Monday, February 4, 2013

Mbowe: Uchaguzi wa madiwani Arusha ufanyike haraka


Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia  na Maendeleo  (Chadema), Freeman Mbowe, ameitaka serikali kuitiusha haraka uchaguzi wa kata tano za Jimbo la Arusha Mjini, kabla ya kuanza kutumia nguvu kubwa ya kushinikiza  uchaguzi huo.
Alitoa kauli hiyo jana eneo la Burka jijini Arusha,  alipokuwa akishuhudia Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, akikabidhiwa kiwanja cha hekari 3.1 na kampuni ya wanasheria ya Mawalla kwa ajili
ya ujenzi wa hospitali ya mama na mtoto aliyoahidi wakati wa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.
 
Alisema inashangaza kuona serikali haitekelezi utawala wa kisheria na kukiuka katiba ya nchi mpaka ishituliwe kwa maandamano.
 
“Mimi nasema serikali ifanye haraka kuitisha uchaguzi, la sivyo tutalianzisha libeneke lisilo na mwisho Arusha kwa sababu haiwezekani wananchi wakose uwakilishi karibu miaka miwili,  huu ni uhuni wa wazi,” alisema Mbowe.
 
“Lakini katika hili tunaona ni uhuni wa wazi sababu sheria ipo wazi, ni siku 90 inatakiwa uchaguzi uitishwe, sasa hii kali miaka karibu miwili na hii ni hofu,” alisema na kuongeza: “Tutazichukua kata hizi tukirudia uchaguzi,
lakini sisi hatuna hofu hata tukikosa ili mradi wananchi wapate uwakilishi.”
 
Kuhusu ununuzi wa kiwanja hicho, alipongeza kampuni hiyo kwa moyo wa uzalendo wa kujitoa na kuwaomba watu wengine wenye mapenzi na maendeleo kusaidia harakati za siasa na maendeleo.
 
“Watu waache woga wa kujitokeza kusaidia harakati za maendeleo  na waache kuona kazi ya wanasiasa ni vurugu kama wanavyomsema Lema. Lakini vurugu za Lema zinasaidia kuwaamsha watendaji serikalini na hii ndiyo
kazi ya mwanasiasa,” alisema.
 
Naye Lema, alisema eneo hilo alianza kulitafuta baada ya uchaguzi na sasa anashukuru kulipata na kuwa limegharimu Dola za Marekani  300,000 (Sh. milioni 480). 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment