ADAI LAZIMA ANG’OKE NA NAIBU WAKE HATA KWA MAANDAMANO
MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema zimebakia siku tatu kumalizika muda aliowapa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na naibu wake Philip Mulugo, kujiuzulu.
CHADEMA kupitia kwa Mbowe ilitoa siku 14 kwa waziri na naibu wake kuachia ngazi kama sehemu ya uwajibikaji kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne yaliyotangazwa hivi karibuni.
Akihutubia mkutano wa hadhara jana mjini hapa katika uwanja wa Luanda –Nzovwe maarufu kama Uwanja wa Dk. Slaa, Mbowe alisema kuwa zimebakia siku tatu kwa viongozi hao kujiuzulu vinginevyo ataongoza maandamano makubwa ya kuwang’oa.
Alisema kuwa viongozi hao ndio walichangia matoke hayo mabaya kutokana na kutowajibika ipasavyo hivyo lazima wahakikishe wanaondoka haka kwa kulazimishwa.
“Mimi nitaongoza maandamano ya kuwang’oa Kawambwa na Mulugo, polisi wajiandae kwa maandamano hayo makubwa, niko tayari kufa kwa hilo na mwili wangu wautupe kando ya barabara,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo ambaye alikuwa akizindua kanda ya kichama ya Nyanda za Juu Kusini, alisema kuwa polisi kuzuia maandamano hayo itakuwa noma.
Februari 18, mwaka huu, akiwa mjini Mwanza wakati wa uzinduzi wa Kanda ya Ziwa Magharibi katika viwanja vya Furahisha, Mbowe alisema Kawambwa na Mulugo pamoja na katibu mkuu wa wizara hiyo, wameshindwa kuiongoza sekta hiyo muhimu, ndiyo maana kwa sasa wanafunzi wanaishia kuandika matusi na kupata sifuri katika mitihani ya kumaliza kidato cha nne.
Alisema waziri huyo lazima ajiuzulu nafasi hiyo, kwani taifa ameliingiza pabaya na kuanza kuzalisha maelfu ya watoto wa maskini kumaliza elimu zao za msingi na sekondari wakiwa hawajui kusoma na kuandika.
Katika matokeo hayo, Kawambwa alisema watahiniwa wote kwa ujumla waliosajiliwa walikuwa 480,036 kati yao wasichana 217,583 sawa na asilimia 45.33 na wavulana 262,453 sawa na asilimia 54.67 lakini waliofanya mtihani huo ni 456,137 sawa na asilimia 95.44, wengine 21,820 (asilimia 4.55) hawakufanya mtihani.
Katika matokeo hayo wanafunzi waliopata daraja la kwanza ni 1,641, la pili 6,453, la tatu 15,426, la nne 103,327 na daraja sifuri wako 240,903.
Mbowe ambaye alipata mapokezi makubwa tangu alipowasili mjini humo juzi, aliweza kuchangisha fedha za papo hapo sh 3,267,550 ndani ya dakika tano za kukijenga chama.
Katika mkutano huo mkubwa Mbowe aliongozana na viongozi wengine wa chama hicho ngazi ya taifa na uongozi mpya wa kanda hiyo.
Mara baada ya kuzindua uongozi wa kanda unaojumuisha mikoa minne ya Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma, Mbowe pia alizindua rasmi harakati za chama hicho kuelekea mwaka 2015.
Hata hivyo alipata wakati mgumu kukata utepe kutokana na umati mkubwa wa watu waliofurika uwanjani hapo kupita kiasi.
Alilazimika kuwaomba wananchi waliofurika uwanjani hapo wageuke nyuma na kurudi hatua tano ili kuweza kuruhusu umati mkubwa uliokuwa karibu na jukwaa uweze kupata sehemu ya kutosha.
“Ndugu zangu wa Mbeya, makamanda wa CHADEMA, hatuwezi kuendelea na mkutano wetu katika msongamano mkubwa kama huu, bora tuvunje mkutano kuliko kushuhudia watu wakiumia, nawaomba wote mgeuke nyuma na mrudi hatua tano,” alisema.
Naye mbunge wa viti maalumu mkoa wa Mbeya, Naomi Mwakyoma, alisema kuwa hivi sasa ni zamu ya wanawake wengi katika mkoa huo kujitokeza na kushiriki kwenye nafasi za uongozi na kwamba hawapaswi kudharau aina yoyote ya uchaguzi.
Alisema kuwa umati mkubwa wa wananchi uliojitokeza katika mkutano huo utakuwa ni alama ya ushindi endapo kundi kubwa la wanawake na vijana wataendelea kujitokeza.
No comments:
Post a Comment