CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kauli ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa kwamba kuna baadhi ya watumishi wa vyombo vya dola wanaripoti kwake, kimesababisha baadhi ya wananchi kukosa imani na vyombo hivyo.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkoa Maalum wa CCM Dar es Salaam baada ya kikao chao kutathimini mambo na matukio mbalimbali yanayolitikisa taifa kwa sasa.
Katika taarifa yao iliyosainiwa na Katibu wa Wilaya ya Dar es Salaam (ya kisiasa - CCM), Daniel Zenda ilisema kuwa Dk. Slaa amekuwa akitoa kauli hizo mara kwa mara tangu wakati wa kampeni za urais mwaka 2010, lakini hajaitwa kuulizwa wala kuchukuliwa hatua.
“Lakini pia kauli ya Dk. Slaa imesababisha wananchi wakose imani na Idara ya Usalama na zaidi kupoteza imani juu ya uwezo wa serikali kuwalinda na kuwahakikishia usalama wa maisha yao, ambapo ni jukumu la kikatiba la serikali,” ilisema taarifa hiyo.
Vijana hao wa CCM, wameitaka Idara ya Usalama kumhoji kwa kina Dk. Slaa athibitishe madai yake kuwa baadhi ya watendaji wa taasisi hiyo muhimu na nyeti wanaripoti kwake kinyume na utaratibu, kanuni na maadili ya taasisi hiyo.
Chama hicho pia kimelaani vikali matukio ya kuvamiwa, kudhuru mwili na kuuawa kwa baadhi ya viongozi wa dini na wanahabari.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mkoa huo umesikitishwa na tukio la kushambuliwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF) na Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, Absalom Kibanda.
“Tunavitaka vyombo vya dola kuwakamata, kuwachukulia hatua za kisheria wote waliothibitika kuhusika na matukio ya namna hiyo bila kuangalia itikadi za kivyama, cheo ama kundi.
“Na pia kuyataka makundi ya kijamii, wanaharakati na wanasiasa kuacha kuingilia/kuvuruga kwa namna yeyote taratibu za kisheria na kiusalama,” ilisema taarifa hiyo.
No comments:
Post a Comment