utendaji wa Serikali hii ya CCM!
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 27 Aprili mwaka 2006 aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii Anthony Diallo aliunda Kamati ya Maalum ya Uchunguzi Kuhusu Uboreshaji wa Tasnia ya Uwindaji
wa Kitalii Tanzania. Lengo la kuundwa kwa Kamati hiyo lilikuwa ni “…
kuchambua na kubaini matatizo yanayoikabili tasnia ya uwindaji wa kitalii na …
namna ya kuyatatua matatizo hayo na kuboresha tasnia hiyo.” Kamati ya Diallo
iliwasilisha Taarifa Kuhusu Uboreshaji wa
Tasnia ya Uwindaji wa Kitalii Tanzania mwezi Juni 2006. Pamoja na mengine,
Kamati hiyo iligundua kwamba licha ya biashara ya uwindaji wa kitalii kutakiwa
kuwa “… ni chanzo kikubwa cha mapato ya fedha za kigeni, (biashara hiyo)
inaingiza fedha kidogo, wastani wa dola za Kimarekani milioni tisa tu kwa mwaka
wakati wenzetu wa Zimbabwe, (biashara) hii inawaingizia dola milioni thelathini
kwa mwaka.”
Aidha, Kamati iligundua kwamba “…
makampuni mengi ya uwindaji hayaajiri wataalam wa ndani ila huwatumia wananchi
kwa kazi ndogo ndogo wakati wa msimu wa uwindaji. Makampuni haya pia
yanawatumia wawindishaji kutoka nje ya nchi badala ya kutumia wawindishaji
bingwa wa Kitanzania.” Vile vile, Kamati ilibaini kwamba licha ya kuwepo
makampuni mengi yanayomilikiwa na raia wa Tanzania, makampuni machache ya
kigeni yanamiliki idadi kubwa ya vitalu vya uwindaji ambavyo vina “… wanyama
wengi ukilinganisha na vitalu vya makampuni ya wananchi ambavyo viko kwenye
maeneo ambayo hayana wanyama wengi.”
Na mwisho, Kamati ilibaini kwamba
“Idara ya Wanyamapori haisimamii kikamilifu tasnia hii kwa maana haina taarifa
muhimu kuhusu vitalu na thamani halisi ya vitalu hivi.” Kwa kadri ya taarifa za
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Taarifa hii ya Kamati ya Diallo haijawahi
kutolewa hadharani na wala kuwasilishwa kwenye Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Inaelekea Kamati ya Diallo
ilitokana na Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2005-2010, iliyokuwa imewaahidi
Watanzania kwamba Serikali ya CCM itaendelea “... kuelekeza nguvu zake katika
kuhifadhi, kulinda, kuendeleza, kudumisha na kuvuna maliasili kwa manufaa ya
Taifa letu.” Ahadi hiyo ilirudiwa kwa karibu maneno hayo hayo katika Ilani ya
Uchaguzi ya CCM 2010-2015. Aidha, tuliambiwa na CCM katika Ilani yake ya 2005
kwamba Serikali yake itahimiza “... miji ianzishe bustani za ufugaji wa
wanyamapori (zoos) kwa maonyesho.” Hakuna bustani ya wanyamapori hata moja
iliyoanzishwa katika kipindi hicho na ndio maana ahadi hiyo ilipotea kabisa
katika Ilani ya CCM ya 2010!
Na kama tutakavyothibitisha,
Serikali ya CCM imeshindwa kabisa kutekeleza mapendekezo ya Kamati ya Diallo.
Badala yake, Serikali hii imeelekeza nguvu zake katika kudidimiza na
kudhoofisha uhifadhi, ulinzi na uendelezaji wa maliasili za nchi yetu. Aidha,
Serikali ya CCM sio tu imeelekeza nguvu kubwa katika uvunaji haramu wa
maliasili za nchi yetu, bali pia imefanya hivyo kwa manufaa ya wafanya biashara
wa kigeni wakishirikiana na wafanya biashara wachache ndani ya nchi na viongozi
waandamizi wa CCM na makada waandamizi wa chama hicho.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka 2009 Bunge lako tukufu
liliunda Kamati ya Uchunguzi ili kuchunguza matukio ya ukiukwaji mkubwa wa haki
za binadamu za wananchi wa Liliondo katika Wilaya ya Ngorongoro ambapo wananchi walidaiwa
kuchomewa nyumba zao na wanawake kudhalilishwa na Jeshi la Polisi. Taarifa ya Kamati hiyo,
iliyoongozwa na Naibu Spika wa sasa wa Bunge lako tukufu, Mhe. Job Ndugai, haikuwasilishwa
Bungeni na, kwa kadri ya ufahamu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imezikwa
kwenye kaburi la Ofisi ya Spika. Matokeo yake, mgogoro kati ya wananchi wa
Loliondo kwa upande mmoja, na Serikali ya CCM na Kampuni ya Orthello Business
Corporation (OBC) inayomilikiwa na mfanyabiashara kutoka Oman kwa upande
mwingine, umezidi kuwa mkubwa kama inavyothibitishwa na maasi ya wananchi wa
Loliondo dhidi ya CCM yaliyoshuhudiwa mwezi uliopita na viongozi na makada wa
CCM waliopo ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka jana Kamati Ndogo ya Kamati ya Kudumu ya
Maliasili, Utalii na Mazingira iliwasilisha taarifa ndani ya Bunge lako tukufu kuhusu
utoroshwaji wa wanyamapori hai. Kufuatia kuwasilishwa kwa taarifa hiyo, Bunge
lilipitisha azimio, pamoja na mengine, kwamba Serikali itengeneze kanuni za
uwindaji ili “… iweze kubana mianya ya rushwa inayoikosesha mapato (na kanuni hizo)
ziwe tayari ndani ya mwaka mmoja kuanzia sasa.” Bunge lako liliazimia pia kwamba
wale wote waliohusika na utoaji wa kibali cha kutorosha wanyama hai wachukuliwe
hatua za kinidhamu. Aidha, Bunge liliitaka “… Serikali kuchukua hatua stahiki
za kisheria dhidi ya watumishi waliohusika kutoa kibali hicho.” Mwisho, Bunge
lako lilirudia mapendekezo ya Kamati ya Diallo ya kuunda mamlaka maalumu kwa ajili
kushughulikia masuala ya biashara ya wanyamapori na uwindaji wa kitalii. Bunge
lako liliipa Serikali kipindi cha mwaka mmoja kutekeleza maazimio hayo. Hadi
wakati wa kuwasilisha Maoni haya Serikali imepuuza utekelezaji wa maazimio ya
Bunge lako tukufu kuhusu jambo hili. Aidha, licha ya Mheshimiwa Waziri kutoa
ahadi kwa Bunge lako tukufu kuwa wanyamapori hai waliotoroshwa nje ya nchi
watarudishwa nchini, hadi leo ahadi hiyo haijatekelezwa na Bunge hili
halielekei kutaka kuchukua hatua stahiki kwa Mheshimiwa Waziri kwa kupuuza kutekeleza
ahadi ya Serikali ya CCM kwa Bunge.
Mheshimiwa Spika,
Mwaka jana Mheshimiwa Waziri alichukua
vielelezo kutoka kwa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu masuala
ya ardhi Mh. Halima Mdee juu ya kampuni ya uwindaji ya Game Frontiers kukodisha
kitalu chake cha uwindaji kwa ajili ya utafutaji wa madini ya urani katika eneo
la Mbarang’andu katika Wilaya ya Namtumbo. Mh. Waziri aliahidi kwamba atachukua
hatua stahiki kuhusiana na suala hilo. Hadi ninapowasilisha Maoni haya,
Serikali haijaeleza hatua zozote, kama zipo, ilizochukua kumnyang’anya mmiliki
wa kampuni hiyo ya uwindaji leseni ya uwindaji katika eneo hilo kwa kukiuka
masharti ya leseni hiyo. Aidha, hadi sasa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni bado
inasubiri majibu ya Serikali kuhusiana na ujangili wa tembo unaohusisha watendaji
wa Serikali kwa kushirikiana na makada wa CCM.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 28 Julai, 2007, aliyekuwa
Waziri wa Maliasili na Utalii Mh. Prof. Jumanne Maghembe alipatiwa taarifa ya
kitafiti juu ya Uwindaji Haramu Katika
Pori Tengefu la Selous na Maeneo Yanayolizunguka iliyoandaliwa na Bw.
Baruani Mshale wa Shule ya Masomo ya Misitu na Mazingira ya Chuo Kikuu cha Yale
cha Marekani. Pamoja na mengine, taarifa ya Bw. Mshale ilidai kwamba kumekuwa
na ‘maslahi haramu’ (vested interests) kati ya Serikali na wafanya biashara wa
uwindaji wa kitalii wa nje ambayo yamesababisha Serikali kufanya maamuzi
yasiyofaa yanayowanyima wananchi vijijini faida zitokanazo na utajiri wao wa
maliasili. Mtafiti huyo anataja viashiria vya maslahi hayo haramu kuwa ni
pamoja na mvutano kati ya Mkurugenzi wa Wanyamapori na aliyekuwa Waziri wa
Maliasili na Utalii na uamuzi wa Rais kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri
ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii aliondolewa kwenye Wizara hiyo. Katika
kile kinachoonekana kwamba ‘maslahi haya haramu ya kisiasa kwa faida ya
kiuchumi ya watu wachache’ yanajulikana serikalini, Mtafiti Mshale alimwambia
Waziri kwamba “inawezekana nakukumbusha kitu ambacho tayari unakifahamu”!
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaamini kwamba ‘maslahi haramu ya kisiasa kwa faida ya kiuchumi ya watu
wachache’ katika sekta ya uwindaji wa kitalii imekithiri ndani ya CCM na
Serikali yake na inawahusisha viongozi na watendaji waandamizi wa chama hicho
na Serikali yake. Kwa mfano, mwaka 2009 shehena ya pembe za ndovu zenye
uzito wa tani 4 kutoka nchini Tanzania na Kenya zilizoripotiwa kukamatwa na
vyombo vya usalama vya Vietnam ilisafirishwa na kampuni ya wakala wa meli
iitwayo Sharaf Shipping Co. Ltd. Taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na
Makampuni (BRELA) zinaonyesha kwamba Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana
anamiliki robo tatu ya hisa za Sharaf Shipping Co. Ltd., wakati robo iliyobaki
ya hisa hizo inamilikiwa na mtu aitwaye Rahma Hussein. Kwa mujibu wa taarifa
ilizonazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Rahma Hussein ni mkewe Abdulrahman
Kinana!
Sio tu kwamba kampuni ya Katibu Mkuu
wa CCM na mkewe imehusishwa na usafirishaji haramu wa pembe za ndovu kutoka
Tanzania, kampuni hiyo inaelekea kutoa ajira haramu kwa wageni. Wakati shehena
ya meno hayo tembo inakamatwa nchini Vietnam, nyaraka zilizoambatana na shehena
hiyo zilionyesha kwamba kibali cha kusafirisha shehena hiyo kilisainiwa na raia
wa India anayeitwa Samir Hemani mnamo tarehe 13 Novemba 2008. Hemani alikuwa
Meneja wa Fedha na Utawala wa Sharaf Shipping Co. Ltd. Hata hivyo, nyaraka za
Idara ya Uhamiaji ambazo Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imezipata zinaonyesha
kwamba wakati Hemani anasaini kibali cha kusafirisha shehena ya meno ya tembo
kwa niaba ya wateja wa Kinana na mkewe, kibali chake cha kuishi Tanzania
kilikuwa kimeisha tangu tarehe 7 Mei, 2008!
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kuhusu
kushiriki kwa Katibu Mkuu wa CCM katika kusafirisha kiharamu nyara za serikali
ambazo kwa vyovyote vile zinathibitisha kuwepo kwa ujangili wa kutisha unaohusu
maliasili wanyamapori wa nchi yetu. Vile vile, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali hii ya CCM itoe kauli mbele ya Bunge lako tukufu juu ya
kuhusika kwa Katibu Mkuu wa CCM katika kuajiri wafanyakazi wageni ambao
walikuwa wanaishi nchini kinyume cha sheria.
Mheshimiwa Spika,
Taarifa ya Tume ya Rais ya Kuchunguza
kero ya Rushwa Nchini ya mwaka 1996 iliyoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu Joseph
Sinde Warioba ililalamikia kile ilichokiita ‘ukaribu wa
wafanyabiashara na viongozi wa kisiasa’ ulioanza kujitokeza mwanzoni mwa
kipindi cha pili cha serikali ya awamu pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi. Taarifa
hiyo ilitoa mfano wa makampuni ya Kigoma Hill Top Hotel, Shenis
Commercial Ltd., Tile and Tube Ltd., Royal Frontier (T) Ltd., Game Frontier (T) Ltd. nee MNM Hunting Safaris Ltd., ambayo
yalikuwa yanamilikiwa na mfanyabiashara Mohsin Abdallah, mkewe Nargis Abdallah
na washirika wao wengine wa kibiashara.
Mohsin Abdallah ni kada maarufu wa
CCM na mjumbe wa zamani wa Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho. Inaelekea kuwa
mfanya biashara na kada huyu maarufu wa CCM ameendelea kuwa na ushawishi mkubwa
ndani ya Serikali ya CCM na hasa hasa katika Wizara ya Maliasili na Utalii.
Zaidi ya hayo, inaelekea kwamba, kama ilivyokuwa kwa Tume ya Warioba miaka kumi
na saba iliyopita, ushawishi mkubwa alionao kada huyu wa CCM unatoa uvundo na
harufu mbaya ya ufisadi.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati Ndogo
ya Kamati ya Kudumu ya Maliasili na Mazingira iliyotolewa ndani ya Bunge hili
tukufu, “Kampuni tatu zenye majina yanayoelekea kufanana na zina Ofisi katika
jengo moja, Royal Frontiers of Tanzania Ltd., Game Frontiers of Tanzania Ltd.,
Western Frontiers of Tanzania Ltd., … zinaonyesha kuwa wanahisa wa Kampuni hizo
wana nasaba za kifamilia hivyo kuleta hisia kuwa lengo la Sheria na Kanuni
kuzuia mtu mmoja kumiliki vitalu zaidi ya vitano linapuuzwa kwa ujanja wa
kusajili Kampuni mpya kwa malengo fulani…. Kamati ilipata ushahidi wa Maelezo
ya Kampuni zinazofanya biashara ya uwindaji wa kitalii kuwa mmiliki wake ni
mmoja, na hata maelezo ya baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kumshauri Waziri
kuhusu Ugawaji wa Vitalu yanaashiria kuwa kampuni zote hizo zinamilikiwa na mtu
mmoja, hali inayoweza kusababisha mtu huyo kupata vitalu vingi kinyume cha
Sheria.”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya Bunge hili tukufu juu ya mahusiano yake
na mfanya biashara na kada huyu wa CCM ambayo yamepigiwa kelele kwa karibu
miaka ishirini. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua kama huu sio
mfano wa wazi wa ‘maslahi haramu ya kisiasa kwa faida ya kiuchumi ya watu
wachache’, basi Serikali iliambie Bunge lako tukufu kuna maslahi gani ya umma
katika mahusiano haya.
Mheshimiwa Spika,
Mohsin Abdallah sio mfanya biashara
na kada pekee wa CCM mwenye maslahi yenye mashaka katika sekta ya uwindaji wa
kitalii. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati ya Diallo, makada waandamizi wa CCM
wenye maslahi ya aina hii ni wengi na baadhi yao wako humu ndani ya Bunge lako
tukufu. Taarifa hiyo inayataja makampuni ya Coastal Wilderness (Tz) Ltd.,
ambayo wakurugenzi wake wanatajwa kuwa Napono Edward Moringe Sokoine na Namelok
Edward Moringe Sokoine; Enzagi Safaris (Tz) Ltd., yenye wakurugenzi Makongoro
Nyerere na Mh. Muhamed Seif Khatib; Said Kawawa Hunting Safaris yenye
wakurugenzi Chande Kawawa na Hassan Kawawa; na M.S.K. Tours & Hunting
Safari Co. ya Mh. Muhamed Seif Khatib.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Kamati Ndogo
ya Kamati ya Maliasili na Mazingira, mengi ya makampuni haya yalipewa vitalu
vya uwindaji wakati hayana uzoefu wala mtaji wa kuendesha biashara ya uwindaji
wa kitalii katika vitalu hivyo. Matokeo yake ni kwamba makampuni hayo
yalishindwa kusimamia uhifadhi wa wanyamapori katika vitalu vyao na kusababisha
tatizo la ujangili kushamiri katika vitalu hivyo. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli mbele ya Bunge lako tukufu ni kwa nini
Serikali hii ya CCM imekuwa ikitoa vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa makada
waandamizi wa CCM ambao wanajulikana kuwa hawana weledi wala uwezo wa
kibiashara wa kuendesha biashara ya uwindaji wa kitalii na hivyo kusababisha
tatizo la ujangili kuwa kubwa zaidi na kuleta hasara kwa taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
Nchi yetu imeanza kufedheheshwa
katika mikutano ya kimataifa ya uhifadhi kwa sababu ya Serikali hii ya CCM
kukumbatia makada waandamizi wa CCM wanaojihusisha na ujangili. Kwa mfano
katika Mkutano wa 16 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Biashara ya Kimataifa ya
Wanyama Walio Hatarini Kutoweka (CITES) uliofanyika Bangkok, nchini Thailand
mwezi uliopita, Mohsin Abdallah alitajwa na Shirika la Upelelezi wa Masuala ya
Mazingira (Environmental Investigations Agency, EIA) kuwa ni mmoja wa majangili
wakubwa wanaojihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo lakini Serikali ya
Tanzania imeshindwa kumchukulia hatua za kisheria kwa sababu ya ushawishi wake
mkubwa katika siasa za ndani ya chama tawala na Serikali hii ya CCM. Kambi Rasmi
ya Upinzani Bungeni inataka kujua ni fedheha ya aina gani kimataifa
itakayoiamsha Serikali hii ya CCM katika usingizi wake wa pono ili iweze
kuchukua hatua za kisheria dhidi ya makada wa CCM wa aina hii?
UKIUKWAJI WA
HAKI ZA WAMAASAI
HIFADHI YA
ENEO LA NGORONGORO
Mheshimiwa Spika,
Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na
Loliondo ni moja ya maeneo ya asili ya jamii za Wamaasai. Kwa mujibu wa taarifa
za kitafiti za ekolojia ya maeneo haya, Wamaasai wameishi katika maeneo hayo
tangu karne ya kumi na nane. Kabla ya mwaka 1959 eneo hili lilikuwa ni sehemu
ya maeneo ya Serengeti-Ngorongoro ambayo yalikuwa yakikaliwa na wafugaji wa
Kimaasai. Mwaka 1959 Serikali ya kikoloni iliigawanya Serengeti-Ngorongoro
baada ya kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa magharibi, na
Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro upande wa milima ya mashariki ya eneo la ekolojia
la Serengeti-Ngorongoro.
Wafugaji wa Kimaasai waliokuwa
wakiishi katika maeneo ya Seronera, Moru na Sironet katika upande wa magharibi
waliondolewa katika maeneo hayo na kuhamishiwa Hifadhi ya Eneo la Ngoroongoro
na Loliondo. Hata hivyo, Serikali ya kikoloni iliahidi kwamba haki za Wamaasai
juu ya ardhi za maeneo walikohamishiwa zitapewa kipaumbele na kulindwa na
Serikali. Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya kikao cha Baraza la Kutunga la Sheria
(LEGCO) cha siku ya Jumatatu ya tarehe 17, Novemba 1953, Gavana wa Tanganyika
wa wakati huo alisema yafuatayo: “Wakati eneo hili lilipotangazwa kuwa hifadhi
ya taifa, ilitambuliwa kwamba kulikuwa na watu waliokuwa na haki za asili za
machungio ya mifugo na maji ndani ya mipaka yake na kwamba haitawezekana
kuwaondoa watu hawa kwa nguvu.”
Kauli hii ya Serikali ilitiliwa nguvu
na Waraka wa Serikali Na. 1 wa 1956 (Government Sessional Paper No. 1 of 1956)
uliochapishwa kufuatia kuongezeka kwa shinikizo la mashirika ya uhifadhi ya
kimataifa yaliyokuwa yanataka Wamaasai wafukuzwe katika maeneo ya
Serengeti-Ngorongoro: “Kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti chini ya
Sheria ya Wanyamapori na baadaye kuundwa kwake upya chini ya Sheria ya Hifadhi
za Taifa hakukuathiri kwa namna yoyote haki zilizokuwepo za mtu yeyote ndani au
juu ya ardhi za Hifadhi. Badala yake, haki hizo sio tu
kwamba zililindwa wazi wazi, bali pia Wamaasai waliokuwa tayari wanaishi ndani
ya eneo la Hifadhi walipewa ahadi chanya na Serikali kwamba haki zao
hazitavurugwa bila ridhaa yao.”
Kufuatia kuchapishwa kwa Taarifa ya
Tume ya Uchunguzi juu ya Ngorongoro iliyoongozwa na Sir Barclay Nihill
aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki, iliyopendekeza Wamaasai
wafukuzwe Serengeti na pia katika maeneo ya Kreta za Ngorongoro na Empakaai,
Serikali ya kikoloni ilirudia msimamo wake kuhusu haki za Wamaasai wa
Serengeti-Ngorongoro katika Waraka wa Serikali Na. 6 wa 1956 (Government
Sessional Paper No. 6 of 1956): “Mapendekezo ya kuwa na maeneo tengefu katika
Kreta hizo mbili hayakukubalika. Yanaashiria kuondolewa kwa Wamaasai kutoka
kwenye maeneo haya mawili. Haikuonekana sawa sawa kuomba ridhaa ya Wamaasai
kuachia haki zao ndani ya Kreta hizo mbili wakati huo huo wakiwa wanaachia haki
zao ndani ya Hifadhi yenyewe.”
Mheshimiwa Spika,
Ahadi za kulinda haki za ardhi za
Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro ziliendelea kutolewa kwa nyakati tofauti na
viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya kikoloni ya Tanganyika. Hivyo basi,
katika kikao cha Baraza la Kutunga Sheria cha tarehe 25 Aprili 1956, Gavana Sir
Richard Turnbull aliliambia Baraza hilo kwamba: “Wakati Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti ilipoanzishwa mwaka 1940, ahadi rasmi zilitolewa na Serikali hii kwa
Wamaasai. Hii haimaanishi kwa kabila lote la Wamaasai bali wale waliokuwa na
haki za kisheria au za asili katika eneo hilo. Nina uhakika kabisa kwamba
hakuna mtu yeyote anayeweza kutegemea Serikali hii, au Serikali yoyote ya
Kiingereza kuvunja ahadi zake rasmi. Imekuwa ni lazima, kwa hiyo, kupata ridhaa
ya Wamaasai kwa ajili ya mabadiliko yanayopendekezwa.”
Miaka miwili baadae Gavana Turnbull
alirejea kauli yake hiyo wakati akifungua Mkutano wa 34 wa Baraza la Kutunga
Sheria tarehe 14 Oktoba, 1958: “Nadhani ni lazima nichukue fursa hii kusisitiza
kwamba kwa misingi yote ya haki na nia njema hakuna Serikali itakayofikiria
kuwaondoa Wamasai kutoka maeneo yote ya hifadhi za wanyama za Serengeti na
Nyanda za juu za Kreta.” Kama
inavyojulikana, baadae Serikali ya kikoloni iliingia mkataba na Wamaasai ambapo
Wamaasai walikubali kuhama kutoka maeneo yao ya Sironet, Moru na Seronera ndani
ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kuhamia kwa eneo jipya la Hifadhi ya
Ngorongoro. Kwa maneno ya Gavana Turnbull, “… uhifadhi wa eneo la Ngorongoro
utajengwa kuzunguka nguzo ya maslahi ya wenyeji wa eneo hilo.”
Na katika mwaka ambao Eneo la Hifadhi
ya Ngorongoro ilianzishwa, yaani 1959, Gavana Turnbull alisisitiza msimamo wa
Serikali yake juu uhifadhi wa Ngorongoro kujengwa kwa kuzingatia maslahi ya wakazi wake katika hotuba
aliyoitoa mbele ya Halmashauri ya Wilaya ya Maasai mwezi Agosti 1959:
“Nataka kuweka wazi kwenu wote kwamba ni
nia ya Serikali kuendeleza Crater kwa maslahi ya watu na matumizi yake, wakati
huo huo Serikali inakusudia kulinda hifadhi ya wanyama katika eneo hilo, pamoja
na kuwepo kwa mgongano wa jamii na serikali bado serikali inathamini na
kuheshimu shughuli za jamii na haitaingilia shughuli za wafugaji wa Kimaasai.”
Mheshimiwa Spika,
Makubaliano kati ya Serikali ya kikoloni
na Wamaasai wa Serengeti-Ngorongoro yalikuwa ndio msingi wa kutungwa kwa Sheria
ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ya 1959. Sheria hiyo iliweka msingi kwamba
eneo hilo litakuwa ni eneo la matumizi mseto wa rasilmali ambako Wamaasai
wataruhusiwa kuishi na kutumia maeneo ya Ngorongoro kwa ajili ya malisho ya
mifugo yao. Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NGorongoro Conservation
Area Authority, NCAA) ilipewa majukumu ya kisheria ya kuhifadhi maliasili za
eneo hilo na pia kuwaendeleza Wamaasai kiuchumi.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa
mingi Serikali ya Tanzania imeshiriki katika ukiukwaji mkubwa wa haki za
binadamu za Wamaasai wa Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Loliondo katika Wilaya
ya Ngorongoro. Serikali pia imekiuka wajibu wake wa kuwaendeleza Wamaasai wa
Ngorongoro kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi ya Eneo la
Ngorongoro. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 1995 na Shirika la Misaada
la Denmark (DANIDA), licha ya NCAA kupokea mamilioni ya fedha za kigeni
kutokana na utalii unaoendeshwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, umaskini
katika familia za Kimaasai ulifikia hatua ambayo 50% ya kaya zao zilikuwa na
chini ya mifugo saba kwa kaya – ambacho kinachukuliwa kuwa chini ya kiwango cha
kujikimu kiuchumi – wakati 40% ya kaya hizo zilichukuliwa kuwa ni fukara kwa
maana ya kuwa na chini ya mifugo miwili kwa kaya.
Miaka karibu ishirini baadaye, hali
ya kiuchumi na kijamii ya Wamaasai wa Ngorongoro imekuwa ni mbaya zaidi kuliko
ilivyokuwa wakati wa utafiti huo wa DANIDA. Ushahidi wa suala hili ni Taarifa ya
Tume ya Uchunguzi ya CCM iliyoundwa na Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahman Kinana na
kuongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Tanzania Bara, Mh. Mwigulu Nchemba iliyosambazwa
jana tarehe 29 Aprili 2013. Wajumbe wengine wa Tume hiyo ni pamoja na Mbunge wa
Longido Mh. Lekule Laizer, Mbunge wa Simanjiro Mh. Christopher ole Sendeka na
Mbunge wa Viti Maalum na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha Mh. Mary Chatanda.
Ukimwacha Mh. Chatanda, wajumbe wengine wa Tume hiyo ni wajumbe wa NEC ya CCM.
Kwa vyovyote vile, taarifa ya Tume hiyo ya uchunguzi inahitaji kupewa uzito na
umuhimu wa kipekee kutokana na uzito kichama wa wajumbe walioiandaa.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya
Mwigulu Nchemba: “Kutokana na ukosefu wa ardhi ya kuendeshea shughuli za
kiuchumi, umaskini umekithiri miongoni mwa wakazi wa Ngorongoro kiasi cha
kupelekea wakuu wa familia kukimbia familia zao.” Ukosefu wa ardhi unaopelekea
umaskini kukithiri ni wa kutengeneza na Serikali hii ya CCM kwani kati ya km2
14,036 ambazo ndio eneo lote la Wilaya ya Ngorongoro, km2 8281 au
59% zimechukuliwa na Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wakati km2 870 au
6% zimechukuliwa na Hifadhi ya Misitu ya Nyanda za Juu Kaskazini. Maeneo ya
wanyamapori na malisho ya mifugo ni km2 3916 au 30%, wakati maeneo
ya kilimo ni km2 435 au 3% ya eneo lote la Wilaya hiyo.
Katika miaka ya mwanzo 2000, NCAA ilipiga
marufuku kilimo cha mazao ya chakula katika maeneo ya Nainokanoka na Endulen
ambayo yako ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Matokeo ya sera hizi za
kuwanyang’anya wananchi wa Ngorongoro ardhi kwa ajili ya mifugo yao na kupiga
marufuku kilimo yamekuwa, kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba, ni
“... tatizo ... sugu la njaa isiyoisha katika Tarafa ya Ngorongoro.” Taarifa
hiyo inafafanua zaidi: “Wananchi wa Ngorongoro wana njaa ya muda mrefu ambayo
haijapatiwa ufumbuzi. Wananchi hawa hawaruhusiwi kulima ndani ya Hifadhi hivyo
hutegemea mgawo wa chakula toka Mamlaka ya Hifadhi.” Ahadi ya Rais Dokta
Kikwete kuwa Serikali ya CCM itashughulikia suala la kilimo cha kujikimu
ambacho kingewasaidia Wamaasai kujipatia chakula, ahadi hiyo haijatekelezwa
licha ya ukweli kwamba “... Mamlaka ya Hifadhi imeshindwa kuwapatia chakula.”
Hivyo, kama walivyosema Profesa Issa
G. Shivji na Dr. Wilbert Kapinga katika kitabu chao The Maasai Rights in Ngorongoro, Tanzania, Serikali ya Tanzania,
kwa kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, imekiuka sio tu haki za
binadamu za Wamaasai wa Ngorongoro, bali pia imeshindwa kutekeleza wajibu wake
wa kuwaendeleza Wamaasai hao kama inavyotakiwa na sheria. Kwa maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, hiki ndio chanzo cha migogoro ya ardhi ya muda mrefu
na isiyomalizika kati ya Wamaasai na Serikali ya CCM na mashirika yake ya
uhifadhi wa wanyamapori. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaamini kwamba njia
pekee ya kutatua matatizo ya kiuchumi na kijamii ya Wamaasai na migogoro juu ya
haki zao za ardhi na rasilmali, ni sharti Serikali iweke utaratibu mpya
utakaoruhusu Wamaasai kufaidika na rasilmali za wanyamapori katika maeneo yao
kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko ilivyo sasa. Kama inavyosema Taarifa ya Tume
ya Mwigulu Nchemba, kuwapatia wananchi wa Ngorongoro mgawo wa shilingi bilioni
moja wakati mapato ya Mamlaka ya Hifadhi ni zaidi ya shilingi bilioni 51 kwa
mwaka ni ‘dhihaka na kuwapuuza.’
Aidha, utaratibu wa uhifadhi
unaosisitiza binadamu na mifugo yao kuondolewa katika maeneo ambayo wameishi
pamoja na wanyamapori kwa karne nyingi hauna msingi wowote kisayansi na
umepitwa na wakati. Kama walivyowahi kusema watafiti Homewood na Rodgers katika
kitabu chao The Maasailand Ecology:
Pastoralist Development and Wildlife Conservation in Ngorongoro, Tanzania,
hakujawahi kuwa na sababu za msingi za kisayansi za kuwakataza wafugaji wa
Kimaasai kutumia rasilmali asili za Serengeti-Ngorongoro kwa ajili ya mifugo
yao. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kutoa kauli rasmi mbele
ya Bunge hili tukufu kama bado kuna sababu zozote za kuendelea kuwazuia
wafugaji wa Kimaasai wa Ngorongoro na Loliondo kutumia maeneo ya malisho ndani
ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo ya Kreta za Ngorongoro, Olmoti na
Empakaai na vile vile katika Hifadhi ya Msitu wa Nyanda za Juu za Kaskazini ili
kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa malisho na maji ya mifugo hasa hasa
wakati wa kiangazi.
LOLIONDO,
WAARABU NA CCM
Mheshimiwa Spika,
Mgogoro wa ardhi katika eneo la Loliondo
ni taswira nyingine ya jinsi ambavyo Serikali ya CCM imekiuka haki za wafugaji
wa Kimaasai kwa manufaa ya wawekezaji wa kigeni katika sekta ya uwindaji wa
kitalii. Kama tulivyoeleza mwanzoni, kufuatia Wamaasai kuondolewa Serengeti
mwaka 1959, baadhi yao walihamishiwa katika Tarafa za Loliondo na Sale na
wengine walihamishiwa katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. Licha ya ahadi za
Serikali ya kikoloni kwamba haki za ardhi za Wamaasai zitaendelea kulindwa
katika maeneo hayo, miaka ya uhuru ilishuhudia Serikali ya Tanzania ikianza
kuhujumu haki hizo. Hivyo basi, mwaka 1975 Serikali iliwaondoa kwa nguvu
wafugaji waliokuwa wakiishi ndani ya eneo la Kreta ya Ngorongoro. Miaka tisa
baadaye, kati ya 1983/84, Serikali ilitwaa eneo la Sukenya lenye ukubwa wa
ekari 10,716 na kuligawa kwa Kampuni ya Bia Tanzania (Tanzania Breweries Ltd.)
Aidha, mwaka 1990 Serikali ilipima vijiji vyote vya Tarafa ya Loliondo na Sale
na kuvipatia hati milki ya ardhi ikiwa ni pamoja na kuvitambua kisheria. Hata
hivyo, mwaka huo huo Serikali hiyo hiyo ilitwaa sehemu ya ardhi ya vijiji hivyo
na kuimilikisha kwa Kampuni ya Orthello Business Corporation (OBC) inayomiliwa
na Brigadia Mohamed Abdulrahim al-Ali anayesemekana kutoka katika familia ya
kifalme ya Oman. Mwaka 1992 Serikali hii ya CCM ilipanua “… wigo wa umiliki wa
ardhi wa kampuni ya OBC na kuiruhusu kampuni hiyo kuwinda katika vijiji vyote
19 vya Tarafa ya Sale na Loliondo.” Ilipofika mwaka 2003, “mkataba wa OBC na
Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya vijiji ukaisha lakini OBC ikaendelea
na uwindaji mpaka sasa.” Licha ya kampuni hiyo kutokuwa na mkataba halali na wananchi
wa Loliondo, mwaka 2009 “operation kubwa ilifanywa na Wizara ya Maliasili na
Utalii kuwaondoa wafugaji katika maeneo ya Sale na Loliondo na kupelekea
wananchi kuchomewa nyumba zao.” Na mwaka 2011 Serikali ya CCM “ikavitangazia
vijiji vyote kurudisha hati miliki za ardhi na pia vijiji vyenye vyeti vya
usajili vikaamriwa vivirudishe.” Inaelekea kwamba amri hii ilikuwa ni sehemu ya
mwisho ya maandalizi ya kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na Sale ardhi zao
kwani mnamo tarehe 26 Machi, 2013 Waziri wa Maliasili na Utalii aliitembelea
Wilaya ya Ngornognoro na kuwatangazia wananchi na wakazi wa Loliondo kwamba
“ameagizwa na Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho
Kikwete, kugawa eneo la Loliondo Game Controlled Area ya zamani katika sehemu
mbili: Yaani km2 2500 zimeachwa kwa ajili ya matumizi ya watu kwa
kilimo, ufugaji, makazi, etc.; km2 zimechukuliwa na Serikali … ili
eneo hilo liwe Game Control (sic!) mpya ya Loliondo.”
Mheshimiwa Spika,
Maelezo yote haya yanatoka katika Taarifa
ya Tume ya Mwigulu Nchemba. Kwa mujibu wa Taarifa hiyo, Serikali hii ya CCM “…
imeamua kumega … eneo la Loliondo Game Control (sic!) Area ya zamani na
kulifanya Game Control (sic!) Area mpya, na kwamba eneo hilo sasa litakuwa mali
ya mwekezaji OBC kwani analimiliki kisheria.” Aidha, kwa mujibu wa Taarifa
hiyo, endapo eneo hilo litamegwa kama ilivyotangazwa na Waziri Kagasheki, “… wakazi
wa Tarafa (ya Loliondo) watakuwa wamebakiwa na eneo la km2 265 tu.
Eneo hili ni dogo sana kwa wakazi 60,000 wa Tarafa hii.”
Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba
inasema wazi kwamba kauli ya Waziri Kagasheki kuhusu unyang’anyi huu wa wazi
wazi wa ardhi ya wananchi ndiyo ‘iliamsha hasira za wananchi.’ Hii ni kwa
sababu, “… eneo … wanalonyang’anywa ndilo eneo pekee wanalolitegemea kwa maji
ya mifugo na matumizi ya kibinadamu. Kuwaondoa ndani ya eneo hilo ni sawa na
kuwauwa. Hivyo wako tayari kufa wakipiginia eneo hilo.” Aidha, “… eneo hilo …
ndilo eneo pekee walilolitenga kwa ajili ya malisho ya mifugo hasa wakati wa
kiangazi panapokuwa na uhaba wa malisho. Kuwaondoa hapa ni sawa na kuiuwa
mifugo yao, jambo ambalo hawako tayari kulishuhudia, bora wafe.”
Mheshimiwa Spika,
Mgogoro kati ya wananchi wa Loliondo
na Sale kwa upande mmoja na Serikali na OBC kwa upande mwingine umekuwa
ukitokota kichini chini kwa zaidi ya miaka ishirini na tatu. Mgogoro huu ni
mali binafsi ya CCM na Serikali zake za awamu ya pili, ya tatu nay a nne ya
Dokta Kikwete. Ni mtoto wa ndoa haramu ya CCM na wawekezaji wa kigeni katika
sekta ya uwindaji wa kitalii. Mtoto alizaliwa na Serikali ya Rais Ali Hassan
Mwinyi, akalelewa na baba wa kufikia Rais Benjamin Mkapa na sasa amefikisha
umri wa mtu mzima chini ya baba wa kambo Dokta Jakaya Mrisho Kikwete!
Licha ya Serikali ya CCM kuwatukana
wananchi wa Loliondo kwa kuwaita Wakenya, ni wazi – kama inavyothibitishwa na
Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba - kwamba waathirika wa landgrab hii ni Watanzania wapatao 59,536 wanaoishi katika vijiji
vya Ololosokwan, Soit Sambu, Oloipiri, Oloirien/Magaiduru, Arash,
Losoito/Maaloni na Piyaya. Vijiji hivi vina shule za msingi na za sekondari
zenye wanafunzi 2,302; zahanati nne na nyumba kadhaa za wahudumu wa afya;
mashine za maji tatu; na mabwawa ya maji mawili. Maelfu ya wananchi hawa na
miundo mbinu iliyojengwa kwa nguvu zao na kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania
inatakiwa kutolewa kafara katika hekalu la urafiki wa Serikali ya CCM na
mwekezaji huyu wa Kiarabu! Huu ndio uso halisi wa Serikali hii sikivu na
inayotaka ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’!
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na hoja na ushahidi ambao
tumeueleza hapa, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM
itoe kauli rasmi mbele ya Bunge lako tukufu juu ya mambo yafuatayo:
1.
Kama kampuni ya OBC ina haki zozote za ardhi katika maeneo ya
Kata za Loliondo na Sale licha ya ukweli kwamba maeneo hayo yalikwishapimwa na
wananchi kumilikishwa kihalali, na vijiji vyao kupatiwa usajili halali kwa
mujibu wa sheria za nchi yetu;
2.
Kama ni halali kwa kampuni ya OBC kuendesha shughuli za
uwindaji wa kitalii katika vijiji vyote 19 vya Tarafa ya Loliondo na Sale
wakati eneo ililopewa kwa ajili mwaka 1990 lilihusu sehemu ndogo tu ya maeneo
ya vijiji hivyo;
3.
Kama kampuni ya OBC inaendesha shughuli za uwindaji wa
kitalii katika maeneo ya Loliondo kihalali licha ya ukweli kwamba mkataba wake
na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa niaba ya wananchi wa Loliondo ulikwisha
muda tangu mwaka 2003;
4.
Kama ilikuwa halali kwa Serikali kuwahamisha wananchi wa
Loliondo kwa nguvu na kuwachomea nyumba zao moto mwaka 2009, na baadaye kudai
wananchi hao ni raia wa Kenya. Kama Serikali hii ya CCM itakiri kwamba vitendo
hivyo vya kinyama havikuwa halali, basi itoe kauli kama iko tayari kuwaomba
radhi na kuwalipa fidia kwa mujibu wa sheria za nchi yetu wananchi wote wa
Loliondo na Sale waliodhalilishwa kwa kuitwa raia wa Kenya na kuathirika na
unyama huo;
5.
Kama Serikali hii ya CCM iko tayari kuwachukulia hatua za
kisheria, au kiutendaji au kinidhamu wale wote walioamuru na au kushiriki
katika vitendo vya kuwaondoa kwa nguvu wananchi wa Loliondo na Sale na
kuwachomea nyumba zao moto pamoja na kuwatendea vitendo vya udhalilishaji au
ukiukaji wa haki zao za kibinadamu;
6.
Kama ni kweli kwamba kitendo cha hivi karibuni cha Waziri
Kagasheki kutoa amri ya wananchi wa Loliondo na Sale kunyang’anywa maeneo yao
mengine na maeneo hayo kukabidhiwa kwa kampuni ya OBC kilitokana na maagizo au
maelekezo ya Mh. Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete au yalikuwa na Baraka zake
kama inavyodaiwa na Taarifa ya Tume ya Mwigulu Nchemba;
7.
Kama huu sio wakati muafaka kwa Waziri Kagasheki kuwajibika
kwa kujiuzulu kwa hiari yake au, kama atashindwa kufanya hivyo, kuwajibishwa
kwa kufukuzwa kazi kwa kusababisha mgogoro wa sasa katika maeneo ya Loliondo na
Sale;
8.
Kama, licha ya ushahidi wote ulioibuliwa na Taarifa ya Tume
ya Mwigulu Nchemba na licha ya upinzani mkubwa wa wananchi, bado kuna sababu ya
kuendelea kuiruhusu kampuni ya OBC kuendesha shughuli zake katika maeneo ya
Loliondo na Sale;
9.
Kama, licha ya ushahidi wote ulioibuliwa na Taarifa ya Tume
ya Mwigulu Nchemba kwamba chanzo cha migogoro ya ardhi katika Wilaya ya
Ngorongoro ni sera za Serikali hii ya CCM, ni halali kwa Serikali na CCM yenyewe
kuendelea kuyalaumu mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya kutetea haki za
binadamu na za wafugaji wa Kimaasai kuwa yanachochea vurugu za wananchi wa
Loliondo na Ngorongoro;
10.
Kama, baada ya mambo yote yaliyoeleza hapa, Serikali hii ya
CCM iko tayari kusitisha uamuzi wake wa kuwanyang’anya wananchi wa Loliondo na
Sale maeneo yao na kuyamilikisha kwa kampuni ya OBC au kampuni nyingine yoyote
katika siku za mbeleni;
Kama alivyopata kusema Dalai Lama: “Lengo
letu kuu katika maisha haya ni kuwasaidia watu wengine. Na kama hatuwezi
kuwasaidia, basi angalau tusiwaumize.” Serikali hii ya CCM ilikuwa na bado ina
wajibu kisheria kuwasaidia Wamaasai wa Wilaya ya Ngorongoro kwa kuwaendeleza
kiuchumi na kijamii. Kama imeshindwa kufanya hivyo, kama ilivyoonyeshwa katika Maoni
haya, basi Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM angalau
iache kuwaumiza wananchi hawa kwa kuwaachia ardhi zao!
