Saturday, February 23, 2013

Chadema yafukuza madiwani wake wawili

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Wilaya ya Musoma, kimewavua uanachama madiwani wake wawili wa viti maalumu, kutokana na utovu wa nidhamu.

Kutokana na uamuzi huo, ni wazi kuwa madiwani hao sasa wamepoteza sifa ya kuwa madiwani na wajumbe wa halmashauri ya wilaya hiyo. 

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mwenezi wa chama hicho Wilaya ya Musoma, Meshack Ntongoni alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kuketi jana.

Katika kikao hicho wajumbe wa kamati hiyo waliazimia kuwavua uanachama madiwani wawili hao kwa mujibu wa wa ibara ya 4.

Ntongoni aliwataja waliovuliwa uanachama kuwa ni Habiba Ally Zedy na Miriamu Daudi Chacha, ambao wamekuwa wakionywa mara kwa mara kutokana na mwenendo wao mbaya ndani ya chama.

“Madiwani hawa tumekuwa tukiwaandikia barua mara kwa mara juu ya mwenendo wao wa utovu wa nidhamu ndani ya chama na kwa viongozi na wamekuwa wakikaidi, hivyo Kamati Tendaji imeamua kuchukua hatua kwa mujibu wa katiba.

“Hiki ni chama ambacho viongozi wanapaswa kufuata utaratibu kwa mujibu wa katiba na hatutaweza kumvumilia kiongozi ama mwanachama yeyote ambaye atakwenda kinyume na katiba yetu,” alisema.

Mwenezi huyo pia aliwataja madiwani waliopewa barua za onyo ni pamoja na Meya wa Manispaa ya Musoma (CHADEMA), Alex Kisurura ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyamatare.

Wengine ni Diwani wa Kata ya Kitaji, Haile Siza Tarai ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji na Diwani wa Kata ya Kamunyonge Angela lima.

Alisema kamati hiyo ilichukua jukumu la kuwafuta uanachama kwa kufuata katiba ya chama ibara ya 5 kifungu cha nne na cha tatu na vifungu vingine.

Alisema madiwani hao waliovuliwa uanachama wamekosa pia sifa ya kuwa madiwani kufuatia taratibu, kanuni na sheria za katiba ya chama kwamba endapo mwanachama atapoteza sifa ya kuwa mwanachama, pia anapoteza sifa za kuwa kiongozi katika ngazi yoyote aliyokuwa akiishikilia.

Alidai kuwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka 2010, hali ya chama hicho jimboni hapo ni tete kufuatia kutoelewana wao kwa wao hali inayokifanya chama hicho kukosa mwelekeo.

“Tangu Chadema tulipochukua jimbo hili (Musoma Mjini), tumekuwa na wakati mgumu sana hasa ya utovu wa nidhamu, hali hii itatupeleka pabaya, hivyo tumeamua kuanza kuwadhibiti kwa kutumia makali ya katiba ili kukinusuru chama,” alisema.


Mtanzania

No comments:

Post a Comment