Friday, April 12, 2013

CHADEMA kutolea tamko vurugu mabaraza ya Katiba


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kitatoa tamko kuhusu vurugu na kasoro zilizojitokeza wakati wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya Katiba mpya.
Tamko hilo litatolewa kesho na viongozi wa kitaifa wa chama hicho, Freeman Mbowe na Dk. Willibrod Slaa, katika kongamano la Wana CHADEMA na wadau mbalimbali kuhusu Katiba mpya.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaimu Katibu wa muda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na Pwani, Henry Kilewo, alisema kongamano hilo litafanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl, Ubungo.
Kilewo alisema mada zitakazowasilishwa katika kongamano ni maudhui ya Katiba mpya, ubovu wa sheria ya mabadiliko, upungufu katika ukusanyaji wa maoni ya wananchi na uteuzi wa wajumbe wa mabaraza ya katiba na mabadiliko yanayohitajika.
Alisema mada hizo zitawasilishwa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika pamoja na Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa chama hicho, Tundu Lissu.
Katika hatua nyingine, Kilewo alisema kabla ya kuanza kwa kongamano hilo watatanguliwa na mkutano wa ndani ambao nao utakuwa na mafunzo ya ujenzi wa chama hicho na mipango ya M4C ya kanda hiyo.

No comments:

Post a Comment