UJANGILI
Mheshimiwa Spika,
Madhara makubwa
ya ujangili inawezekana kwa kiasi kikubwa yanasababishwa na mfumo wa kiuwajibikaji
ambao hauko wazi, kwani mtu anayetoa vibali au anayejua ni mnyama gani
anatakiwa kuwindwa ni Afisa wanyamapori wa Wilaya(DGO), ambaye kiuwajibikaji
yupo chini ya Mkurugenzi wa halmashauri. Taasisi inayowajibika kwa wanyamapori
ni Wizara ya Maliasili na Utalii, tunaweza kuona mfumo ulivyo na nani anatakiwa
kuwajibika kwa nani na mazingira gani wanafanyiakazi na wawindaji wanauzito
gani kifedha.
Mheshimiwa Spika,
Ujangili pia
unazidishwa na kutokuwepo kwa askari wa kutosha. Kwa mujibu wa taarifa ya
Waziri hapa Bungeni, “... Idara ya Wanyamapori inasimamia Game Reserves 28, inasimamia
Game Controlled Areas zaidi ya 40, kwa ujumla inasimamia maeneo yenye zaidi ya
kilomita za mraba laki mbili. Vigezo vya
Kimataifa kwa ajili ya ulinzi peke yake vinasema kwamba Askari mmoja wa
wanyamapori anapaswa alinde eneo lisilozidi kilomita za mraba 25. Kwa hiyo, kwa kilomita za mraba laki mbili
unajikuta kwamba Askari tuliopaswa kuwa nao karibia Askari 8,400. Hivi tunavyozungumza Askari tulionao hawafiki
1,700 kwa Tanzania nzima.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa tafsiri
ni kwamba ni rahisi kwa askari waliopo kukaa kwa muda mrefu katika eneo moja na
matokeo yake ni kuwapa majangili ratiba nzima ya mfumo wa ulinzi na mienendo ya
wanyama. Kwa mfano hifadhi nzima ya Katavi ina wafanyakazi 45 tu, eneo lake ni
karibu ha.10,000. Eneo hilo halina mawasiliano ya aina yoyote na ratiba ya
tembo kutoka eneo moja kwenda lingine inajulikana kwa majangili. Hapa ni
dhahiri kuwa mauaji ya tembo yanayofanyika ushiriki wa watendaji hauwezi kuepukwa?
Ujangili na
silaha za Kivita
Mheshimiwa
Spika,
Kumekuwepo na malalamiko mengi toka
kwa watendaji kuwa majangili wanatumia silaha za kivita katika kutimiza azma
yao. Kambi Rasmi ya Upinzani inaliona hili kuwa ni jambo la kimtandao zaidi.
Kwani tunaamini kuwa taasisi zenye uwezo wa umiliki wa silaha hizo ni jeshi la
polisi na jeshi la wananchi.
Mheshimiwa
Spika,
Upatikanaji wa silaha hizo kwa
majangili ni lazima kuwe na uhusiano wa moja kwa moja na baadhi ya watendaji
katika majeshi hayo mawili. Hili linazidisha hofu kutokana na ukweli kwamba
tembo wanazidi kuuawa na TANAPA hawana silaha za kukabiliana nazo, silaha
zilizoagizwa zimezuiwa kwa ajili ya kulipiwa ushuru, na hilo linawezekana ni
kosa la maksudi la kimtandao ili kukwamisha upatikanaji wa silaha za
kukabiliana na ujangili. Utaratibu wa kuagiza silaha unajulikana kuwa jeshi
ndilo lenye jukumu hilo.
Mheshimiwa Spika,
Mtandao wa ujangili ni mkubwa sana
kwani upo katika uuaji, usafirishaji, masoko, polisi, TRA na mahakama.
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya mahakimu wa mahakama za wilaya katika mikoa
ya Mara, Simiyu, Shinyanga,Katavi na Kigoma ni sehemu ya mtandao huo kwani
watuhumiwa wengi wanaokamatwa na nyara zikiwemo silaha hupewa dhamana na
hawarudi mahakamani. Mfano, mtuhumiwa aliyekamatwa kwa tuhuma za kuwinda faru,
nyani na ngiri ndani ya hifadhi ya serengeti mwaka 2010, madubu Masunga Dusara
(33) mkazi wa Ng'walali haonekani mahakamani baada ya hakimu mkazi wa mahakama
ya shinyanga, Lydia Ilunda kumpa dhamana
kwa masharti nafuu.
Kambi rasmi ya upinzani inaitaka
serikali itoe taarifa kwanini wale waliotajwa katika ripoti ya ujangili
wameweza kupewa nafasi kubwa ya uongozi wa nchi hii? Biashara ya pembe za ndovu
inamilikiwa na nani? Usafirishaji wa pembe hizo na nyaraka nyingine unaratibiwa
na magenge gani katika bandari na viwanja vya ndege? Ni kwa kiasi gani vyombo
vya serikali kama jeshi la Polisi, usalama wa taifa na mamlaka ya mapato nchini
(TRA) vinahusika?
Mheshimiwa Spika,
Mwezi Desemba shehena yenye tani 1.3
ya meno ya Tembo iliyofichwa kwenye magunia ya Alizeti ilikamatwa na Maafisa wa
Forodha wa HongKong, Shehena hii ilikuwa na thamani ya dola za kimarekani
milioni moja na nusu, pia wiki mbili kabla ya hapo takribani tani nne za meno
ya Tembo zilikamatwa huko huko Hong Kong. Kwa matukio haya mawili, hawa ni sawa
na Tembo 900 waliouwawa. Aidha, katika mwezi Desemba 2012 Polisi mkoani Arusha
walikamata nyara nyingi za Serikali katika eneo la Kisongo, zikiwemo ngozi za
Simba na wanyama wengine, pembe za ndovu na wanyama wengine na vichwa vya
wanyama. Nyara hizi zilikuwa tayari kwa kuuzwa nje ya Nchi, vivyo hivyo mkoani
Katavi walikamatwa majangili kadhaa na kuachiwa huru kwa amri kutoka juu kwa
mujibu wa taarifa za maafisa wa wanyama pori.
Mheshimiwa
Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
katika mjadala wa makadirio ya bajeti ya mwaka 2012/2013 ilizungumza sana juu
ya hali tete iliyopo katika usalama wa wanyamapori kwa ushahidi wa kutosha ili
kuweza kuisaidia serikali katika kulinda rasilimali asili ya wanyamapori kambi
rasmi ya upinzani ilichoambulia kwa serikali ni kubezwa na kudhalilishwa na sio
kupokea maoni yetu na kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika,
Wakati hivi karibuni nchini Kenya
watetezi wa hifadhi waliishinikiza serikali kuanzisha sheria kali dhidi ya
ujangili ili kuwepo na adhabu stahiki, pili idara ya wanyamapori ya kenya (KWS)
na wahifadhi maliasili kutangaza teknolojia mpya ambayo itasaidia kupambana na
ujangili kama ilivyotangazwa na Daily
Nation ya tarehe 26 March 2013, na tatu serikali ya Kenya kuongeza askari
zaidi ya 1,000 ili kukabiliana na ujangili, haya yote yakifanyika Kenya
kukabiliana na ujangili, Serikali ya Tanzania inaendelea kulinda majangili
ambao taarifa zao zimekuwa zikizifikia mamlaka zilizo chini ya serikali.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya upinzani bungeni inapenda kutoa rai kwa
serikali, pamoja na kejeli na udhalilishaji kwa kambi yetu ya kuashiria kuwa na
chuki ya wazi na CHADEMA, hili halina tija kwa wananchi waliowachagua, ni vema
wakarejea kuwa na uzalendo kwa nchi yetu na kuona umuhimu wa kulinda rasilimali
zetu na kuwafanya watanzania wanufaike na rasilimali hizo.
Mheshimiwa Spika, kutokana na taarifa za kanzidata ya mfumo wa taarifa za
biashara ya tembo, Elephant Trade Information System (ETIS) kwa kipindi cha
mwaka 2002 hadi 2012, Tanzania katika matukio ya kukamatwa kwa shehena za pembe
za ndovu kwa matukio 23 sawa na asilimia 28% ya shehena zote kubwa duniani, kwa
takwimu hizo imethibitika kuwepo mauaji ya tembo 24,000 kwa shehena
zilizokamatwa za pembe za ndovu, hivyo Tanzania kuwa ni nchi inayotoa pembe za
ndovu kwa wingi duniani.
Mheshimkiwa Spika, kwa mwaka 2012 tu
shehena zilizokamatwa nchini Hong Kong zenye uzito wa kilo 1,330 pia kwa
mfululizo kuwepo kwa shehena zilizokamatwa kwa nyakati tofauti nchini Vietnam
kilo 6,232 mwezi March 2009 na 2005. 6
mwezi August, pia nchini Ufilipino (Philippines) kilo 3,346, mwaka 2011,
Malaysia, na nchi nyingine duniani, kwa matukio haya baadhi na kutokuwepo kwa
hatua zozote zinazochukuliwa ni dhahiri Dola imekuwa ni mhusika mkubwa wa
kulinda tatizo hili la ujangili na hivyo kuendelea kuwa na walakini na
kutokuhusika kwa dola kuchochea tatizo la ujangili kuendelea kuwa kubwa.
Mheshimiwa Spika, ni matarajio hasi kwa nchi kwa takribani miaka saba ijayo
Tanzania itakuwa na historia ya kuwa na akiba ya tembo, ikiwa tafiti za
mwenendo wa mauaji ya tembo kuonesha kukua na kuashiria mauaji kufikia 10,950
kwa mwaka huu wa 2013, ni dhahiri juhudi za kutokomeza ujangili zilizopo
zitatufikisha mwaka 2020 tukiwa hatuna akiba ya tembo hata mmoja tena.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inapenda kutoa rai kwa serikali kama ilivyotoa katika hotuba
ya bajeti ya mwaka jana, kwamba kuna haja ya kuangalia upya mfumo mzima wa
ulinzi wa wanyamapori kama kweli serikali inayo nia ya dhati ya kukabiliana na
taizo la ujangili nchini.
Kwanza Mheshimiwa Spika, kabla ya
kuanza kuchukua hatua dhidi ya tatizo la ujangili kwa nia ya kizalendo kwa
nchi, ni vema sasa serikali ikaanza
kujitathmini yenyewe na viongozi ndani ya serikali na chama cha mapinduzi juu
ya tuhuma zilizopo kwa viongozi wake kuhusishwa na ujangili ili kuweza kutoka
nje kwa ujasili kushughulikia tatizo hilo baada ya kuwajibisha viongozi
wahusika na kuacha watendaji na viongozi safi ndani ya serikali na chama
watakao shughulikia pasipo kuwa na haya.
