Bunge linatarajia kufuta utaratibu wa kurusha matangazo ya moja kwa moja kupitia televisheni kwa madai ya kukomesha vitendo vya baadhi ya wabunge kukiuka kanuni za bunge na kuleta vurugu kwa kutafuta umaarufu bila kujua kwamba tabia hiyo inaleta picha mbaya katika jamii.
Hayo yalisemwa na Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila jijini Dar es salaam jana wakati akitoa taarifa ya mapendekezo ya kuanzisha kamati ya bajeti na kuvunjwa kwa baadhi ya kamati za bunge.
Alisema ili kuleta maadili kwa baadhi ya wabunge ambao wamekuwa wanashindwa kufuata kanuni za bunge na kutumia nafasi kutafuta umaarufu kwa sasa wameomba kufutwa utaratibu wa kurusha matangazo ya bunge ya moja kwa moja badala yake watarekodi ili kuondoa hoja zisizokuwa za msingi.
Aliongeza kuwa kuna idadi kubwa ya wabunge wamekuwa wakikiuka kanuni za bunge makusudi na kusababisha kuleta vurugu bungeni wakati jamii ikiendelea kutazama mabishano yasiyokuwa na hoja za msingi.
Dk. Kashilila alisema kuwa kwa sasa kuna baadhi ya kamati za bunge ambazo zimevunjwa kutokana na baadhi ya kamati hizo kuingilia katika utendaji jambo ambalo limekuwa likipoteza maana ya kamati hizo.
Hivi karibuni baadhi ya kamati ikiwemo ile ya Mashirika ya umma POAC zimefutwa na kuacha maswali mengi kwa baadhi ya wananchi juu ya hatua hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment