Monday, February 18, 2013

Seif awashukia Makinda, Ndugai


KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamadi amesema kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limejaa uonevu, upendeleo, ubaguzi na fitina kutokana na utawala mbovu wa Spika Anne Makinda na Naibu wake, Job Ndugai.Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alibainisha kuwa gaidi namba moja wa Watanzania si Osama bin Laden bali ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) na viongozi wake kutokana na kushindwa kutatua kero zilizopo.
Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mkutano wa Operesheni Mchakamchaka (V4C) uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa wa chama hicho, akiwemo Mwenyekiti wake, Prof. Ibrahim Lipumba.
Seif aliliponda Bunge, akiliita ni la kihuni na kwamba kwa takribani miaka 50 iliyopita, kikao kilichomalizika hivi karibuni ndicho kimedhihirisha upeo wake katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi, hasa serikali inapokuwa haina majibu.
“Katika mazingira ya uonevu, upendeleo, ubaguzi na utengano hasa wa kipato, dhuluma na fitina unaotokana na utawala mbovu, huwezi kuwa na taifa huru, tulivu na lenye amani. Tuseme nchi yetu ni wastahimilivu sio utulivu…utulivu utakuja wenyewe pale Watanzania watakapokuwa na haki sawa,” alibainisha.
Seif alifafanua kuwa, sasa hivi kuna mgawanyo wa kidini, ukabila na mikoa kutokana na kutokuwepo mgawanyo sawa wa rasilimali za umma.
Akiunga mkono madai ya wananchi wa Mtwara juu ya gesi iliyopatikana katika mikoa ya kusini, Seif alisema hiyo ni sadaka inayowapasa kuanza kuwanufaisha wao kwanza, huku akibainisha kuwa wamefikia hapo kutokana na historia ya utawala wa chama kilichopo madarakani.
“Watu hawa wako sahihi na wasipuuzwe! Unajua serikali makini haiwezi kupishana na watu inaowaongoza na kwa mambo kama haya serikali inapaswa kutoa upendeleo maalumu kwa wanyonge ili kuwawianisha kiuchumi na si vinginevyo,” alifafanua.
Naye Prof. Lipumba alionesha kusikitishwa na serikali kushindwa kuutumia mkoa huu kama kitovu cha uchumi wa nchi kutokana na kuwa na uoto wa ardhi unaofaa kwa kilimo na maji ya kutosha.
“Ni mkoa wenye ardhi kubwa yenye rutuba, maji ya kutosha, chanzo cha nguvu ya umeme, mbuga za wanyama tatu, vyuo vya kutosha vya taaluma…kwa kweli hakuna sababu wananchi wa mkoa huu kuwa masikini wa kutupwa,” alisema.
Alisema Serikali ya CCM haina mwelekeo wa kuwawezesha Watanzania kuukabili umasikini, huku akidai kuwa inashangaza kuona vyanzo vya umeme vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 5,000 ambayo vingeweza kuongeza kasi ya ujenzi wa viwanda na ongezeko la ajira kwa vijana, badala yake umeme unaozalishwa ni megawati 560 tu.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment