Sunday, February 17, 2013

Mkakati mpya CHADEMA waitisha CCM


KASI ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) bungeni, na mkakati mpya wa kuendesha chama hicho kupitia utawala wa majimbo yaliyomo ndani ya kanda kumi, imeelezwa kuitisha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Sambamba na hilo, chama hicho tawala kimedaiwa kutishika na jinsi CHADEMA ilivyojipanga kwa kununua pikipiki zaidi ya 300 na kuzisambaza nchi nzima, magari na vifaa vingine kama nyenzo za kueneza chama kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Kanda hizo na mikoa yake kwenye mabano ni Mashariki/Dar es Salaam (Dar es Salaam na Pwani), Kusini (Lindi na Mtwara), Kaskazini (Tanga, Manyara, Arusha, Kilimanjaro), Kati (Morogoro, Dodoma na Singida), Nyanda za Juu Kusini (Njombe, Iringa, Mbeya na Ruvuma), Magharibi (Rukwa, Katavi, Tabora na Kigoma), Ziwa Mashariki (Shinyanga, Simiyu na Mara), Ziwa Magharibi (Mwanza, Geita na Kagera), Pemba (Kusini Pemba na Kaskazini Pemba) na Unguja (Mjini Magharibi, Kusini Unguja na Kaskazini Unguja).
Chini ya mkakati huo mpya ambao unatarajiwa kuzinduliwa wakati wowote kuanzia sasa, CHADEMA inatarajiwa kufanya mikutano ya ndani na kuanzisha matawi katika ngazi ya chini kabisa.
Hali hiyo itakifanya chama hicho kufika katika vijiji na maeneo yote nchini na hivyo kuwa na mtaji mkubwa kwa ajili ya uchaguzi mkuu mwaka 2015.
Chini ya mkakati huo mpya, kila kanda itakuwa na uwezo wa kuendesha operesheni zake bila kutegemea makao makuu ya chama hicho.
Habari kutoka ndani ya serikali na CCM, zilisema kuwa mkakati huo wa CHADEMA, umesababisha serikali kutumia mbinu kupunguza kasi ya chama hicho.
Moja ya mbinu hiyo inatajwa kuwa ni kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano ya vyama vya siasa kwa kisingizio cha kuibua vurugu.
Hofu hiyo ya maandamano imetokana na mkakati wa CHADEMA kutaka kupeleka kwa wananchi hoja binafsi za wabunge wake zilizozuiliwa bungeni ili wajue ukweli na kueleza jinsi muhimili huo wa dola ulivyotumia ubabe kuzizima.
Katika mkutano wa kumi uliomalizika hivi karibuni mjini Dodoma, Bunge lilizuia kujadili hoja binafsi ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, iliyohusu kuboresha huduma ya maji katika jiji la Dar es Salaam.
Hoja nyingine zilizozuiliwa ni ya Mbunge wa Iringa, Peter Msingwa na Joshua Nassari wa Arumeru Mashariki.
Mkakati wa kutaka kuzuia mikutano na maandamano ya CHADEMA, ulitangazwa pia na Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akifungua mkutano wa mwaka wa wakuu wa Jeshi la Polisi nchini, mjini Dodoma mwanzoni mwa wiki.
Bila kutaja chama lengwa, Kikwete alilitaka Jeshi la Polisi nchini kubabiliana na maandamano na mikutano, kwa madai kuwa ni kati ya vichocheo vya vurugu nchini.
Kikwete alisema hivi karibuni suala la maandamano nchini limechukua sura mpya na kuonekana kama la kawaida wakati yanasababisha uvunjifu wa amani katika baadhi ya sehemu.
Kwa mujibu wa habari hizo, mkakati mwingine wa kupunguza kasi ya CHADEMA uko bungeni ambapo kiti cha spika katika mkutano wa kumi wa Bunge mjini Dodoma, kilitumia ubabe kuzima hoja za msingi za wabunge wa CHADEMA.

Tanzania Daima

No comments:

Post a Comment