Saturday, March 16, 2013

Polisi yaibua utata sakata la Lwakatare


VIDEO YAKE YAACHA MASWALI MENGI MTANDAONI
WAKATI Jeshi la Polisi likiendelea kumshikilia na kumhoji Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, baadhi ya wananchi wameonyesha wasiwasi na jeshi hilo katika kushughulikia matukio ya kihalifu nchini.
Lwakatare alikamatwa juzi makao makuu ya chama hicho, kisha kuhojiwa na kupekuliwa nyumbani kwake kwa tuhuma za uchochezi na uvunjifu wa amani nchini.
Kada huyo ambaye anahusishwa na picha ya video iliyosambazwa kwenye mtandao ikimwonyesha akipanga mikakati na kuwaelekeza watu ambao sura zao hazionekani kufanya matukio ya kumteka mtu ambaye hatajwi kwa jina, kwa siku ya pili jana aliendelea kuhojiwa na kupekuliwa.
Hata hivyo, hatua hiyo ya Jeshi la Polisi kumkamata haraka Lwakatare na kumhoji kwa kutumia mkanda huo wa video kwenye mtandao imeleta mashaka ambapo baadhi ya watu wanatafsiri kitendo hicho kama mkakati maalumu wa kuichafua na kuidhoofisha CHADEMA.
Wachambuzi hao wa masuala ya kisiasa na watalaamu wa mitambo licha ya kutotaka kulizungumzia suala hilo kwa undani ili wasiingilie kazi ya polisi, walisema inashangaza kuona wepesi wa jeshi hilo katika tukio la Lwakatare wakati wako watuhumiwa wametajwa kuhusika na uhalifu mkubwa hawakamatwi wala kuhojiwa.
Katika orodha hiyo, wanamtaja mtumishi wa Ikulu, Ramadhan Ighondo, ambaye alitajwa na gazeti la MwanaHalisi pamoja na Dk. Stephen Ulimboka mwenyewe kuwa alihusika kumteka na kumtesa kiongozi huyo wa madaktari Juni 26, mwaka huu, lakini hadi leo hakuwahi kuhojiwa na polisi.




