Friday, March 15, 2013

Chadema yachachamaa kukamatwa Lwakatare


Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetoa angalizo kwa Jeshi la Polisi nchini kwa kulitaka lisiingize ushabiki wa kisiasa wenye lengo la kukichafua katika uchunguzi dhidi ya Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa chama hicho, Wilfred Lwakatare.

Hata hivyo, wakati Chadema wakitoa tamko hilo, Lwakatare aliyekamatwa tangu juzi bado anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi.

Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, wakati akizungumza na waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam kuelezea mazingira ya kukamatwa kwa Lwakatare na maofisa wa Jeshi la Polisi kutoka makao makuu.

“Chadema haitakubali kuona upelelezi wa suala la Lwakatare Jeshi la Polisi linaingiza ushabiki wa kisiasa, Chadema katika hatua ya awali tunafuatilia kwa karibu sakata lote la ukamataji wa Lwakatare na kuona sheria za nchi, taratibu na misingi ya haki za binadamu inafuatwa kikamilifu,” alisema Dk. Slaa, ambaye aliongozana na baadhi ya viongozi waandamizi wa chama hicho.






Baadhi yao ni Makamu Mwenyekiti, Said Arfi; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi; Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse; Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, Mbunge wa Viti Maalum, Susan Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Owenya na Mbunge wa Viti Maalum, Naomi Kaihula.

 Dk. Slaa alisema chama chake kina mashaka na upelelezi huo kuingiliwa na ushabiki wa kisiasa kwa sababu uzoefu unajionyesha kuwa Chadema kimekuwa kikitoa taarifa polisi kulalamikia mchezo mchafu unaofanywa na baadhi ya watu wanaoandika barua na nyaraka mbalimbali za kughushi zenye lengo la kukichafua.

Alisema licha ya jitihada hizo zinazofanywa na Chadema kikiwa na matumaini kuwa vyombo vya ulinzi vitayafanyia kazi masuala hayo, lakini katika hali ya kushangaza yanapuuzwa bila kufanyiwa kazi, jambo linalotia mashaka uadilifu wa Jeshi la Polisi.

 Alitoa mfano kuwa wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora, kuna kijana anayedaiwa kuwa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  alipewa bunduki kwa lengo la kudhuru watu wakati wa kampeni, lakini licha ya Chadema kutoa taarifa na kutaja namba ya bastola husika na mahali ilipotengenezwa, mpaka sasa polisi hawajatoa tamko lolote kama ilisajiliwa kwa jina la nani na mtuhumiwa alijisalimisha kwa mlinzi wa amani.

Alisema tukio jingine ambalo Chadema walilalamikia polisi ni suala la mtu mmoja kuandika barua ya kughushi ikidaiwa kuandikwa na Lwakatare akiomba Sh. milioni 200 kwa ajili ya vijana wanaodaiwa kuwapeleka Igunga kutoka Tarime kwa ajili ya uchaguzi.

“Pamoja na matukio haya na mengine kuripotiwa, polisi hawajafanya upelelezi wowote, lakini kwa tukio tu la Lwakatare na picha yake kubandikwa kwenye mtandao, polisi tayari wameshamkamata, ni dhahiri kuna mchezo unachezwa dhidi ya Chadema na polisi kuiingizwa kwa kujua au kutokujua katika mtego huo,” alisema Dk. Slaa.

Alisema si nia ya Chadema kuingilia upelelezi wa polisi katika suala la Lwakatare, lakini ni imani ya chama hicho kwamba sheria na taratibu zinazozingatia katiba inayolinda haki za mtu zitafuatwa.

Dk. Slaa alisema tukio la kukamatwa Lwakatare na kuhusishwa kupanga njama za kumdhuru mwandishi na picha kuwekwa kwenye mitando ya kijamii linaweza likawa limepangwa na vyombo vya usalama.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso licha ya kukataa kutoa ufafanuzi kuhusiana na maendeleo ya uchunguzi dhidi ya Lwakatare kwa siku ya jana, alisema vyombo vya usalama haviwezi kuhusika kupanga njama hizo.

Juzi Jeshi la Polisi kupitia kwa Senso, lilisema limemkamata Lwakatare ili kuchunguza taarifa zilizosambazwa dhidi yake kwenye mitandao zinazohatarisha uvunjifu wa amani nchini.

Kwa upande wake Dk. Slaa,  alisema juzi mchana maofisa watatu kutoka makao makuu ya polisi walifika katika makao makuu ya chama hicho wakimtafuta Lwakatare na kueleza kuwa wana shida ya kutaka kuonana naye na kwamba kwa kuwa alikuwa anawafahamu maofisa hao, aliwaruhusu kuonana naye.  Baada ya dakika chache, maofisa hao walirudi tena kwa Dk. Slaa na kueleza kuwa wanaomba kuondoka na Lwakatare kwenda makao makuu ya jeshi hilo kwa ajili ya mahojiano.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment