Saturday, February 9, 2013

Pareso ahoji mapato ya utalii


MBUNGE wa Viti Maalumu, Cecilia Pareso (CHADEMA) ameitaka serikali ieleze halmashauri ambazo zipo karibu na sehemu za utalii zinavyonufaika na mapato ambayo yanapatikana kutokana na sekta hiyo.
Pareso alitaka kupatiwa maelezo hayo jana bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza kwa kuitaka serikali kueleza iwapo halmashauri hizo zinafaidika kutokana na makusanyo yanayotokana na utalii.
Pia alitaka kujua kama serikali inatoa gawio lolote kwa halmashauri ambazo zipo karibu na vyanzo vya utalii, ili ziweze kunufaika kutokana na mapato yanayokusanywa.
Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Magogoni, Kombo Khamisi Kombo (CUF), alitaka kujua Tanzania inaingiza mapato kiasi gani ikilinganishwa na vituo vingine vilivyoko nchi nyingine wanachama.
Aidha, alitaka kujua ni wastani wa watalii wangapi wanaoingia nchini kila mwaka.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Chakula na Ushirika, Adam Malima kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema jumla ya dola bilioni 6.3 zilipatikana katika kipindi cha mwaka 2007 hadi 2011 kupitia njia ya utalii ambapo kwa kipindi hicho watalii 3,854,467 walifika.

No comments:

Post a Comment