MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ameibana serikali na kuitaka ieleze ni kwanini inashindwa kuweka wazi matumizi ya miradi mbalimbali inayofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa ikiwa ni pamoja na ufisadi wa Kampuni ya Meremeta.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni jana, Mnyika alisema kuwa licha ya kuwa mambo ya jeshi yanahitaji usiri kama vile ununuzi wa silaha na mambo mengine lakini kwanini serikali inashindwa kuweka wazi mapato na matumizi yanayotokana na jeshi hilo.
Awali katika swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) alitaka kujua ni kwanini bajeti za wizara zinazohusu ulinzi na usalama zinasomwa hadharani.
Pia alitaka kujua licha ya bajeti hizo kusomwa hadharani ni kwanini hazipewi kipaumbele.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Pereira Ame Silima, alisema mambo ambayo hayahusu masuala ya kiusalama na silaha yanawekwa hadharani.
“Si kweli kuwa mapato na matumizi ya jeshi hilo hayajadiliwi, yanaweza kujadiliwa na unaweza kukumbuka kuwa baadhi ya viongozi wa jeshi hilo ambao walionekana kutofanya mambo ambayo ni mazuri wamechukuliwa hatua.
“Kama kuna ubadhirifu unaweza kufanyiwa kazi, kwani hilo halizuiliwi kufanyika na kinachokuwa siri ni matumizi ya silaha na mambo mengine ya kiusalama zaidi,” alisema Silima.
Alisema kwa kuwa bajeti za shughuli za ulinzi na usalama ni sehemu ya matumizi ya umma ambayo hutumia fedha kutoka mfuko mkuu wa serikali, ni lazima zipitie mkondo wa kisheria.

No comments:
Post a Comment