TAMKO
LA BAVICHA KUHUSIANA NA MATOKEO MABOVU YA KIDATO CHA NNE KWA MWAKA 2012
Kama muhimili wa vijana na masuala
ya vijana nchini, Baraza la Vijana wa CHADEMA, BAVICHA limeshtushwa na
kufedheheshwa na matokeo mabovu ya Kidato cha Nne ya mwaka 2012 yaliyotangazwa
siku chache zilizopita na Waziri wa elimu Nchini.
Mshtuko huu unatokana na ukweli kuwa
94% ya wanafunzi wote waliofanya
mtihani wamefeli vibaya sana na haijawahi kutokea katika historia ya elimu
nchini.
Ikumbukwe kupanda kwa kasi kiwango
cha kufeli kwa wanafaunzi wa kidato cha nne mwaka huu ni muendelezo wa kushuka
kwa kiwango cha ufahulu ambacho mtiririko wake unaanzia mwaka 2006.
Haya ni matokeo ya kupuuzwa kwa
sauti za mashirika yasiyo ya kiserikali na wadau wa elimu ambao tumekuwa tukipiga
kelele kuhusu hatma ya elimu ya nchi huku serikali ikibeza sauti hizo. Tafiti
nyingi zimefanyika, mapendekezo mengi yametolewa lakini serikali daima imekuwa
kiziwi juu ya tafiti na mapendekezo hayo
SABABU
KUU YA MATOKEO MABOVU
BAVICHA inatambua kuwa matokeo haya
mabovu kuwai kutokea Tanzania yanatokana na sababu moja kuu ambayo ni UDHAIFU wa serikali ya CCM. Kwa udhaifu
huo, serikali hii;
·
Haijatambua umuhimu wa haki ya
elimu kwa watoto na vijana wa Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii.
·
Imeshindwa
kuweka miundombinu na mazingira wezeshi ya kutoa elimu bora kwa raia wake
·
Imeshindwa
kutambua waalimu ni injini muhimu kwa Maendeleo ya nchi na hivyo kuwapuuza na
kuwadharau siku zote
·
Imeamua
kukumbatia mfumo wa elimu ambao uharamia wake ndio matokeo haya ambayo kwayo
maisha ya vijana yanaharibika
·
Imeshindwa
kufuatilia kwa ukaraibu matokeo ya tafiti mbalimabli za mashirika yasio ya
kiserikali ambazo zimekuwa zikionyesha ubovu wa sekta nzima ya elimu na pia
kupendekeza hatua za kuchukuliwa.
ATHARI
ZA MATOKEO HAYA
1. Wanafunzi
344,210 waliopata madaraja ya IV na 0 wanaungana na wenzao 481,295 walifeli
darasa la saba mwaka 2008 na hivyo kufanya kundi hili lililoanza darasa la
kwanza mwaka 2002 kuzalisha jumla ya vijana 825,505 wasioajirika popote kwa
kuwa hawana ujuzi wala elimu ya kukidhi vigezo vya kuajiriwa.Kwa elimu ya
Tanzania ilivyo, kundi hili halina hata uwezo wa kujiajiri kwa vyovyote vile.
2. Kwa kuwa
wanafunzi waliopata madaraja ya I,II na III ambao ndio wenye vigezo vya
kujiunga na kidato cha tano na sita ni 23,520,
ni wazi kuwa baadhi ya shule zitakosa wanafunzi wa ngazi hizo kwani uwezo uliopo wa kudahili wanafunzi kwa ngazi hiyo ni
zaidi ya wanafunzi 50000.
3.
Vyuo vikuu navyo kwa mwaka mwaka 2015 vitakosa
wanafunzi wa kudahili kwani ni wazi kuwa kundi hili litalojiunga na kidato cha
tano litachujika kutokana na wale watakaofeli kwa kuwa mazingira yanatoa mwanya
huo ukiachilia mbali wale watakaoshindwa kujiunga na ngai hiyo kwa matatizo ya
ada na nk. na hivyo kuchangia kukosekana kwa wataalamu ambao watakuwa
wanahitajika kuzalishwa kwa wakati huo.
Vyuo vikuu nchini vinadaili wanafunzi zaidi ya 65,000 kwa mwaka wakati wanafunzi watakaokuwepo ni chini ya 23,520 hivyo kuvitia hasara vyuo hivyo
kwa wakati huo. Kwa hali hii, serikali ya CCM haiwezi kufikia lengo lake la
kudfikisha wanafunzi zaidi ya 300,000
ifikapo 2015 kama ilivyoahidi.
4. Kwa hali
hii, ni ukweli usiofichika kuwa serikali ya CCM haiwezi kufikia lengo la kuwa
na Taifa lililoelimika ifikapo 2025 kama inavyobainishwa kwenye dira (Vision 2025)
na badala yake itafanikiwa kuwa na Taifa la watu mbumbumbu kwa wakati huo
5. Kutokana na
serikali dhaifu iliyopo madarakani kushindwa kubuni vyanzo vya ajira ili kuweza
kuajiri watu wake wenye taaluma, ujuzi na wasio na ujuzi, ni dhahiri kuwa
vijana hawa zaidi ya 800,000 watakuwa wanajihusisha na vitendo viovu kama
ukabaji, madawa ya kulevya, wizi na ujambazi pamoja na ukahaba na hivyo kuwa na
jamii ya watu waovu daima
HATUA
ZA KUCHUKUA
1. BAVICHA
tunaitaka serikali kutangaza hali hii kuwa ni janga la Taifa na hivyo hatua za
haraka kama vile, kutangaza sasa elimu bora ndio kipaumbele cha serikali kwa
raia wake, kuboresha bajeti ya elimu ikiwemo kuboresha maslahi ya walimu na
mazingira yao ya kufanya kazi.
2. Kama suala
la uharaka na la kutatua tatizo moja kwa moja, ni lazima kufumua mfumo wa elimu
uliopo na kuhakikisha tunakuwa na mfumo unotambua vipaji vya watu na
kuviendeleza kuliko kuendelea na huu wa kulazimisha elimu ya kukariri.
Licha ya
mfumo huo, ni vema sasa wakaguzi wa shule wakapewa meno ya kuchukua hatua pale
wanapobaini mambo hayaendi sawa kwenye baadhi ya shule kwani ni wazi kuwa kuna
shule ambazo hazikidhi viwango vya kuitwa shule lakini bado zinaachwa kuendelea
kuitwa shule.
3. Kama sehemu
ya uwajibikaji, BAVICHA inasisitiza kuwa Waziri, Katibu Mkuu pamoja na
Mkurugenzi wa elimu ya Sekondari wajiuuzulu mara moja ndani ya siku 14 kama
ilivyokwisha tangazwa na chama.
4. Wananchi
wanapaswa kuzingatia ukweli kuwa serikali ya CCM imeshindwa kutekeleza ahadi
yake ya kutaka ufahulu kwa madaraja ya I, II na III kufikia asilimia 70 ifikapo
2009. Tumeshapita 2009 na leo hii ufahulu kwa madaraja hayo ni 6% tofauti 37% ya mwaka 2004. Suluhisho pekee hapa ni kuiondoa CCM madarakani
kwa kuwa imeshindwa kutekeleza ilani yake na pia kushindwa kuisimamia serikali
yake dhaifu.
5. Wakati
tunasubiri CCM kungo’oka madarakani Mwaka 2015, BAVICHA tunaagiza viongozi wa Wilaya na Mikoa
kufanya mawasiliano na vijana ambao
wamekumbwa na kadhia hii ili washiriki maandamano tutakayoyaandaa kwa lengo la kuishinikiza serikali iliyoharibu
maisha yao;
·
Kumtaka
waziri, Katibu Mkuu wa Wizara na Mkurugenzi wa Sekondari kujiuzulu iwapo
hawatakuwa wamefanya.
·
Kuishinikiza
serikali sasa ifanye kipaumbele kuwa elimu bora kwa raia wake na hivyo pamoja
na mambo mengine kuhakikisha walimu bora wanapatikana, bajeti ya elimu
inaongezeka ikiwa ni pamoja na kuongeza mishahara na marupurupu ya waalimu
kuanzia na bajeti ya mwaka 2013/2014
·
Kuitaka
serikali ya CCM ieleze hatma ya maisha ya vijana waliofelishwa na mfumo mbovu
wa elimu inaousimamia
6. BAVICHA, tutawaagiza
wabunge wetu vijana kuhakikisha kwenye vikao vijavyo vya bunge, Serikali inatoa
hatma juu ya janga hili la kitaifa na majibu muafaka juu ya hatma ya malaki ya
vijana waliofelishwa na vile vile kuhakikisha wanayapa masuala yote ya elimu kipaumbele
namba moja kwenye mijadala ya kibunge
7.
Aidha, BAVICHA
katika vikao vyake vikubwa viwili vilivyopita iliona tatizo hili na kuamua
kuunda kamati ndogo kuangalia sekta nzima ya elimu inavyoathiri hali za Vijana
nchini na kuja na mapendekezo yake. Kwa hatari hii ya Matokeo ya Kidato cha
nne, kamati hii itazingatia hali hiyo na kupanua wigo wa kazi zake.
Imetolewa leo tarehe 21/02/2013, Jijini Dar es
salaam na;
Deogratias Munishi
Katibu Mkuu – BAVICHA
No comments:
Post a Comment