Mheshimiwa Spika, pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali kuona
umuhimu wa kurejea sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009 kifungu cha 103
kinachohusu adhabu kwa makosa ya
yanayohusu umiliki wa silaha zinazotumiwa na shughuli za ujangili kuifanyia
marekebisho ili adhabu kali zaidi zitolewe kuliko sheria inavyosema kwa sasa.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani
bungeni pia inaitaka serikali kushirikisha wadau wa ulinzi hususani jeshi la
Wananchi (JWTZ) kushiriki katika ulinzi wa wanyamapori kutokana na mamlaka za
hifadhi na jeshi la polisi kuzidiwa nguvu na mitandao ya ujangili ambayo
imekuwa ikitumia silaha kubwa za kivita katika shughuli za ujangili.
SEKTA NDOGO
YA WANYAMAPORI
Mheshimiwa Spika,
Shoroba (corridor za wanyama –Mapitio ya Wanyama) zote za wanyama
nilazima zilindwe kikamilifu, hii ni kutokana na ukweli kuwa wanyama huwa
wanaendelea kupita njia ile ile wakati wote wa maisha yao na katika mapito hayo
ndio pia hupata muda wa kuzaliana. Mbali na hilo ni pia katika shoroba hizo majangili
ndipo hutumia mwanya huo kuwaua. Aidha, pamoja na umuhimu wa Shoroba hizi za
wanyama serikali imekuwa ya kwanza kuziharibu na mfano ni ushoroba uliopo
Mvomero ambako yalikuwa ni mapito ya Tembo serikali imejenga jengo la Mkuu wa
Wilaya na Halmashauri kwenye eneo hilo,
na ni hivi majuzi tu Tembo aliyekuwa anapita eneo hilo iliamriwa auwawe
na maaskari wa wanyama pori baada ya kukwama njiani kutokana na kukosa njia
eneo hilo, pia upo mfano wa shoroba iliyopo kati ya Tarangire na Manyara
inayopitia njia ya Mijingu nayo imevamiwa na kaya za watu wasiozidi 22 na
kufunga njia hiyo.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali ambayo inasema kuwa
inahifadhi uhalisia wa mazalia ya wanyamapori wetu, inakuwaje wataalam wetu na
Serikali badala ya kulinda wanakuwa ndio waharibifu wakubwa? Hifadhi ya Taifa Rubondo
ni hifadhi ambayo ni Kisiwa kinachoundwa na visiwa tisa vidogo vidogo ambapo
kisiwa hiki cha Rubondo ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana Samaki
wakiwemo Sato na Sangara wenye ukubwa wa uzito wa kilo hadi 100. Wanyama
wanaopatikana katika hifadhi hiyo ni pamoja na Viboko,Pongo, Nzohe, Fisi maji,
Mamba na Pimbi, wanabadilishana makazi na wanyama wengine waliohamishiwa katika
hifadhi hii kama Sokwe, Tembo, Mbega weusi na weupe na Twiga.
Mheshimiwa Spika,
Kukosekana kwa shoroba za kuwafanya
wanyama waweze kutoka na kurudi katika hifadhi ni tatizo kubwa kijenetik, kutokana na utafiti
uliofanyika unaonyesha kuwa kitendo cha wanyama kukaa eneo moja kwa muda mrefu
na kuzaliana wenyewe kwa wenyewe kunaweza kuadhiri wanyama hao. Hili linatokana
na ukweli wa kibailojia kuwa uzaliano wa kindugu (In breeding) una madhara
makubwa kwa jamii kwani kama kwenye familia ina magonjwa ni dhahiri kuwa
familia nzima itakuwa na magonjwa hayo na vivyo hivyo, kwa hifadhi ambazo
wanyama wake wametengwa na kufungiwa sehemu moja. Hii ni hatari kwa muendelezo
mahiri wa hifadhi hiyo.
TAASISI YA UTAFITI WA WANYAMAPORI-TAWIRI
Mheshimiwa Spika,
Uwekezaji katika tafiti umeendelea kuwa ni vigumu kwa serikali
yetu hususani katika sekta ya wanyamapori kutokana na kutokuwa moja ya
vipaumbele vya serikali, na hii ni kutokana na dhana ya serikali kutotambua
umuhimu wa rasilimali hizi kwa maendeleo ya uchumi wa nchi,taasisi ya utafiti
wa wanyamapori ambayo ni TAWIRI na inafanyakazi zake lakini kutokana na
kutokupatiwa fedha za kutosha za kufanya tafiti zake kwenye sekta ya
wanyamapori kumepelekea taarifa muhimu na za maana kutokupatikana hapa kwetu
kwa maendeleo ya sekta ya wanyamapori, badala yake tafiti muhimu kwenye sekta
hii zinafanyika kwa ufadhili toka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inasema kuwa huu ni udhaifu kwa nchi
ambayo inapata mapato mengi kupitia sekta hii na kutowekeza zaidi katika
utafiti wa sekta hii, kwa mfano kwa mwaka wa fedha 2011/2012 makusanyo sekta wanyamapori yalikuwa kiasi cha shilingi 15,074,053,972.10
na kwa mwaka wa fedha 2012/2013 makisio yalikuwa shilingi 25,175,381,917.00
Hizi ni fedha nyingi kwa sekta ambayo uwekezaji katika sekta hiyo ni karibia na
hakuna, kuna haja ya serikali kuona umuhimu wa kujitathmini zaidi na kuona ni
muhimu zaidi kwa maendeleo ya sekta ya wanyamapori kuwa na fungu maalumu kwa
ajili ya kuwezesha tafiti mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
Kuna taasisi ambayo imepewa dhamana ya kuratibu na kuwezesha tafiti
mbalimbali hapa nchini ambayo ni COSTECH, lakini cha ajabu ni kwamba taasisi
hii imekuwa haitoi kipaumbele kwa watafiti ambao wanafanya utafiti kwenye sekta
hii ya wanyama na badala yake utafiti unaegemea sana fedha za mashirika ya nje
ambayo yanakuwa na haki zote za tafiti husika. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka
Serikali kuweka vipaumbele kwa kuangalia mchango wa sekta kwenye uchumi husika
ambako tafiti zitafanyika.
MAHUSIANO
KATI YA TANAPA NA JAMII ZINAZOZUNGUKA MBUGA
Mheshimiwa Spika,
Wananchi wanaozunguka Mbunga za
hifadhi ndio wenye jukumu kubwa la kuhakikisha ulinzi wa wanyama. Hivyo basi,
mahusiano kati ya Mbuga na wananchi ni muhimu sana. Mipaka ya hifadhi
iliyowekwa miaka hiyo wakati idadi ya wananchi katika vijiji mbalimbali ilikuwa
ni ndogo na hivyo mipaka ya hifadhi ilikuwa ndani ya vijiji na shughuli za
vijiji hazikuwa na madhara katika hifadhi hizo. Kutokana na kuongezeka kwa
idadi ya wananchi katika maeneo hayo na shughuli zao za kiuchumi kuwa kubwa na
hivyo kupelekea maeneo ya hifadhi kutumiwa.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha uhifadhi wa wanyama wetu unaendelea
vyema, ni lazima ushirikishwaji wa wananchi katika zoezi lolote la kuweka
mipaka ya hifadhi au kuchukua mipaka iliyokuwepo miaka ya sitini ni muhimu, pia
ni bora kuangalia kama nchi tuangalie jukumu letu la msingi ni nini kati ya
kulinda raia wake au kulinda wanyama?
Mheshimiwa Spika, Mbuga ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha inapakana na jamii kubwa
na kwa sasa kuna mgogoro wa ardhi baina ya TANAPA na wananchi wa Ruaha kwa kuwanyang’anya
ardhi yao hasa kwenye kata ya Rwembe, na hivyo kuwafanya wananchi kushindwa
kufanya shughuli za maendeleo kama vile kilimo na wakati hawana njia nyingine
ya kupata kipato chao cha kijikimu.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kutoa kauli
kuhusiana na madhira haya wanayopata wananchi wa kata ya Rwembe ambao vijiji
vyake vinne wamezuiliwa wasifanye shughuli yoyote ya maendeleo na uongozi wa
TANAPA.
I: USHIRIKISHWAJI WA JAMII
KATIKA UHIFADHI WA WANYAMAPORI NA MALIASILI (WILDLIFE MANAGEMENT AREAS-WMA).
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa jamii zinashiriki na kunufaika na
maliasili zetu hasa wanyamapori na kukuza uhifadhi wa wanyamapori nje na maeneo
ya makazi yao hivyo kuanzisha Maeneo ya Jumuiya ya Usimamizi Wanyamapori (WMA).
Kazi kuu za WMA ili kuwa ni kuhamishia usimamizi wa Maeneo ya Jumuiya ya
Usimamizi Wanyamapori kwa wananchi vijijini na hivyo basi kuulinda ushoroba wa
wanyama, njia za uhamaji, maeneo ya usalama wa wanyama, na kuhakikisha kwamba
jamii zilizo katika maeneo hayo ya wanyama zinafaidika vilivyo kutokana na
uhifadhi wanyamapori. Kuzuia matumizi
haramu ya wanyamapori nchini kote kwa kuchukua hatua endelevu za usimamizi,
ulinzi na kutekeleza sheria.
Mheshimiwa Spika, kitendo chochote kitakachofanyika cha kuzifanya hizi WMA
kushindwa kufaidika na uwekezaji wa wananchi katika hilo ni hujuma kwa na
wananchi na kinapelekea wananchi badala ya kuwa wasimamizi wanakuwa wahujumu.
Mheshimiwa Spika, MBOMIPA ni
kifupi cha chenye maana ya – matumizi bora maliasili IDODI na PAWAGA ina undwa
na vijiji 21 kama wanachama waanzilishi. Vijiji vyote vipo katika Tarafa za
Idodi na Pawaga Wilaya ya Iringa. ilianzishwa mwaka 1998 iko Mashariki ya
Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Asasi ya MBOMIPA inasimamia eneo lenye ukubwa wa km za
mraba 773. Eneo hili lina aina na idadi kubwa ya wanyama wakubwa, wadogo, ndege
na madhari nzuri ya kuvutia kandokando ya mto Ruaha ambao ndio Mpaka na Hifadhi
ya Taifa ya Ruaha.
Mheshimiwa Spika, matatizo
yanayoikumba asasi hii ya WMA yanaakisi asasi zingine za uhifadhi za wananchi.
MBOMIPA ilipata mwekezaji tangu mwaka 2008 anayeitwa Kilombero North Safari
(KNS) kwaajili ya ujenzi wa hoteli na lodges za kitalii. Mwekezaji huyu
hajajenga hoteli yoyote hadi sasa na amekuwa akiwadanganya wananchi na Jumuiya
juu ya ujenzi wa hoteli kulingana na makubaliano na MBOMIPA. Mwekezaji huyu pia amekuwa akilazimisha
kufanya shughuli ya Uwindaji kwenye kanda hiyo na kukiuka sheria ya uwindaji na
Resource Zone Management Plan (RZMP) ambayo imepitishwa na MBOMIPA kwa mujibu
wa sheria.
Mheshimiwa Spika, Ujangili ni
mkubwa sana hasa wa tembo kwenye kanda ambayo inasimamiwa na Mwekezaji huyu, na
hata tarehe 20 na 21 April 2013 wameuwawa tembo 4 wakubwa karibu kabisa na
kambi ya mwekezaji (KNS) na meno yote kuchukuliwa na Majangili. Hili suala linajulikana kwa watendaji karibu
wote wa Serikali, hii inatokana na maslahi na mahusiano binafsi kati ya
wahusika na wamiliki wa Kilombero North Safari. Taarifa zilizopo ni kwamba,
kampuni ya kilombero hunting ina wanahisa ambao baadhi yao ni wajumbe wa bodi
ya asasi ya MBOMIPA ambao pia ni wafanyabiashara wawili maarufu iringa, mbunge
mmoja na mfanya biashara maarufu nchini ambaye mdogo wake ACRAM AZIZ ni msimazi
wa karibu kwa niaba ya kaka yake. Hii ndiyo siri ya ubabe wa kampuni ya
kilombero North safari katika eneo la LUNDA ndani ya eneo la MBOMIPA.
Mheshimiwa Spika, Usimamizi wa
eneo la Asasi ya MBOMIPA unakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na vitendo
vya rushwa vinavyofanywa na kampuni zinazotaka kupata maeneo ya uwindaji hasa
KAMPUNI YA KILOMBERO HUNTING SAFARI na nyingine ambayo inatoa rushwa kwa baadhi
ya wajumbe wa bodi ya MBOMIPA, Afisa wanyamapori (W) Iringa, baadhi ya Viongozi
wa Vijiji na Wajumbe wa Vijiji kwenye Asasi.
Mheshimiwa Spika, Kiini cha
Mgogoro na migongano inayotokea kwenye eneo la asasi linasababishwa na maslahi
ya Wawindaji na siyo suala la Uhifadhi endelevu wa eneo husika. Kwa kuwa lengo
ni Uhifadhi wa Wanyama pori na mazingira yao, mgogoro huo utaisha pale tu
ambapo jumuiya hii itaondokana na kuachana kabisa na shughuli za uwindaji
katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inasema kuwa, eneo la MBOMIPA kuendelezwa kwa shughuli za Utalii wa
Picha ambazo ni endelevu, na ipige marufuku shughuli zote za uwindaji. Aidha
ifanye ukaguzi maalum kwa WMA hiyo ili kubaini mwenendo wa asasi hiyo kama
unazungatia maslahi mapana na uanzishwaji wake hatua za haraka zichukuliwe ili
kunusu raslimali za nchi kuishia kwenye mifuko ya wahujumu uchumi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kutoa taarifa ni kwa kiasi gani makubaliano kati ya
WMA na kampuni ya Kilombero North Safari yametekelezwa kwa kiwango gani?
UKUSANYAJI
WA MADUHULI
Mheshimiwa Spika, katika ukusanyaji wa maduhuli ndani ya idara mbalimbali
kumekuwepo na baadhi ya takwimu zinazoashiria ubadhirifu wa rasilimali za umma
kwa kuzingatia viwango vinavyotajwa kwenye makadirio ya makusanyo,ukisoma
katika randama ya wizara iliyowasilishwa ndani kamati, kifungu namba 1001-idara
ya utawala na usimamizi wa rasilimali watu kinatoa kiasi cha fedha
zinazotarajiwa kukusanywa kutokana na vyanzo vya mapato kwa mwaka 2013/2014.
Mheshimiwa Spika,kwa mfano taarifa
inaonesha makusanyo katika mauzo ya vifaa chakavu ni shilingi 1,000 (Elfu
moja)mapato yatokananyo na mauzo ya vifaa sh 1,000 (Elfu moja),Masurufu ambayo
hayajarejeshwa sh 1,000 (Elfu moja) pia katika kifungu cha 2001 mapato mengine
sh 1,000 (Elfu moja) kwa kutokuwa makini na watendaji wa wizara na kutumia
mbinu chafu kuiba rasilimali za umma kwa kuweka viwango vidogo vya makadirio ya
ukusanyaji huku takwimu hizi kutokuakisi uhalisia ni dhahiri taifa litaendelea
kutafunwa na baadhi ya watendaji wasio waamininfu.
Mheshimiwa Spika, kwa akili ya
kawaida wizara haiwezi kufanya kazi ya kukusanya shilingi elfu moja kwa mwaka
mzima na huu ni mfano wa maeneo machache kwa kuonesha tabia hii kukithiri ndani
ya serikali kwa wahujumu na kujificha katika mgongo wa serikali kutopata mapato
ya kutosha huku mapato yakipatikana kwa kiwango kikubwa na bila taarifa zake
kuwekwa wazi.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka serikali kutolea ufafanuzi hujuma hii inayofanywa na
watendaji na ni kwa vipi wizara inadhibiti taarifa za makadirio ya maduhuli kwa
kuhakiki ili ziwe na uhalisia zaidi
kuliko hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha
mwaka 2012 serikali imeendelea kutoa vibali vya kuendelea na uwindaji kwa kampuni zilizokuwa na malimbikizo ya
madeni, mfano kampuni saba za uwindaji: M/S Malagarasi Hunting Safaris,
Mwanahuta & Company Limited, Usangu Ltd, Rana Tours & Safaris Ltd,Coastal
Wilderness (T) Ltd, Kilimanjaro Game Trails Ltd na Said Kawawa Hunting Company
Ltd kampuni hizi kwa jumla
zikidaiwa na wizara jumla ya dola za kimarekani 973,493.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka serikali kutoa maelezo ya kina juu ya sababu za kutoa vibali
pamoja na kampuni hizi kushindwa kulipa maduhuli kwa wakati na kuendelea
kuruhusiwa kufanya shughuli za uwindaji.
Mheshimiwa Spika, pia wawindaji
halali waliopewa leseni wamekuwa wakifanya shughuli za uwindaji na kufikia
mwisho wa mwaka 2012 bado serikali haikukusanya maduhuli yenye jumla ya dola za
kimarekani 216,000 na kuisababishia hasara serikali, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inachelea kulithibitishia bunge kuwa ni vitendo vya rushwa
vinavyoifanya serikali ikose mapato na mapato hayo kuingia mifukoni mwa
watumishi wasio waaminifu ndani ya
wizara, hivyo basi Serikali itoe ufafanuzi wa kina nini tafsiri yake
kama siyo ruhusa?.
SEKTA NDOGO YA UTALII
Mheshimiwa Spika, Taarifa za upotevu
wa mapato ya serikali imeendelea kuonekana katika sekta ya utalii kupitia ada
ya Utalii isiyokusanywa, Dola za Kimarekani 158,000 kwa mujibu wa Kanuni Na. 4
ya Kanuni za Utalii (ada na tozo) za mwaka 2009 inaeleza kuwa “ada ya leseni kwa kila daraja italipwa kila
mwaka kwa kiasi ambacho kimeainishwa katika Jedwali la Pili la Kanuni hizo”.
Mapitio ya makusanyo ya mapato yatokanayo na Leseni za Uendeshaji wa Huduma za
Utalii katika Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2011/2012
yameonyesha kuwepo kwa Kampuni zilizojiingiza kwenye biashara ya kutoa huduma
ya utalii lakini hawajalipa ada ya Leseni za Utalii yenye jumla ya Dola za
Kimarekani 158,000.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
mpango wa maendeleo wa miaka mitano, malengo ya kiutendaji ni kuboresha mfumo
wa makusanyo ya mapato yatokanayo na shughuli za utalii. Kambi ya Upinzani
inauliza kama mambo yaliyowazi ya ukusanyaji yanashindikana, huo mfumo
utaboreshwa vipi wakati hujuma inafanywa kwa ushirika na watendaji?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka serikali kutoa maelezo ya kina ni kwa jinsi gani
imehakiki ili kutorudiwa kwa matatizo haya ya kupoteza mapato. Aidha, Kambi
Rasmi ya Upinzani inaishauri serikali kuchukua hatua kwa watendaji
wasiozingatia sheria na kanuni katika kutimiza majukumu yao maana utaratibu huu
ni hujuma inayofanywa na wafanyabiashara na watendaji wasio waaminifu kwa umma.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
mpango wa maendeleo, unaonyesha kuwa kwa mwaka huu wa fedha uwekezaji kwenye
sekta ya utalii ni shilingi bilioni 43.968 wakati kitabu cha bajeti fedha zilizotengwa za maendeleo katika sekta
ya utalii inaonyesha shilingi bilioni 1 tu sawa na asilimia 2.2 tu ya fedha
zilizotengwa kwenye mpango wa maendeleo wa miaka mitano. Kambi Rasmi ya
Upinzani inaitaka Serikali kueleza kwa nini hili limekuwa hivi? Na nini tafsiri
ya kuwa na mapango wa maendeleo wa taifa kama hatuwezi kuutekeleza? ni kweli sekta hii itaweza kuwa shindani na
wenzetu katika jumuiya ya Afrika ya Mashariki au tupo tukisubiri miujiza? Kama
si dharau kwa ofisi ya rais idara ya mipango
ni nini hiki?
L: SEKTA NDOGO YA MISITU NA NYUKI
Misitu
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa
kitabu cha Transforming the informal Sector, How to overcome the Challenges
(ESAURP) kinaainisha takwimu za ukubwa wa eneo la misitu Tanzania ikiwa ni
hekta million 33.5 za misitu ambayo ni sawa na asilimia 38% ya eneo la ardhi
yote nchini,pia kinaainisha mchango mkubwa unaoweza tolewa na sekta ya misitu
katika uchumi kwa kuirasimisha sekta hiyo kuweza kuweka mazingira bora ya ajira
kwa wananchi ikizingatiwa shughuli za misitu ni moja ya chanzo kikubwa cha
kipato kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Spika, na kwa mujibu wa
taarifa za TRAFFIC 2007 zinaanisha kuwa ni asilimia 4 tu ya mazo ya misitu
huvunwa kihalali na asilimia 96 huvunwa bila kupata vibali rasmi na serikali
kukosa mapato kwa uvunaji mkubwa unaofanywa kutokana na kutorasimisha biashara
ya mazao ya misitu na kuwa na utaratibu ulio rasmi wa kufuatailia uvunaji wa
mazao haya ya misitu, Kambi rasmi ya Upinzani bungeni inaitakla serikali kuona
umuhimu wa kuona aslimia kubwa ya wananchi wanaotegemea bidhaa za misitu
kuendesha maisha yao kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, katika hizo
asilimia 96 ambazo huvunwa bila ya kupata kibali, kuna miti ambayo inavunwa kwa
ajili ya uchomaji wa mkaa, kwa mujibu wa tafiti zilizokwishafanyika, sekta ya
mkaa huingiza zaidi ya dola milioni mia sita na hamsini sawa na zaidi ya
shilingi trilioni moja kwa mwaka na kuajiri mamilioni ya watanzania hususani
waishio vijijini. Ni wazi kuwa sekta hii imeachwa bila mikakati na sheria
unganifu. Kama nilivyoeleza kwa kina katika hotuba yangu ya wizara ya
mazingira, Tanzania tunapaswa kujifunza kutoka Brazil ambayo inazalisha mkaa
asilimia 11% na Tanzania pekee
inazalisha asilimia 3% ya mkaa wote unaozalishwa duniani. Sekta hii
ikiwekewa mikakati mizuri ya makusudi itaweza kuzalisha mikaa kwa njia ya
kisasa huku ikipunguza hewa ya ukaa na kuifanya sekta hii kuwa endelevu.
Mheshimiwa Spika, Brazil huzalisha
asilimia 11% ya mkaa wote unaozalishwa duniani. Kwenye miaka ya 1990 asilimia
60.3% ya uzalishaji wa mkaa Brazil ulifanywa kutoka kwenye uvunwaji wa misitu
ya asili baadaye mkakati wa makusudi ulifanywa ili mkaa uzalishwe kutoka katika
misitu ya kupandwa. Ingawa matumizi ya mkaa nchini Brazil ni kwa ajili ya
viwanda vya kufua chuma. Jambo la msingi ni kwamba uvunaji wa mkaa kwa misitu
asili ilipungua kwa asilimia 82% kati ya mwaka 1989 hadi 1996. Makampuni
makubwa yalipewa jukumu la kupanda miti, kuzalisha na kusambaza mkaa kwa ajili
ya kuifanya iwe endelevu. Hapa nchini upo uwezekano kabisa wa kuboresha ubora
wa mkaa kwa kuwajengea uwezo wazalishaji na kuifanya kuwa sekta rasmi huku
tukiendelea kuboresha mazingira yetu. Hali hii ikiwezekana itasaidia sana
katika kuboresha na kuhifadhi misitu katika Tanzania.
Ikiwa sekta ya mkaa itafanywa kuwa
endelevu ni dhahiri kuwa athari zitokanazo na mkaa kama vile uharibifu wa mazingira, hewa ya ukaa
iharibuyo tabia nchi na gesi ya ozone kupunguzwa
kwa kiasi kikubwa.
Kambi rasmi ya upinzani inaitaka
serikali kuanzisha mikakati ya makusudi ya kuweza kuifanya sekta ya mkaa iwe
sekta rasmi na endelevu kwani ni nishati tegemewa na asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania. Pia, mchango wake wa
zaidi ya shilingi trilioni moja katika ukuaji wa pato la Taifa ni mkubwa
ukilinganisha na mazao mengine yatokanayo na misitu hivyo haiwezi kupuuzwa na
kuachwa bila mkakati wowote.
Mheshimiwa Spika, na badala ya kuacha
serikali iendelee kupoteza mapato kupitia watendaji katika halmashauri ambao
wamekua wakitoza faini kwa bidhaa za misitu na mapatao yake kutoingizwa katika
mfuko wa serikali, na ukweli ni kwamba hata tusipo rasimisha mkaa utaendelea
kutumika na itaendelea kuwa ni biashara ya wakubwa tu, na kama taifa misitu
itaendeleka kukatwa na mapato tutaendelea kuyakosa. Kwani ukweli ni kwamba
hatuna chanzo mbadala cha nishati kwa watanzania wa kipato cha chini. Hivyo
basi, ni wakati muafaka kwa serikali kurasimisha biashara za misitu na
kuwafanya wananchi waendelee kufanya kwa utaratibu maalumu na kuweza kuipa
serikali sehemu ya mapato hayo.
Mheshimiwa Spika, mwanamazingira
mmoja duniani aliwahi kusema hivi, naomba kunukuu,”To be poor and be without trees, is to be the most starved human being
in the world”, Hakuishia hapo na
akasema tena “To be poor and have trees,
is to be completely rich in ways that money can never buy” mwisho wa
kunukuu.
Mheshimiwa Spika, tatizo la uharibifu
wa misitu bado limeendelea kuwepo nchini na kuathiri juhudi za utunzaji wa
misitu nchini, itakumbukwa mnamo tarehe 19 April 2013, ilizungumzwa ndani ya
bunge hili kuwa magogo yamekuwa yakisafirishwa nje ya nchi kupitia bandari ya
Dar es Salaam katika maswali kwa mawaziri huku tatizo la madawati kwa wanafunzi
likiwa halijapata suluhu. Swali linakuja je pamoja na majibu ya waziri kuwa
serikali imekwisha piga maruku usafirishaji wa magogo nje ya nchi ni sahihi
kuwa hali iliyopo sasa inathibitisha utekelezaji wa katazo hilo la serikali?
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani haihitaji kujua nani alitoa taarifa zilizo sahihi kati ya mbunge na
waziri, lakini jambo kubwa hapa ni kusimamia sera na taratibu rasmi za serikali
katika kulinda misitu nchini, itakumbukwa kuwa takwimu zinaonesha kuwa ni
asilimia 4 tu ya misitu yetu ambayo huvunwa kwa vibali halali na asilimia 96 ni
kwa njia isiyo halali, hii ni kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na chama cha waandishi wa habari za mazingira (JET)- “Biashara
haramu ya mazao ya misitu yaisumbua Serikali”.
Mheshimiwa Spika, kutokana na
ubadhirifu huo katika sekta ya misitu serikali inakosa mapato yatokanayo na
uvunaji wa misitu, pia wananchi wa pembezoni mwa misitu wanashindwa kujikwamua
katika umaskini, kwa kurejea taarifa ya shirika la mazingira la TRAFFIC ya
mwaka 2007 ilitoa takwimu zilizoonesha hasara inayoipata serikali kwa mwaka
kutokana na biashara haramu ya misitu ikiwa ni shilingi bilioni 75, pamoja na
kuonesha hasara hiyo ya mapato ya serikali pia ilieleza uhusikaji wa viongozi
wa serikali katika ubadhirifu huo.
Mheshimiwa Spika, kambi rasmi ya
upinzani bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa misitu katika kukuza uchumi
na kuwaondoa wananchi katika wimbi la umaskini, hivyo kuweka kipaumbele katika
swala la usimamizi wa misitu iliyopo.
Nyuki
Mheshimiwa Spika, Katika hotuba ya
waziri mkuu aliainisha moja ya vipaumbele vya ofisi yake ikiwa ni pamoja na
Ufugaji Nyuki, na kueleza mwenendo wa sekta ya nyuki nchini, pamoja na maelezo ya waziri mkuu bado
sekta hii ipo nyuma ikilinganishwa na
matamshi ya kuonesha kuwepo kwa juhudi kubwa katika kuiwezesha sekta hii kukua
na kuwa na tija kwa uchumi wa nchi na jamii husika,Ufugaji wa Nyuki ni shughuli
ya kiuchumi inayoweza kuwaongezea Wananchi wetu kipato na kuwaondolea umaskini.
Katika kipindi cha miaka minne iliyopita 2009 - 2012, uzalishaji wa Asali
ulifikia Wastani wa Tani 8,747 na Nta Tani 583 kwa mujibu wa taarifa ya Waziri
mkuu bungeni katika hotuba ya makadirio ya bajeti ya 2013/2014,
Mheshimiwa Spika, swala la kipaumbele
chochote cha serikali si kufanya kwa malengo ya kutangaza nia kwa wananchi kwa
maslahi ya kisiasa, kuna haja ya serikali kuhakiki inatekeleza vipaumbele kwa
kuonesha utendaji halisi hasa kuifanya sekta ya nyuki kuwa na manufaa kwa
wananchi wanaoingia katika biashara hiyo, takwimu zinazotolewa na taarifa za
serikali juu ya kuiwezesha sekta ya ugfugaji nyuiki si za kuridhisha kutokana
na rasilimali nyuki tulionayo nchini.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya
Upinzani bungeni inatoa rai kwa serikali juu ya uwekezaji katika sekta ya nyuki
kwa kuendeleza sekta hiyo kuweza kuwafanya wananchi waweze kuuza bidhaa za
nyuki na sio bidhaa ghafi.
Mheshimiwa Spika, taarifa za mauzo
yatokanayo na bidhaa za misitu,licha ya ukweli kwamba bidhaa za misitu zimekuwa
kianzio kikubwa cha mapato kwa Wizara ya Maliasili na Utalii,wizara inaendelea
kukiri katika taarifa zake kwa uwazi
kwamba hakuna udhibiti wa kutosha kwenye eneo la misitu,hivyo kusababisha makusanyo
ya maduhuli sawa na asilimia 40 kutokusanywa kwa kutokana na changamoto
mbalimbali hususani kuingiliwa na wanasiasa, maslahi madogo kwa watumishi
wasimamizi wa misitu,ulegevu katika usimamizi wa sheria na Kutoeleweka vizuri
kwa vianzio vya kodi na wakusanyaji mapato kama vilivyoainishwa kwenye kifungu
49 cha sheria ya misitu ya mwaka 2002 (Act No 14 of 2002).
Mheshimiwa Spika, Kambi rasmi ya
Upinzani bungeni inaitaka serikali kuona umuhimu wa kuboresha maslahi ya
watumishi wa umma ili kuwapa motisha na kulinda rasilimali za taifa, pia
kuzingatia sheria katika utekelezaji wa mipango ya serikali hivyo itaweza
kudhibiti siasa kuingilia utendaji.
M: HITIMISHO
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru
Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na nguvu hadi wakati huu. Napenda kushukuru
viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kwa msaada mkubwa ambao wamekuwa
wakinipatia katika kutekeleza majukumu yangu ya kibunge na uwaziri kivuli wa
maliasili na utalii. Napenda kuwashukuru wananchi wa Jimbo la Iringa mjini kwa
kunipa nguvu, msaada na ushirikiano tangu wanichague niwe Mbunge wao hadi
wakati huu. Nawaambia kwamba nawapenda na nitaendelea kuwatumikia kadri ya
uwezo wangu wote.
Mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni
kwa familia yangu, kwa uvumilivu mkubwa kwa kipindi chote ninachokuwa sipo
nyumbani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema
hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani naomba kuwasilisha.
_____________________________________
Mchungaji Peter Msigwa (Mb) Iringa Mjini
Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani
Wizara ya maliasili na Utalii
29.04.2013
VERY GOOD PIECE OF SPEECH
ReplyDeleteHotuba nzuri xana paliponifurahisha ni kutajwa kwa kinana waziwazi kama wakala wa meli zinazopora mali zetu,chadema mnatukosha sana
ReplyDeleteamen God will help you be in power soon 2015 is longer long
ReplyDeleteHotuba ya aina yake kwa kweli, na pia hotuba hii imesema hali halisi ya wizara hii ambayo imejaa kila aina ya ufisadi, serikali ingekuwa ni sikivu ingezifanyia kazi tafiti hizo badala ya kupindisha ukweli kama alivyofanya waziri Nchimbi, kwa nini wasiagize uchunguzi ufanyike??? na kwa nini alihamaki kujibu hoja hiyo kama haina ukweli?? big up Mchungaji/Chadema. message sent
ReplyDelete