Monday, February 18, 2013

Mnyika amshukia Waziri Maghembe


MBUNGE wa Ubungo, John Mnyina (CHADEMA) amemshukia Waziri wa Maji, Prof. Jumanne Maghembe, akisema kauli zake kwenye mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) juzi, kuhusu hali ya upatikanaji maji katika Jiji la Dar es Salaam, zimedhihirisha udhaifu wa serikali na chama chake.
Mnyika alisema kuwa Maghembe alirudia maelezo aliyoyasema bungeni kuwa serikali imejiandaa kuhakikisha kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unakuwa na maji ya kutosha, na kwamba katika mpango wake wa muda mfupi hadi kufikia Aprili 2014 maji yatakuwa ya kutosha.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema kuwa alitarajia CCM na Waziri Maghembe wangetumia mkutano huo kuwaeleza wananchi sababu za ahadi ya mwaka 2005 ya chama hicho, kwamba tatizo la maji jijini humo lingemalizika mwaka 2010 kwa wananchi asilimia 90 kupata maji badala ya kutoa ahadi mpya.
“Serikali ya CCM ilishindwaje kutekeleza na badala yake hali kuwa mbaya zaidi? Wananchi wa Dar es Salaam wana kila sababu ya kuendelea kulaani hatua ya Naibu Spika Job Ndugai na Waziri Maghembe kukiuka kanuni ya 57 (4) na 58 (5), ambazo zinakataza mabadiliko ya hoja yenye kupingana na hoja ya msingi, na haziruhusu mbunge mwingine yeyote kuondoa hoja bungeni, isipokuwa mtoa hoja mwenyewe,” alisema.
Mnyika alifafanua kuwa, wananchi wa Dar es Salaam na Watanzania wakumbuke kuwa upatikanaji wa maji katika jiji hilo wakati wa ukoloni ulikuwa wastani wa asilimia 68, lakini miaka 51 ya utawala wa CCM jiji limerudi nyuma, na sasa upatikanaji ni wastani wa asilimia 55, tena kwa mgawo mkali.
“Waziri Maghembe kwa kueleza kwamba tatizo la maji litamalizika Aprili 2014, anapaswa kukiri kwa wananchi kwamba Rais Kikwete hakuwaeleza ukweli wananchi wa Dar es Salaam alipodai kuwa tatizo hilo litakuwa historia Februari 2013,” alisema.
Mnyika aliongeza kuwa, inaelekea CCM iko katika wakati mgumu hadi inafikia hatua ya kupandisha kwenye jukwaa lake mawaziri wa serikali na kutoa maneno ya kipuuzi kama hayo yaliyotolewa na Waziri Maghembe.
Katika hotuba yake kwenye mkutano huo wa CCM, Maghembe alisema kuwa Mnyika anatakiwa kutosherehekea mimba wakati mwenye mtoto ni CCM, kwamba serikali ya chama hicho ndiyo imeweka miradi iliyopo katika Jimbo la Ubungo na inaiendeleza.
“CCM na Waziri Maghembe wanashindwa kabisa kutambua kwamba miradi ya maendeleo ni kodi za wananchi, na kwamba wajibu wa mbunge ni kuwawakilisha na kuisimamia serikali ili fedha za kodi zao zielekezwe kwenye miradi muhimu ya maendeleo,” alisema.
Mbunge huyo alisisitiza kuwa, yafaa wananchi kufahamu kuwa hata ahadi hiyo ya maji kupatikana Aprili 2014 ni kiini macho kwa kuwa Waziri wa Maji alitoa maelezo yenye kulidanganya Bunge.
Mnyika alirejea msimamo wake kuwa imebakia wiki moja aweze kutangaza utaratibu wa maandamano ya kwenda Wizara ya Maji kudai uwajibikaji, hatua za haraka za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.
Alisema kuwa alitoa wiki mbili tangu Februari 10 mwaka huu, kwa Waziri wa Maji kujitokeza na kutoa majibu kwa umma, kwamba hata hivyo majibu aliyoyatoa mwishoni mwa wiki kupitia mkutano wa CCM hayajakidhi matakwa ya hoja binafsi aliyoiwasilisha bungeni.
“Waziri Maghembe kama alivyolipotosha Bunge, amerudia kutoa maelezo yasiyokuwa ya kweli, kwamba hoja binafsi niliyoiwasilisha bungeni tayari ni sehemu ya mpango wao na inafanyiwa kazi na serikali,” alisema Mnyika.

No comments:

Post a Comment