Saturday, February 9, 2013

Wapinzani kutua Dar kwa kishindo


WAUNGANA KUPINGA UONEVU BUNGEN
MAPOKEZI makubwa yanawangoja wabunge wa vyama vya upinzani kesho, watakapowasili wakitokea bungeni Dodoma na kisha kufuatiwa na mkutano mkubwa wa hadhara utakaofanyika katika viwanja vya Temeke Mwisho jijini Dar es Salaam.
Wabunge hao wakiongozwa na wale wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanapokelewa kama mashujaa waliokataa vitendo vya uonevu na udhalilishaji vilivyofanywa na Spika Anne Makinda na Naibu wake Job Ndugai kwa madai kuwa wanalitumia Bunge kama kijiwe cha kupitishia masuala ya serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), badala ya kuwatetea wananchi.
Taarifa ya mapokezi na mkutano huo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Oganaizesheni na Mafunzo wa CHADEMA, Benson Kigaila, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana.
Alisema wabunge hao watapokewa katika eneo la Ubungo na kisha msafara wa magari na pikipiki utaenda hadi Tazara na kufuatiwa na maandamano ya miguu hadi Temeke Mwisho kutakapofanyika mkutano huo.
Kigaila alisema wameshawaandikia barua ya mwaliko viongozi wote wa vyama vya upinzani, wakiwaomba washiriki katika maandamano na mkutano huo kwa kuwa Bunge limekuwa halitetei tena maslahi ya wanyonge kama matarajio ya Watanzania wengi yalivyokuwa awali.
Mkutano huo utakuwa mwanzo wa mikutano mingine mingi kwa ajili ya kuwashitaki wabunge wa CCM, wakiongozwa na Spika Makinda kwa kutumia wingi wao kukandamiza haki za msingi za Watanzania.
NCCR-Mageuzi waunga mkono
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura, alisema hajapata taarifa ya mwaliko wa mkutano na maandamano hayo ila akasema kama yatakuwa na tija kwa taifa watashiriki.
Sungura alisema wao hawana ugomvi na chama kingine chochote cha siasa nchini zaidi ya CCM, hivyo kama kuna watu wanaona njia nzuri ya kuiondoa madarakani ni kushirikiana, wao wapo tayari.
“Nipo safarini sijapata taarifa hizo, ngoja niwasiliane na watu ofisini, ila sisi mbaya wetu ni CCM tu na siyo vyama vingine, hivyo tunaweza kuungana nao,” alisema Sungura.
Mrema aivutia pumzi
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Taifa wa TLP, Augustino Mrema, alisema anasubiri Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge itoe taarifa yake kwa spika na baada ya hapo waangalie majibu na uamuzi wa spika kama utaendelea kuwa wa kuligawa taifa.
“Jana tulikuwa na kikao na vyama vyote vyenye wabunge pamoja na waziri mkuu, na tulikubaliana namna ya kutatua matatizo ya ndani ya Bunge, ila pia ninasubiri uamuzi wa Kamati ya Maadili na Madaraka ya Bunge na kisha uamuzi wa Spika kwa kuwa leo ndio utaelezwa bungeni,” alisema Mrema.
Hata hivyo, kamati hiyo katika ripoti yake iliegemea na kuitetea serikali pamoja na kiti cha spika, huku ikielekeza mashambulizi zaidi kwa wabunge wa upinzani, hususan wa CHADEMA.
CUF waishangaa CHADEMA
Hata hivyo, Chama cha Wananchi (CUF), kimejinadi kikidai kuwashangaa CHADEMA kutaka kuwashirikisha katika maandamano hayo, kwa vile wanajua kuwa hiyo ni ngome yake.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro, amesema kuwa CHADEMA kinajichanganya baada ya kuona hawatapata uungwaji mkono katika Wilaya ya Temeke, na kwamba hawawezi kushiriki kwa vile wamekuwa wakiitwa CCM B.
“Mimi siwaelewi hawa CHADEMA, katika mambo mengine wanatuita sisi CCM B, wakitaka kwenda katika ngome yetu wanatualika,” alisema Mtatiro na kuongeza kuwa, wao hawatashiriki kama chama, bali hawawezi kuwazuia wafuasi wao kwenda kusikiliza mkutano huo.
Mnyika airarua serikali
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amewahimiza Watanzania kuzinduka katika usingizi wa pomo na kuiondoa CCM madarakani kwa sababu imeanza kutumia mabavu na hila kubaki katika uongozi.
Akihutubia katika mkutano mkubwa uliofanyika mjini Dodoma juzi, Mnyika alitoboa siri ya kuzimwa kwa hoja yake binafsi kuhusu sakata la maji jijini Dar es Salaam kwa vile ingeivua nguo serikali.
Mnyika alisema Spika wa Bunge alitaka kuficha ufisadi mkubwa unaofanywa na serikali katika miradi mingi ya maji hapa nchini.
Alisema kutokana na spika na naibu wake kuzima hoja za wabunge wa upinzani, sasa CHADEMA kitazunguka nchi nzima kutoboa ukweli wote ili wananchi watoe hukumu kwa serikali.
Mnyika alisema inasikitisha kuona nchi inatafunwa na baadhi ya watu wachache serikalini kwa maslahi binafsi na kuliacha taifa likiangamia.
“Nataka nikuambie hoja yangu ilikuwa ni ya siku nyingi na ilipitia vigezo vyote, lakini cha kushangaza wanasema haikufuata vigezo vinavyotakiwa,” alisema Mnyika.
Mkutano huo uliwekewa zuio na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi kwa madai kuwa kama mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa hakuona umuhimu wa kufanyika.

No comments:

Post a Comment