MBUNGE wa Ubungo John Mnyika leo ataongoza maandamano ya amani kwenda Wizara ya Maji kupata majibu kuhusu matatizo ya maji, licha ya kuzuiwa na Jeshi la Polisi.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kinondoni, ACP Charles Kenyela amekataza maandamano na mkutano huo kwa madai kuwa eneo la Manzese Bakhresa walilopanga kufanyia mkutano ni maegesho ya magari ya mizigo.
Akizungumza kwa niaba ya Mnyika, mratibu wa maandamano hayo kutoka ofisi ya mbunge, Gaston Garubindi, alisema kuwa maandalizi yamekamilika na mbunge huyo ataongoza kama ilivyopangwa.
Garubindi alisema kuwa Kenyela amewadanganya wananchi kwa kueleza kuwa Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe hakuwa na taarifa wakati ofisi ya mbunge ilimwandikia barua yenye kumbukumbu namba OMU/MJ/001/2013 na nakala nyingine kupelekwa kwa viongozi wengine wa wizara hiyo.
Kuhusu suala la hofu ya kuzuka kwa vurugu, Garubindi alisem kuwa polisi ndio watakaoanzisha vurugu hizo kutokana na kutoa vitisho vya kuzuka kwa maafa.
“Maafa hayaletwi kwa sababu ya maandamano ya amani, siku zote polisi ndio wanaleta maafa katika maandamano, tumeeleza ni mandamano ya amani lakini wanatujibu kisiasa zaidi,” alisema.
Pia alisema kuwa maandamano hayo hayatazuia shughuli zozote za kijamii wala kuleta uvunjifu wa amani kwani lengo ni kupata majibu ya hoja ya mbunge aliyoitoa bungeni, hivyo anataka mrejesho kama alivyotumwa na wananchi anaowawakilisha.
No comments:
Post a Comment