Saturday, April 27, 2013

CHADEMA kufanya harambee Mwanza


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kupitia kitengo chake cha Movement for Change (M4C), Kanda ya Ziwa, kimeandaa karamu ya chakula cha usiku kwa ajili ya kuchangisha fedha zitakazosaidia viongozi wake kuifikia jamii ya watu waishio vijijini.
Taarifa ya Kiongozi wa M4C Kanda ya Ziwa, ‘Kamanda’ Alphonce Mawazo, inaeleza kuwa hafla hiyo itafanyika Aprili 28 mwaka huu katika Hoteli ya Gold Crest jijini hapa.
Kwa mujibu wa Mawazo, hafla hiyo itahudhuriwa na wabunge mbalimbali wa CHADEMA wakiongozwa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, pamoja na wadau kutoka mikoa sita ya Kanda ya Ziwa watahudhuria pia.
Alisema wabunge wengine watakaoshiriki kufanikisha karamu hiyo ya wadau, wananchi, wapenzi na mashabiki wa CHADEMA ni pamoja na Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia na Ezekiel Wenje wa Nyamagana jijini Mwanza.
”CHADEMA kupitia M4C Kanda ya Ziwa tumeamua kuandaa karamu hii ya chakula ili tupate fedha zitakazotusaidia kuwafikia wananchi wa vijijini. Hizi ni harakati maalumu za kuleta ukombozi kwa kuiondoa madarakani CCM mwaka 2015.
Kwa hiyo tunawaomba wadau, wanaharakati, wananchi, wana CCM, wapenzi na mashabiki wa CHADEMA na wapenda maendeleo wote waje tushiriki pamoja kufanikisha safari ya CHADEMA kuingia madarakani 2015,” alisema Mawazo.
Alieleza kuwa wameandaa kadi maalumu kwa watu wote wanaohitaji kushiriki hafla hiyo na kutoa wito kwao kuwasiliana na viongozi wa CHADEMA ili wapate hizo kadi.
Kuhusu mafanikio ya M4C Kanda hiyo ya Ziwa, alisema: “CHADEMA tumefanikiwa sana kubomoa ngome nyingi sana za CCM. Tumekwenda visiwani, mijini na vijijini kote huko wananchi wameamua kuhama analojia ya CCM na kujiunga na dijitali ya CHADEMA.”
Alitumia nafasi hiyo kutoa salamu kwa CCM katika mikoa yote sita ya Kanda ya Ziwa kwamba, mwaka 2015 majimbo na kata nyingi zitachukuliwa na CHADEMA, kwani wananchi wameamua kubadilika baada ya kuchoshwa na utendaji mbovu wa serikali ya chama tawala.
Alisema pamoja na majimbo na kata hizo kunyakuliwa na CHADEMA, pia mwaka huo 2015, CCM haitakuwepo madarakani, bali chama chake hicho kikuu cha upinzani hapa nchini ndicho kinachokwenda kuongoza dola.

No comments:

Post a Comment