“Naibu Katibu Mkuu wa CCM (bara), Mwigulu Nchemba, akihojiwa na kituo cha televisheni cha Star Januari, mwaka huu, alitamka kuwa anayo video inayowaonyesha viongozi wa CHADEMA wakipanga mauaji. Huyu polisi hawakumhoji ili awapatie video hiyo, kwa nini iwe haraka kwa Lwakatare?” alihoji mtoa taarifa.
Wachambuzi hao walitaja mlolongo wa matukio ya kinyama waliyotendewa baadhi ya watu akiwemao Saeed Kubenea, Dk. Ulimboka, marehemu Daudi Mwangosi na sasa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absolam Kibanda, wakisema kuwa jeshi la polisi limeshindwa kuwakamata wahusika wa vitendo hivyo licha ya kujitutumua kuunda kamati za uchunguzi kila yanapotokea.
Waligusia pia mauaji ya raia wasio na hatia waliouawa kwa risasi na polisi kwenye mikutano na maandamano ya CHADEMA halafu uchunguzi wake ukaishia kwenye majibu yasiyowataja wazi wahusika na kuwachukulia hatua.
Kutokana na mtiririko wa matukio hayo pamoja na kejeli za hivi karibuni za mtoto wa Rais Ridhiwan Kikwete na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nauye, kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook kuhusu sakata la kuteswa kwa Kibanda, wachambuzi hao wanadai huo ni mkakati wa kuidhoofisha CHADEMA.
“Haya hayakuanza leo, huu ni mkakati wa wahuni wachache wanaotumia mwamvuli wa Idara ya Usalama wa Taifa kufanya matendo haya halafu wanahamisha watu kwenye ajenda kwa kutunga mambo tofauti ya kuwabambika watu,” kilisema chanzo chetu na kuongeza: “Katika hili vyombo vya habari vinapaswa kushikamana kuhoji uchunguzi wa matukio makubwa umeishia wapi. Waliomdhuru Kubenea si walijulikana? Wako wapi? La Ulimboka na Mwangosi polisi wameshindwa na sasa hili la Kibanda wanataka kuwahamisha kwenye hoja kwa kukimbilia kuhangaika na Lwakatare.”
Video yakosolewa
Katika hatua nyingine, wataalamu wa mitambo ya video wamekuwa wakitoa maoni yao kwenye mitandao ya kijamii kukosoa ukanda wa video unaomuonyesha Lwakatare akidaiwa kupanga mikakati ya kudhuru watu.
Wataalamu hao walitoa sababu kadhaa wakidai kuwa video imechukuliwa Desemba 28, mwaka jana, baada ya sikukuu ya Krismasi bila kama inavyosikika lakini wakahoji kwa nini video ije kutolewa sasa hivi baada ya tukio la kuteswa kwa Kibanda.
Katika sababu ya pili wanasema video imechukuliwa na kamera yenye Mega Pixel zaidi ya 5, na kwamba kamera za siri huwa hazina pixel kubwa kiasi hicho. Ni wazi wahusika walikuwa wanajua kabisa kuwa wanajirekodi.
Wanaongeza kuwa kauli ya Nchemba kuhusu kuwa anayo video ikiwaonyesha viongozi wa CHADEMA wakipanga mauaji ya watu, tangu CHADEMA imtake apeleke video kwenye vyombo vya dola ili wahusika wachukuliwe hatua ni kwa nini hakufanya hivyo.
“Mhusika kuweka hiyo video ‘Bukoba Boy’ amejiunga na Youtube Machi 11, mwaka huu, na tarehe hiyo akaweka hiyo video ambayo aliichukua Desemba 28 mwaka jana.
“Je, kama analipenda taifa hili kwa nini asingeweka tangu kabla ya tukio pengine Kibanda angeepukana na hatari hii? Walihoji wachambuzi hao.”
Waliongeza kuwa kama kweli polisi ina nguvu kwa nini haijamkamata huyu mtu mpaka sasa hivi kwa kuwa ni hatari kwa taifa.
“Katika dakika ya 16 na sekunde ya 55 ya video hii, Lwakatare anasema ‘ama nilivyopewa na kuichunguza hii changamoto ina maana kuna mtu kamtuma kusema haya maneno, swali je ni nani?” Wanahoji.
Katika dakika ya 17 sekunde ya 32, Lwakatare anasema, “Kama huyu mtu anakuwa na sehemu nyingi sasa tutafuatilia ngapi? Lazima awe na sehemu moja maalumu kuwa hakosi.”
Wanaongeza kuwa hivi mtu anayepanga mauaji anachagua sehemu, kwamba mbona Mwangosi aliuliwa kwenye mikono ya polisi; ina maana ndiyo ilikuwa sehemu yake.
Wanahoji kuwa mbona kijana kwenye maandamano ya CHADEMA alikufa ina maana Morogoro kila siku palikuwa na mikutano na hapo palikuwa sehemu yake ya kuuawa?
“Mwisho kwa nini video imekatishwa katikati? Je, kuna matukio mengine yatafanyika halafu ndiyo waje na video ya sita maana hiyo ni video ya tano? Mwanzo kabisa ya video wanarekebisha maiki, na mchukua video anasema, “tuta-‘note’ upya hapo.
“Hii ina maana kuna marekebisho ya kubadili kamera yalifanyika hata video inavyoanza tunaona kabisa walikuwa kimya,” alisema mtaalamu huyo wa video.
Dk. Slaa afichua mipango
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa amefichua mipango ya Jeshi la Polisi kutumika kisiasa kufanya michezo michafu dhidi ya chama hicho.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Dar es Salaam, alisema kwa mara kadhaa wameripoti polisi matukio mbalimbali kuhusu mbinu chafu walizokuwa wakifanyiwa lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
Alisema hata katika sakata la Lwakatare hashangazwi kwani kiongozi huyo amekuwa akiwindwa kwa muda mrefu kwa kuzushiwa tuhuma mbalimbali.
Dk. Slaa alisema ameisikiliza vizuri video inayomhusisha Lwakatare na tuhuma za uchochezi ambapo kuna mtu anamuuliza maswali elekezi lakini mtu huyo haonekani.
Alisema jeshi la polisi halijawahi kuchukua hatua stahiki kwa suala la mauaji ya Mwangosi kwa kumwajibisha Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa aliyesimamia na kufanikisha mauaji hayo.
Hata sakata la Dk. Ulimboka baada ya kuteswa, polisi wameshindwa kumhoji mtuhumiwa anayedaiwa kuwa ofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wa Ikulu, ambaye alidaiwa kuhusika.
Dk. Slaa alifafanua kuwa hawezi kushangaa ikiwa jeshi la polisi halitamhoji Kibanda.
Aliongeza kuwa Lwakatare kuhusishwa kwa sakata la sasa la mkanda wa video uliopo katika mtandao ni mwendelezo wa kukihujumu chama, unaoratibiwa na Usalama wa Taifa, huku ukitekelezwa na jeshi la polisi.
“CHADEMA inafahamu kwa undani kwamba uzushi huu wa tepu ya ‘Bukoba Boy’ umeanzishwa na kuhusisha Usalama wa Taifa, akiwemo Ighondo na wenziwe pale Ada Estate,” alisema.
Hata hivyo alishangazwa na jeshi la polisi kufanya haraka kumshikilia Lwakatare, kwani vyombo vya habari hivi majuzi vimemtaja kwa jina, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, kuwa alihusishwa na utekwaji na uteswaji wa Kibanda, lakini jeshi halikusema lolote hadi sasa.
“Ridhiwan Kikwete na Nape Nnauye waliingia kwa ID zao kwenye mitandao kukejeli suala la kuteswa Kibanda lakini jeshi halikuchukua hatua, lakini hili la Lwakatare wanafanya haraka kumkamata, hizi ni mbinu tu za kuichafua CHADEMA.
Alisema kuwa mara nyingi wametoa madai kwa Rais aunde Judicial Commission of Inquiry (Tume Huru ya Kimahakama kuchunguza vifo vyote vyenye utata na sura ya kisiasa) lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.

No comments:

Post a Comment