Wednesday, March 13, 2013

UNDP yaipa Tanzania fedha za uchaguzi


Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) limetoa msaada wa dola za marejani milioni 22.5  (Sh. bilioni 36) kwa Tume ya taifa ya Uchaguzi (Nec) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Pamoja na mambo mengine, fedha hizo zitatumika kuboresha Daftari la Kudumu laWapigakura. 

Mwenyekiti wa Nec, Jaji mstaafu Damian Lubuva, alisema fedha hizo kwa kiasi kikubwa zitatumika katika maandalizi ya kuboresha daftari hilo na maandalizi ya mchakato wa kura ya maoni ya Katiba mpya mwaka 2014.

Alisema  yapo maeneo ambayo yanapaswa kufanyiwa maandalizi mapema katika kipindi cha uchaguzi ikiwamo kuhakiki idadi ya wapiga kura wapya na wa zamani ili kuleta uchaguzi huru na haki.

Alisema fedha hizo pia zitatumika katika masuala ya habari, mawasiliano na teknolojia (ICT), kusaidia mikakati ya tume hizo, utoaji wa elimu ya haki za binadamu kwa polisi, mafunzo kwa wagombea wanawake, kusaidia utoaji wa elimu ya mpigakura, pamoja na mafunzo ya utumiaji wa vifaa vya kisasa.

Aliongeza kuwa lengo kubwa laNec na Zec ni kufanya maandalizi mapema ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuepuka lawama kutoka kwa wapiga kura ya kutokuwapo kwa majina yao katika daftari.

Alifafanua kuwa hadi kufikia 2015, zoezi la kuhakiki majina katika daftari litakuwa limekamilika endapo serikali itatoa kiasi cha fedha kilichobakia kwa kuwa msaada waliupata hautatosheleza katika zoezi zima la maandalizi ya uchaguzi.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwakilishi wa UNDP nchini, Tanzania, Dk.Alberic Kacou, alisema UNDP imejikita katika usaidizi endelevu wa maendeleo ya demokrasia nchini, ikiwamo kusaidia taasisi zinazojishughulisha na masuala ya uchaguzi.

Mbali na UNDP, wafadhili wengine walioonyesha nia ya kusaidia katika utekelezaji wa mradi huo kupitia bajeti ya UN ni Norway, Sweden, Ireland, Finland, Canada, Uingereza, Umoja wa Ulaya (EU), Denmark, na Uswis watakaochangia kupitia mfuko wa pamoja wa wafadhili.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment