TAARIFA KWA UMMA
KIKAO CHA KAMATI YA URATIBU WA KANDA NA UZINDUZI WA KANDA YA KASKAZINI
Kufuatia
azimio na maamuzi ya Baraza Kuu la CHADEMA lililofanyika hivi karibuni jijini
Dar es Salaam, iliamuliwa kuwa chama kishushe mamlaka ya uendeshaji kwenye
mfumo wa kanda kama zilivyogawanywa.KIKAO CHA KAMATI YA URATIBU WA KANDA NA UZINDUZI WA KANDA YA KASKAZINI
Itakumbukwa kuwa azimio hili ni sambamba na sera ya CHADEMA kuhusu mfumo mpya wa utawala (majimbo) na mapendekezo ya chama kwa tume ya mabadiliko ya katiba kuhusu kuigawanya nchi katika majimbo 10 ya kiutawala/kiserikali.
Katika mgawanyo huu, Kanda ya Kaskazini ilipangwa kuwa na mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara.
Mkoa wa Arusha ulichaguliwa kuwa makao makuu ya Kanda ya Kaskazini.
Tarehe 16 na 17 Februari 2013 kutakuwa na kikao cha kwanza cha Chama Kanda ya Kaskazini ambacho kitajumuisha wabunge wote kutoka mikoa ya kanda hii, akiwemo Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Mh. Freeman Mbowe (KUB), viongozi wa chama wa mikoa.
Pia kitahudhuriwa na Wenyeviti na Mameya wa halmashauri zinazoongozwa na CHADEMA pamoja na wajumbe wa Kamati Kuu ya chama, wanaoishi kwenye kanda ya kaskazini pamoja na mwasisi wa CHADEMA Mzee Edwin Mtei.
Aidha siku ya tarehe 17 Februari kikao kitajumuisha viongozi kutoka majimbo yote ya Kanda ya Kaskazini, takribani majimbo 30 na kuleta wajumbe zaidi ya 200 katika Jiji la Arusha.
Siku hiyo hiyo ya tarehe 17 Februari tutakuwa na uzinduzi wa kanda yenyewe na kuitambulisha timu ya uratibu, utakaohitimishwa na mkutano mkubwa wa hadhara.
Tunawaomba wananchi/wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini wajitokeze kwa wingi sana kwa ajili ya uzinduzi wa kanda yao hii na pia kuunga mkono mpango huu wa chama ambao mbali ya kukifanya chama na viongozi kuwa karibu zaidi na wananchi pia katika kufanya shughuli za kisiasa kwa ufanisi wa hali ya juu na kwa kiasi kikubwa umeshusha madaraka na mamlaka ya uendeshaji na usimamizi wa chama kwa watu ngazi ya chini.
Imetolewa leo tarehe 13 Februari 2013.
Arusha.
Amani Golugwa
KNY: Kamati ya Muda ya Uratibu
KANDA YA KASKAZINI (TANGA, KILIMANJARO, ARUSHA & MANYARA)
No comments:
Post a Comment