POLISI WASAKA MAANDISHI YAKE OFISI ZA CHADEMA
WAKATI afya ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare, ikiendelea vizuri, daktari wa serikali aliyefika polisi kumwangalia anadaiwa kukwepa kumpatia matibabu.
Hatua hiyo ilimlazimu Lwakatare kupatiwa matibabu na kaka yake ambaye ni daktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Lwakatare ambaye anasumbuliwa na ugonjwa wa kisukari na hivyo kuhitaji uangalizi wa karibu, alikamatwa na Jeshi la Polisi Jumatano ya wiki iliyopita baada ya kuonekana katika video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii akidaiwa kupanga mikakati ya kudhuru baadhi ya watu.
Chanzo chetu kilisema kuwa daktari huyo wa serikali alifika polisi Kanda Maalumu ya Dar es Saalam juzi kwa ajili ya kumwangalia Lwakatare, baada ya baadhi ya magazeti kuripoti afya yake kudhoofu.
Kwamba alimwangalia Lwakatare na kuahidi kuwa anaenda na angerudi baadaye kumletea dawa lakini hadi jana alikuwa hajarudi, hatua iliyoifanya familia ya Lwakatare kumwita ndugu yao, Dk. Lwakatare ampatie matibabu.
“Hali yake kwa sasa kwa kweli ni nafuu, kaka yake alimletea dawa,” kilisema chanzo chetu.
Akizungumza kwa simu wakili wa Lwakatare, Nyaronyo Kicheere alisema kuwa mteja wake anaendelea vema sasa.
Aliongeza kuwa jana polisi walikwenda makao makuu ya ofisi za CHADEMA kutafuta karatasi zozote ambazo mteja wake aliwahi kuandika kwa mkono ikiwa ni sehemu ya kuendelea na upelelezi.
Alisema kuwa maofisa wa polisi walikwenda makao makuu ya CHADEMA wakiwa na Lwakatare pamoja na yeye mwenyewe kuchukua sampuli za karatasi zenye mwandiko wa Lwakatare.
Hata hivyo, jambo hilo lilifanyika bila kuwepo uongozi wa chama katika ofisi hizo kwani ilikuwa ni siku ya mapumziko.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu, Mkurugenzi wa Sheria na Katiba wa CHADEMA, Tundu Lissu alisema ili kuingia kukagua eneo fulani, polisi wanahitajika kuwa na waranti ya kupekua.
Alisema kuwa waranti hiyo hutolewa na polisi au mahakama, na kwamba hata kama walikuwa nayo ilikuwa vizuri zaidi kama wangewataarifu wenye ofisi.
Kuhusu Lwakatare kufikishwa mahakamani leo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini Advera Senso alisema kuwa upelelezi bado unaendelea, na kwamba huenda akafikishwa.
Alipoulizwa kwa simu ni kwanini hana uhakika na hilo, Senso alisema: “Nimekwambia huenda atapelekwa mahakamani.”
Ikulu yaruka
Siku moja baada ya gazeti hili kuripoti madai ya kunaswa mawasiliano ya siri ya ofisa mmoja wa Ikulu, akiwapongeza vijana walioandaa video ya Lwakatare na kwamba hiyo ni kete kubwa kwa CCM, ofisi hiyo imeibuka na kukanusha taarifa hizo.
Ikulu imesema kuwa ofisi ya Rais Jakaya Kikwete isibebeshwe msalaba wa watu wengine kwani haiwezi kuhusika kwa namna yoyote kuteka, kuua au kuwashambulia raia wake.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salva Rweyemamu wakati akizungumzia tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri, Absalom Kibanda.
Rweyemamu alitoa ufafanuzi huo akijibu taarifa ya gazeti hili juzi iliyonasa na kuchapisha mawasiliano ya ofisa mmoja wa Ikulu akipongeza kazi ya Idara ya Usalama iliyofanikiwa kuandaa video ya Lwakatare.
Salva alisema Ikulu kamwe haiwezi kuhusika na vitendo vya kuteka raia wake kwani jukumu lake ni kulinda haki za raia wake wote.
“Ikulu haiwezi kuhusika na mambo ya kijinga kama haya. Inachokifanya ni kuhakikisha inawasaka wahusika ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria na ndiyo maana hata Rais Kikwete alimtembelea Kibanda kule Afrika Kusini alikolazwa,” alisema Salva.
Alisema anamfahamu Kibanda, ameumizwa na jinsi alivyovamiwa na kupigwa na kusababishiwa maumivu na majeraha ya kudumu.
“Kibanda ni mdogo wangu, mimi ndiye niliyempokea na kumfundisha kazi, siwezi kufurahia alichofanyiwa,” alisema.
Kuhusu mawasiliano ya ofisa wa Ikulu, Salva alimtaja afisa huyo kuwa ni Muhidin Michuzi ambaye ni mmoja wa wapiga picha wa rais.
Akifafanua kuhusu mawasiliano hayo ya Michuzi, Salva alisema haikuanzia kwake kwani naye alitumiwa na mtu mwingine.
“Yale mawasiliano hayakuanzia kwa Michuzi. Yeye alitumiwa tu, alichokifanya ni ku-‘share’ ile taarifa na watumishi wengine wa Ikulu. Hapa kosa lake nini?” alihoji Salva.
Hata hivyo, Salva alitahadharisha kwamba ni kosa kisheria kwa mtu yoyote kuingilia mawasiliano ya mtu na kuyaweka hadharani.
Alivitaka vyombo vya habari kuviachia vyombo vya dola kuchunguza tukio la kushambuliwa kwa Kibanda badala ya kuandika habari za mitaani.
No comments:
Post a Comment