Friday, March 1, 2013

Mbowe: Tuache harakati tuchukue nchi

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amewataka wafuasi wa chama hicho, kuachana na siasa za vurugu na kujiepusha kujenga uhasama na vyombo vya dola ili kukiwezesha kuingia Ikulu mwaka 2015. akihutubia mamia ya wakazi wa mkoa wa Mbeya katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jana, Mbowe alisema siasa za chuki zimepitwa na wakati. 

Alisema siasa za kiharakati zimekuwa zikichochea vurugu, kitendo ambacho kimefanya chama hicho kueleweka vibaya kwa jamii.

Alisema sasa ni wakati wa wafuasi wake kubadili mfumo wa siasa zao ili kujenga mikakati imara ya kukiwezesha na kukubalika zaidi kwa Watanzania.

“Msikubali kujiingiza kwenye uhasama na vyombo vya dola, wala kuingia katika mitego ya kuhatarisha amani…naamini wapo watendaji wa jeshi la polisi ambao hupenda kuminya haki zetu za kikatiba kama vile kufanya maandamano,tunasema hawa nao watuelewe,”alisema Mbowe.

Kutokana na hali hiyo, alivitaka vyombo vya dola kuheshimu haki za kisiasa ili kuepusha malumbano yasiyo ya lazima, baina ya vyombo hivyo na wafuasi wa CHADEMA.

Kuhusu matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka huu, Mbowe alipinga hatua ya Serikali kuunda tume ya kuchunguza matokeo hayo kwa maelezo kuwa Watanzania hawahitaji tume, bali wanataka uwajibikaji kwa viongozi wote waliosababisha kushuka kwa ufaulu.

Alisema uundaji wa tume hiyo, utapoteza fedha nyingi za umma zinazoweza kutumika katika miradi mingine ya maendeleo kwa wananchi, wakati sababu za hali hiyo zinafahamika. Kutokana na hali hiyo,amewataka wanafunzi wote waliofeli mtihani huo na wanafunzi wa wa shule za sekondari, vyuo vikuu, wazazi na wafanyabiashara kuungana kwa pamoja kuingia barabarani kupinga matokeo hayo.

Alisema hatua hiyo, inakuja kutokana matokeo hayo kuumiza Watanzania na baadhi ya wanafunzi wameripotiwa kujiua baada ya kufeli.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde (CHADEMA) alipinga hatua ya uongozi wa Bunge kutaka kuzuia kuoneshwa moja kwa moja ‘live’kwa vikao vya Bunge kwa madai hatua hiyo, ina lengo la kuficha ukweli kwa watanzania.

“Kutokana na kuongezeka kwa wabunge wa upinzani bungeni, nguvu ya kuuibua mambo ya ufisadi na mengine yenye manufaa kwa Taifa, imekuwa ikiongezeka sasa, wanataka kuficha ukweli wa mambo,” alidai Silinde.

Mkutano huo, uliohudhuriwa na maelfu ya wakazi wa mkoa wa Mbeya, uliitishwa na chama hicho kwa ajili ya uzinduzi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini ya CHADEMA na kuhudhuriwa na viongozi wake kutoka mikoa ya Ruvuma, Iringa, Njombe na Mbeya.

No comments:

Post a Comment