KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, amesema kuwa Bunge limewachefua kwa kuwataka wabunge wao wahojiwe na kamati batili, kwani ilivunjwa na Spika Anne Makinda katika Mkutano wa Kumi wa Bunge uliofanyika Januari mwaka huu.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Slaa amemuagiza Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, kwa niaba ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, kumwandikia barua ya kukataa hatua hiyo na huhoji uhalali wa kamati iliyomaliza muda wake kuendelea na kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dk. Slaa alisema kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za Bunge, kamati ambazo zimeshavunjwa haziwezi kuendelea kufanya kazi yoyote kwa kuwa ni batili mpaka hapo zitakapoundwa nyingine.
Alilitaka Bunge kurejea kanuni za kudumu za Bunge namba 113 (7), inayozungumzia ukomo wa uhai wa kamati za Bunge, uhai wake unaishia Mkutano wa Kumi wa Bunge ambapo inakuwa ni nusu ya kwanza ya uhai wa Bunge lenyewe.
Dk. Slaa alisema kutokana na kifungu hicho, inaonesha dhahiri kwamba Spika Anne Makinda na wasaidizi wake wana matumizi mabaya ya sheria, kutoifahamu vizuri ama kulewa madaraka, hali ambayo CHADEMA haitakubaliana nayo.
Hivyo alisema Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge ambayo ilikuwa chini ya Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan Ngwilizi (CCM) haitawahoji wabunge wake kwa kuwa imekwisha maliza kazi yake tangu Februari 8, mwaka huu.
Msimamo wa CHADEMA unakuja zikiwa ni siku mbili tangu Ofisi ya Bunge kupitia Katibu Mkuu Dk. Thomas Kashililah, itumie Jeshi la Polisi kuwapa taarifu baadhi ya wabunge wa chama hicho kuwa wanahitajika jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na kamati hiyo.
Dk. Slaa alisema Bunge lisifanye makusudi huku likijua kuwa linavunja sheria kwa kuwataka wabunge hao wakahojiwe na kamati isiyokuwepo na kwamba kinachotakiwa kuhojiwa tayari kimekwishatolewa hukumu bila kuwahusisha wahusika Februari 8, mwaka huu.
Katibu Mkuu huyo alisema kama wabunge wa CHADEMA wanaitiwa kuhusu vurugu zilizotokea bungeni Februari 4, mwaka huu, tayari zimeshatolewa hukumu yake kwa kuwataja wahusika kuwa ni Tundu Lissu (Singida Mashariki) John Mnyika (Ubungo), Paulina Gekul (Viti Maalumu) na Joshua Nassari (Arumeru Mashariki).
Alisema katika hukumu hiyo ambayo ilisomwa na Spika Makinda ilikuwa ya upande mmoja wa kamati yenyewe iliyokaliwa na wabunge wa CCM ambao waliwaona wabunge wa CHADEMA pekee ndio waliofanya vurugu, huku ikishindwa kuwaita wahusika kwa mahojiano.
Kutokana na maelezo hayo, Dk. Slaa alisema kwa kuwa kamati ilishamaliza kazi yake, hakukuwa na haja ya kupitisha sheria na kukusanya wabunge wengine kwa ajili ya kuhojiwa.
Aidha, alisema hata kama kamati ya Brigedia Ngwilizi ingekuwa hai, wabunge wake wasingeitii kwa kuwa tayari ameshawahukumu.
Hata hivyo Dk. Slaa alitumia nafasi hiyo kumtaka Spika Makinda kwenda kozi kwa ajili ya kujifunza sheria ya kuongoza Bunge kutokana na kushindwa kwake katika kipindi chote alichokalia kiti hicho.
“Nasikia Spika Makinda huwa anasema kuwa niwafundishe wabunge wangu sheria, kanuni na taratibu za Bunge kwa kuwa nazifahamu vizuri. Kwani yeye na wanasheria wake wanafanya nini? Kupoka kwake sheria na taratibu za bunge ndiko kunasababisha vurugu?” alihoji Dk. Slaa na kuongeza:
“Nataka nimwambie kwamba wakati nipo bungeni, maspika waliokuwa wakiongoza Bunge akiwemo Samuel Sitta walikuwa wakijua kuongoza kwa kufuata sheria na kanuni zake na ndiyo maana hakuna vurugu zilizokuwa zikitokea na si yeye.”
Aidha, alisema maspika hao walikuwa wanajua kwamba mabunge yote ya Afrika na yale ambayo Tanzania inaiga kutoka kwao yana sheria na taratibu zinazowaruhusu kuchangia hata kuzomea kwa kutaja chama chao na si hivi ambavyo Spika Makinda anavyofanya.
Lissu anena
Akizungumza kwa niaba ya wenzake walioandikiwa barua za kuhojiwa, Lissu alisema hakuna atakayekwenda, kwa kuwa barua ya siri waliyopewa na Bunge kutaka wahojiwe haijajitosheleza kisheria.
Lissu alisema kwa mujibu wa sheria na kanuni za Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, zinamtaka Katibu Mkuu wa Bunge, Dk. Kashililah kuandika barua hizo kwa niaba ya Spika Makinda lakini hakufanya hivyo.
Lakini pia Lissua alisema hata barua ya polisi (Police message) waliyopewa si taarifa tosha ya kujipeleka wao kuhojiwa, bali walipaswa kupelekewa taarifa ya kuitwa kwa ajili ya mahojiano na Bunge.
Kutokana na maelezo hayo, Lissu alisema hakuna jambo lililofuatwa kisheria, hivyo hakuna watakayemwona na kwamba alidai kuwa tayari hukumu yao ilishatolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Brigedia Ngwilizi, Februari 8, mwaka huu.
“Hata kama kamati hiyo ingekuwa bado hai, bado tusingeenda kwa kuwa tayai tumeshapewa hukumu yetu ambayo ilisomwa na Spika Makinda kwa kutudhalilisha kwa taifa kwamba sisi ni watovu wa nidhamu, lakini pia ni vinara wa vurugu bungeni,” alisema.
No comments:
Post a Comment