Saturday, February 23, 2013

Siri za kufeli hizi hapa


CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebainisha baadhi ya siri za matokeo mabaya ya wanafunzi waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka jana kuwa ni pamoja na utoro wa walimu katika vituo vyao vya kazi na wahitimu wa ualimu kukimbia fani hiyo.
Kwa mujibu wa  Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo (CHADEMA) walimu wamejikuta katika hali hiyo kutokana na ukata wa maisha unaowakabili hali hiyo ikishusha ubora wa elimu nchini na lawama za matokeo hayo zinakwenda moja kwa moja kwa serikali.
Na katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto amesema Waziri wa Elimu Dk. Shukuru Kawambwa na uongozi wa juu wa wizara yake wanapaswa kujiuzulu na wizara hiyo ihamishiwe Ofisi ya Rais.
Maelezo ya Lyimo
Lyimo, Mbunge wa Viti Maalumu- CHADEMA, katika mazungumzo yake na waandishi wa habari jana Jumanne, Makao Makuu ya CHADEMA, alisema kutotulia kwa walimu katika vituo vyao vya kazi kutokana na hali mbaya za maisha, ndicho chanzo cha wanafunzi wengi wa kidato cha nne kufanya vibaya katika mitihani yao ya kitaifa.
Alisema walimu wengi wanatumia muda wa kazi kufanya shughuli zao binafsi zitakazowaongezea kipato kwa sababu Serikali haiwalipi mishahara kwa wakati.
Kwa mujibu wa waziri huyo kivuli, sababu hiyo na nyingine, ndizo zinazowafanya pia baadhi ya watu wengi waliosomea ualimu kuhama fani hiyo na kwenda kufanya kazi nyingine zenye kuwaingizia kipato kizuri kuliko ualimu.
“Kusema walimu ni wachache ni uongo wa hali ya juu. Walimu wapo wengi, lakini wanakimbilia fani nyingine zenye maslahi zaidi. Ukitembea katika ofisi mbalimbali utakutana na wafanyakazi wengi waliosomea ualimu. Lakini hawataki kufundisha kwani maslahi ni madogo sana hayakidhi mahitaji ya kila siku,” alisema Lyimo na kuongeza:
“Sekta ya elimu ndiyo sekta pekee serikalini ambayo wafanyakazi wake wanaweza kukaa miezi mitatu bila  mshahara. Katika hali hii unadhani ni mwalimu gani atakubali kukaa darasani afundishe wakati maisha yake ni mabaya?
“Suluhisho pekee la kukuza kiwango cha elimu nchini ni kuboresha maslahi ya walimu kwa sababu wengi wanaopelekwa vijijini, hawakai katika vituo vyao vya kazi kutokana na hali mbaya ya maisha na hata walimu walio mjini wanajishughulisha na biashara katika maeneo ya shule, hatuwezi kufika kwa hali hii.”
Aidha, alitofautiana na mbunge wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi) kwa kuweka wazi kuwa mitaala ya kufundishia ipo, lakini hailingani na uwezo wa mwalimu kwani kwa kiasi kikubwa walimu hawashirikishwi katika kuiandaa mitaala hiyo na ndiyo maana wanafundisha tofauti na mitaala inavyoeleza.
“Matokeo haya pia yanasababishwa na utaratibu mbaya wa kuandaa mitaala ya kufundishia. Labda niweke wazi, mitaala ya kufundishia ipo lakini walimu hawashirikishwi katika kuiandaa unadhani watawafundisha nini wanafunzi.
“Mathalan, kuna somo jipya la teknohama linalohusu teknolijia ya habari, mwalimu anapewa hili somo afundishe wakati hajahudhuria semina wala kukaa darasani kusoma kuhusiana na mambo ya teknohama, unatarajia nini?” alihoji Lyimo.
Kwa mujibu wa Lyimo chama hicho kikuu cha upinzani nchini kitazindua sera yake ya elimu mapema mwezi ujao  na mambo makubwa watakayoyaainisha katika mpango mkakati ni pamoja na kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi chuo kikuu kwa kutumia raslimali zilizopo nchini.
Kauli ya Zitto
Kwa upande wake, Zitto Kabwe katika mazungumzo yake na mwandishi wetu alisema Waziri na uongozi wa juu wa Wizara ya Elimu unapaswa kujiuzulu kutokana na matokeo hayo mabaya na zaidi ya hapo, wizara hiyo ihamishiwe chini ya ofisi ya rais.
“Wizara hii inabidi kuihamisha iwe chini ya Rais na Rais aelezwe wazi kwamba kazi yake ni kuhakikisha kiwango cha kufaulu na ubora wa elimu nchini vinaongezeka, asipoweza basi aachie ngazi,” alisema Zitto.
Wadau wengine wa elimu nchini wamekosoa umakini wa serikali katika usimamizi wa sekta ya elimu nchini wakidai serikali ndiyo iliyochangia kushuka kwa elimu na hasa matokeo ya sasa ya kidato cha nne.

Maoni hayo yametolewa katika wakati ambao tayari matokeo ya matokeo mitihani ya kidato cha nne kwa mwaka huu, yakiwa yamekwishatangazwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa.
Katika matokeo hayo, asilimia 60 ya watahiniwa walipata daraja sifuri, matokeo ambayo yameelezwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kutokea nchini.

Raia Mwema

No comments:

Post a Comment